Tazama :Kijiji kizima kilivyosombwa na mafuriko mpaka baharini Libya

Vikosi vya uokoaji nchini Libya vinatatizika kuopoa miili ya waathiriwa ambayo imesombwa na maji mithili ya tsunami mpaka baharini.

Takribani watu 2,300 wamepoteza maisha, kulingana na mamlaka ya ambulensi huko Derna, jiji lililoathiriwa zaidi.

Mabwawa mawili na madaraja manne yaliporomoka huko Derna, na kuzamisha sehemu kubwa ya jiji wakati kimbunga Daniel kilipopiga Jumapili.

Takribani watu 10,000 wameripotiwa kupotea, Shirika la Red Crescent linasema, na idadi ya vifo inatarajiwa kuongezeka zaidi.

Baadhi ya misaada imeanza kuwasili, ikiwemo kutoka Misri, lakini juhudi za uokoaji zimetatizwa na hali ya kisiasa nchini Libya, huku nchi hiyo ikigawanyika kati ya serikali mbili zinazohasimiana.

Marekani, Ujerumani, Iran, Italia, Qatar na Uturuki ni miongoni mwa nchi ambazo zimesema zimetuma au ziko tayari kutuma misaada.

Picha za video zilizorekodiwa gizani Jumapili zinaonesha mto wa maji ya mafuriko ukitiririka jijini huku magari yakidunda bila msaada katika mkondo huo.

Kuna visa vya kuhuzunisha vya watu kusombwa hadi baharini, huku wengine waking'ang'ania juu ya paa ili kuokoa maisha.

"Nilishtushwa na kile nilichokiona, ni kama tsunami," Hisham Chkiouat, kutoka serikali yenye makao yake mashariki mwa Libya, alisema.

Aliiambia BBC Newshour kwamba kuanguka kwa moja ya mabwawa kusini mwa Derna kumesababisha sehemu kubwa za jiji hilo kuingia baharini.

"Kitongoji kikubwa kimeharibiwa - kuna idadi kubwa ya waathirika, ambayo inaongezeka kila saa."

Kasim Al-Qatani, mfanyakazi wa kutoa misaada katika mji wa Bayda, alikiambia kipindi cha Newsnight cha BBC kuwa ilikuwa vigumu kwa waokoaji kufika Derna kwani njia nyingi kuu za kuingia mjini humo "zimekosa huduma kwa sababu ya uharibifu mkubwa".

Uchunguzi umeanzishwa ili kujua ni kwa nini mafuriko yalisababisha uharibifu huo, alisema, akiongeza kuwa Dinar ya Libya 2.5bn (£412m; $515m) itatolewa kusaidia kujenga upya Derna na mji wa mashariki wa Benghazi.

Miji ya Soussa, Al-Marj na Misrata pia iliathiriwa na dhoruba ya Jumapili.

Wataalamu wa uhandisi wa maji waliiambia BBC kwamba kuna uwezekano bwawa la juu, karibu kilomita 12 (maili nane) kutoka jiji, lilishindwa kwanza, na kusababisha maji yake kupita chini ya bonde la mto kuelekea bwawa la pili, ambalo liko karibu na Derna, ambapo vitongoji vilifurika. .

"Mwanzoni tulifikiri kuwa ni mvua kubwa lakini usiku wa manane tulisikia mlipuko mkubwa na bwawa lilikuwa likipasuka," Raja Sassi, ambaye alinusurika pamoja na mke wake na binti yake, aliliambia shirika la habari la Reuters.

Mwandishi wa habari wa Libya Noura Eljerbi, ambaye anaishi Tunisia aliiambia BBC kwamba aligundua tu kwamba karibu jamaa zake 35 ambao wote waliishi katika jengo moja la ghorofa huko Derna walikuwa bado hai baada ya kuwasiliana na timu ya uokoaji ya eneo hilo.

"Nyumba imeharibiwa lakini familia yangu ilifanikiwa kutoka kabla hali haijawa mbaya zaidi. Wako salama sasa," alisema.

Bw Qatani alisema hakuna maji safi ya kunywa huko Derna, na ukosefu wa vifaa vya matibabu.

Aliongeza kuwa hospitali pekee ya Derna haiwezi tena kuchukua wagonjwa kwa sababu "kuna zaidi ya maiti 700 zinazosubiri hospitalini na sio kubwa".

Libya imekuwa katika machafuko ya kisiasa tangu mtawala wa muda mrefu Kanali Muammar Gaddafi kupinduliwa na kuuawa mwaka 2011 na kuacha taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa mafuta likigawanyika vilivyo na serikali ya mpito, inayotambulika kimataifa inayoendesha shughuli zake kutoka mji mkuu, Tripoli, na nyingine mashariki.

Mwandishi wa habari wa Libya Abdulkader Assad alisema mkanganyiko kuhusu hili unatatiza juhudi za uokoaji.

"Una watu ambao wanaahidi msaada lakini msaada hauji," aliiambia BBC. "Hakuna timu za uokoaji, hakuna waokoaji waliofunzwa nchini Libya. Kila kitu katika miaka 12 iliyopita kilihusu vita."

Lakini licha ya mgawanyiko huo, serikali mjini Tripoli imetuma ndege yenye tani 14 za vifaa vya matibabu, mifuko ya mwili na zaidi ya madaktari 80 na wahudumu wa afya.

Brian Lander, naibu mkurugenzi wa masuala ya dharura katika Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa, alisema shirika hilo lilikuwa na chakula cha familia 5,000.

Derna, takribani km 250 mashariki mwa Benghazi kando ya pwani, imezungukwa na vilima vya karibu vya eneo lenye rutuba la Jabal Akhdar.

Mji huo ulikuwa ambapo wapiganaji wa kundi la Islamic State walijijenga nchini Libya, baada ya Gaddafi kuanguka. Walifukuzwa miaka kadhaa baadaye na Jeshi la Kitaifa la Libya (LNA), vikosi vinavyomtii Jenerali Khalifa Haftar ambaye ni washirika wa utawala wa mashariki.

Jenerali huyo mwenye nguvu alisema maafisa wa mashariki kwa sasa wanatathmini uharibifu uliosababishwa na mafuriko ili barabara ziweze kujengwa upya na kurejesha umeme kusaidia juhudi za uokoaji.

Tovuti kuu ya habari ya Al-Wasat nchini Libya imesema kuwa kushindwa kujenga upya na kudumisha miundo mbinu ipasavyo huko Derna baada ya mzozo wa miaka mingi ndio chanzo cha idadi kubwa ya vifo.

"Machafuko ya usalama na ulegevu wa mamlaka ya Libya katika kutekeleza ufuatiliaji wa karibu wa hatua za usalama [za mabwawa] ulisababisha maafa," ilimnukuu mtaalamu wa uchumi Mohammed Ahmed akisema.