Yanga yaweka rekodi Afrika, taji la kwanza Ligi Kuu kileleni Kilimanjaro

Na Alfred Lasteck

.

Chanzo cha picha, Yanga

Klabu ya Yanga ilitwaa taji lake la 30 la Ligi Kuu Tanzania Bara wakiandika historia ya aina yake, huku wakiwa wametwaa kombe hilo mara tatu mfululizo.

Baada ya ubingwa unaoongeza historia ya klabu hiyo yenye maskani yake jijini Dar es Salaam, sasa wameweka rekodi mpya Afrika kwa kuwa klabu ya kwanza kupandisha taji lake katika kilele cha mlima Kilimanjaro, mrefu zaidi barani Afrika.

Mabingwa hao wanatazamiwa kushuka dimbani kesho katika uwanja wa New Amaan Complex kuvaana na kikosi cha Azam kwenye fainali ya Kombe la Shirikisho nchini Tanzania.

Safari ya kombe kwenda kilele cha Mlima Kilimanjaro

Kombe hilo lilifika kilele cha mlima huo jana ijumaa na kuwa klabu ya kwanza kuweka rekodi hiyo.

.

Chanzo cha picha, Yanga

Kwa mujibu wa Mamlaka za hifadhi ya Mlima Kilimanjaro, Kombe hilo lilipita kwenye vituo kadhaa na hatimaye jana kufika kileleni likiitangaza Yanga, na Taifa la Tanzania.

Kampuni ya waongoza watalii, Zara Tours wamesema Yanga wameona umuhimu wa Kilimanjaro na njia nzuri ya kusherehekea mafanikio.

Mahasimu wao Klabu ya Simba nao waliwahi kushiriki katika kupanda kwenye mlima huo kwa kupeleka “kibegi chenye jezi” kileleni na kufanya uzinduzi wa jezi yao ya msimu.

Rais wa Klabu ya Yanga, Hersi Said aliiambia BBC kuwa kama klabu ya Yanga wameendelea kupata mafanikio makubwa kwa kutwa taji la ligi kwa mara ya tatu mfululizo na kuwafanya mabingwa kwa mara ya 30, rekodi ambayo haijawahi kufikiwa na klabu yoyote nchini Tanzania.

Hersi alisema, “Tumeamua kusherekea mafanikio yetu katika moja ya kitovu cha utalii Afrika. Tumepeleka kombe kwenye kilele cha juu zaidi Afrika na dunia imeona kwa kiasi gani Yanga imepiga hatua.

Rekodi 2023/24 zilizoipeleka yanga kilele cha Kilimanjaro

  • Imeshinda mechi zote ilizocheza katika uwanja wa nyumbani
  • Imeshinda mechi 26 katika msimu huu
  • Imepata pointi 80
  • Imeifunga kila timu iliyoshiriki ligi msimu huu
  • Pia imefunga magoli 71 na kuruhusu 14 pekee msimu mzima
  • Imetoa mfungaji bora wa ligi, magoli 21- ambaye ni Aziz Ki (raia wa Burkina Faso)

Kombe Kilimanjaro lawavuruga mashabiki Simba, Yanga

Katika harakati za tambo kati ya mashabiki wa klabu hizo kongwe, Ali Abeid ambaye ni shabiki wa Yanga alisema, “Yanga ndio klabu bora na yenye rekodi bora ya kisoka Afrika Mashariki na Kati”

.

Chanzo cha picha, Yanga

Kwa upande wake, Juma Shabani alitamba kwa kusema, Simba inafahamika kote Afrika kwa kuwa timu kutoka Tanzania iliyofika mara nyingi hatua ya juu ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika.

Nani anapaswa kuungwa mkono kati ya hao mashabiki wawili?

Baada ya Yanga kutwaa ubingwa wa Ligi wamefuzu moja kwa moja kushiriki Klabu Bingwa Afrika msimu ujao. Vilevile Azam iliyoshika nafasi ya pili.

Simba kwa miaka ya hivi karibuni imekuwa na mwendelezo wa kushiriki Kombe la Klabu Bingwa lakini msimu ujao watashiriki Kombe la Shirikisho kwasababu walishaka nafasi ya tatu kwenye ligi ya msimu wa 2023/24 iliyoisha hivi karibuni.

Nini kimechangia mfululizo wa mafanikio ya Yanga

Meneja wa timu ya Yanga, Walter Harrison anasema, mafanikio yanatokana na uongozi ulio bora, kikosi bora cha wachezaji, benchi la ufundi na mashabiki ambao siku zote wako na klabu yao.

Harrison anasema, “Siku zote tumekuwa tukijiandaa vyema kwaajili ya kila mchezo na kuheshima wapinzani wetu. Timu imekuwa kitu kimoja na matokeo yake ndicho tunachokiona, mataji na heshima ya klabu iko juu…

“…ni ndoto yetu pia kushinda taji la Shirikisho kesho dhidi ya Azam na mataji mengine mbeleni, ” anasema Meneja huyo.

Azam, Yanga fainali kesho Zanzibar

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Yanga inashuka dimbani kesho kutetea taji la Kombe la Shirikisho.

Mabingwa hao wa kihistoria Tanzania watakabiliana na matajiri wa Azam kwenye dimba la New Amaan Complex uliopo visiwani Zanzibar.

Kuelekea mchezo huo, Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi amesema, “Yanga ndiyo timu inayocheza soka safi zaidi Tanzania kwa sasa, ‘and this is fact’."

Kwa upande wake Kocha wa Azam FC, Bruno Ferry amesema wamejiandaa vizuri kupambana na Yanga. Ferry amesema wataingia bila shinikizo na wamewaandaa wachezaji wao kucheza bila shinikizo.

Beki wa Yanga, Ibrahim Abdullah 'Bacca' amesema wamejiandaa vizuri kupambania ubingwa wa tatu mfululizo wa michuano ya CRDB Bank Federation Cup dhidi ya Azam FC.

"Tuko vizuri, tumejipanga kuhakikisha hatupotezi na tunatetea taji letu...mazoezi ya mwisho leo yatasema.”

Naye Kiungo wa Azam FC, Feisal Salum amesema wao kama wachezaji wanatambua ubora wa Yanga hivyo wataingia dimbani kwa kuiheshimu. "...tunawaheshimu na sisi waje kwa kutuheshimu, wakifanya makosa tutawaadhibu.”