Dabi ya Simba na Yanga kuchezeshwa na waamuzi kutoka Misri

uyjh

Chanzo cha picha, CITIZEN

Muda wa kusoma: Dakika 2

Bodi ya Ligi kuu ya soka Tanzania bara TPLB imetangaza maofisa wa mchezo wa watani wa jadi kutokea Kariakoo kati ya Young Africans Sc na Simba Sc, utachezeshwa na waamuzi wa kigeni kutoka nchini Misri.

Kwa mujibu wa taarifa ya Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, Mwamuzi wa kati atakuwa Amin Mohamed Amin Omar kutoka Misri akisaidiwa na Mahmoud Ahmed Abo El Regal kama Mwamuzi msaidizi namba moja na Samir Gamal Saad Mohamed ambaye atakuwa msaidizi namba mbili, wote kutokea Misri.

Ahmed Mahrous naye kutoka Misri atakuwa afisa wa nne wa kigeni katika mchezo huo. Mtathimini waamuzi atakuwa ni Alli Mohamed kutoka Somalia.

Kamishna wa mchezo huo utakaopigwa Juni 25, 2025 majira ya jioni katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, anatarajiwa kuwa Salim Omary Singano, kutokea Tanzania.

Huku kukiwa na masuala lukuki ya kupambania ikiwemo ubingwa na fedha tasilimu, pia ni nadra kwa Yanga na Simba kupambana katika mchezo wa kukamilisha msimu wa Ligi Kuu Bara huku zote mbili zikiwa na nafasi ya kutwaa ubingwa tangu kuanzishwa tena kwa mfumo ligi ya nyumbani na ugenini mwaka 1982.

Misimu mingine tisa ya kusisimua ambayo kama ilivyo mwaka huu ubingwa uliamuliwa siku ya mwisho kabisa ya kufunga msimu:

Mwaka 1986 Tukuyu Stars waliibuka wababe dhidi ya Simbajapo iliwabidi kungojea uamuzi wa Mahakama Kuu kuhusu kesi ya Simba kupokwa alama 2 kwa kumchezesha mchezaji Francis Mwikalo isivyo halali. Msimu uliofuata, 1987 Yanga wakaibuka na kicheko dhidi ya Majimaji ya Songea.

Kunako 1988 ubingwa ulikwenda Tanga Coastal Union ikifaidika na Yanga kufungwa na Simba, iliyoepuka kushuka daraja licha ya wagosi wa kaya kuchapwa na African Sports.

Miaka miwili baadaye 1990 ikawa zamu ya Simba kucheka siku ya mwisho wakiichapa African Sports na Mkwakwani Tanga.

Mwaka 1999 na 2000 ilizaa shangwe na vifijo katika mashamba ya miwa Tuliani Morogoro kwa Mtibwa kuwatambia Yanga siku ya mwisho ya ligi katika uwanja wa Jamhuri

Mwaka 2003 Simba iliyotinga dimbani kumaliza msimu ikiwa ya 3, iliibuka bingwa kwa sababu wapinzani wao walipata matokeo mabaya.

Msimu uliomalizika 2011 ulizua shangwe kwa Yanga kutwaa ubingwa situ siku ya mwisho ya msimu bali pia kwa faida ya tofauti ya magoli ya kufunga na kufungwa dhidi ya mtani Simba. Hali hiyo ikajirudia tena mwaka 2017 Yanga wakinufaika tena kwa magoli.

Baada ya miaka minane hali hiyo imerejea. Fauka ya hayo, hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa mechi yoyote ya ligi za ndani ya vilabu Tanzania bara, kuchezeshwa na waamuzi wa kigeni.