Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Vita vya Ukraine: Zijue boti zisizo na nahodha zinavyotumika
Kwa mujibu wa Moscow mashambulizi mawili ya boti zisizo na nahodha za Ukraine dhidi ya meli za kivita za Urusi yamezimwa. Jeshi la wanamaji la Ukraine limekanusha kuhusika na mashambulizi hayo.
Boti zisizo na nahodha zimekuwa zikitumiwa na Ukraine na Urusi tangu kuanza kwa vita. Ni aina mpya ya teknolojia ya boti zisizo na nahodha ambazo zimekuwa zikishika kasi katika Bahari Nyeusi.
Boti zisizo na nahodha zikoje?
Ni boti ndogo zisizo na mshika usukani. Tofauti na ndege zisizo na rubani, hizi hufanya kazi juu au chini ya maji. Zina majina mengi huitwa, ikiwa ni pamoja na meli zisizo na nahodha au ndege zisizo na rubani za baharini.
Zipo katika maumbo na ukubwa tofauti tofauti, na hutumiwa kwa kazi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na ufuatiliaji wa mazingira. Zinatumika kwa madhumuni ya kijeshi pia - kama vile kusafisha mabomu ya ardhini, kuchunguza au kulipua meli za adui.
Boti au meli hizi zisizo na nahodha zilianza kuonekana tangu kuanza kwa vita. Moja iliripotiwa kusombwa na maji katika ufuo wa Crimea unaokaliwa na Urusi.
Hufanyaje kazi na zinagharimu kiasi gani?
Vitu vya kawaida vya boti hizo ni pamoja na vilipuzi na kamera ambazo hupeleka picha kwa mtu anayezidhibiti.
‘Huongozwa kwa mbali na binadamu hadi kufika eneo la kushambulia,’ anaelezea Sidharth Kaushal kutoka taasisi ya Rusi. Anaongeza, ‘baadhi ya meli za Ukraine zisizo na nahodha zimetengenezwa kutokana na ufadhili kutoka michango ya watu wa kawaida. Kwa kawaida hutengenezwa kwa matumizi ya kibiashara - badala ya kijeshi.’
Vyombo vya habari vya Urusi na wanablogu wamedai - Urusi pia ilitumia boti hizo wakati wa shambulio kwenye daraja katika mji wa bandari wa Odesa. Hata hivyo, BBC haijaona ushahidi wowote wa kuunga mkono hili.
Ni boti ngapi zisizo na nahodha kila upande unamiliki? Hazijulikani. Pia, haijulikani ni kiasi gani zinagharimu, lakini ndege moja isiyo na rubani iliyotangazwa na serikali ya Ukraine inagharimu pauni 197,000.
Meli zisizo na rubani pia zinaweza kutumwa haraka - bila hitaji la wafanyakazi waliofunzwa kikamilifu.
Zilianza kutumika lini dhidi ya Urusi?
Utafiti wa BBC unaonyesha - Ukraine imefanya takribani mashambulizi 10 kwa kutumia meli zisizo na nahodha - zikilenga meli za kijeshi, kituo cha jeshi cha wanamaji wa Urusi huko Sevastopol, na bandari ya Novorossiysk. Kwa kuzingatia taarifa za mamlaka ya Urusi na Ukraine, na ripoti za vyombo vya habari vya ndani.
Vyanzo vya ulinzi vya Ukraine vimeiambia CNN - boti zisizo na nahodha pia zilitumika katika shambulio kwenye daraja la Kerch mwezi Julai.
Mwezi Mei, picha ziliibuka zikionyesha meli zisizo na nahodha zikikaribia meli ya kijasusi ya Urusi iitwayo Ivan Khurs, lakini haijulikani ikiwa meli hiyo ilishambuliwa.
Urusi inasema tukio hilo lilitokea maili 90 (140km) kaskazini mwa Uturuki - karibu maili 120 (193km) kutoka pwani ya Ukraine. Hii inaonyesha kwamba boti hizo zinaweza kusafiri umbali mrefu.
Zina athari gani kwenye vita?
Ukraine kuzitumia kunaashiria enzi mpya ya vita vya majini. Mbinu hiyo inaleta hatari inayoongezeka kwa Urusi, kwa mujibu wa wachambuzi.
Ikilinganishwa na manowari, boti hizo ni ngumu kugundulika kwenye rada kwa sababu husafiri chini ya maji na hazina kelele sana.
Ukraine haina jeshi kubwa la wanamaji, boti za aina hiyo zimeizuia Urusi kuchukua udhibiti kamili wa Bahari Nyeusi, anasema Katarzyna Zysk, profesa katika Taasisi ya Mafunzo ya Ulinzi ya Norway.
Shambulio dhidi ya kituo cha jeshi la wanamaji la Urusi huko Sevastopol, Oktoba 2022, lilikuwa la kwanza katika historia kutumia boti na ndege zisizo na mwendeshaji.
Takribani meli tatu za Urusi ziliharibiwa katika shambulio hilo, kulingana na GeoConfirmed, shirika linalochambua picha za satelaiti na vyanzo vingine vya picha. Tangu wakati huo, Urusi imeimarisha ulinzi karibu na kambi hiyo kulingana na picha za hivi karibuni za satelaiti zilizoonekana na BBC.
"Bado sio mapinduzi," anasema Prof Zysk. "Bado tuko katika hatua ya majaribio".
Hata hivyo, mkakati wa Ukraine umevutia kimataifa, na "unasukuma majeshi mengine ya majini kuunda mifumo ya aina hii," anaongeza.