Rwanda: Kurejea kwangu nyumbani miaka 30 baada ya mauaji ya kimbari

Niliondoka nyumbani kwetu nchini Rwanda, nchi yangu ya kuzaliwa, miaka 30 iliyopita nikiwa na umri wa miaka 12 – mimi na familia yangu tukikimbia madhila na maovu ya mauaji ya kimbari ya 1994.

Nimelelewa nchini Kenya na Norway na kisha nikapata makao ya kudumu jijini London Uingereza. Mara nyingi niliwazia hali ingekuwa vipi ikiwa nitarejea nyumbani na kutazama jinsi taifa lilivyopona na raia wenzangu walivyopata maridhiano na uwiano.

Nilipopata nafasi hii ya kusafiri ili kuandaa Makala haya maalum kuhusiana na suala hili, nilikuwa mwenye furaha ila pia nilihisi kuwa na wasiwasi kuhusu kile nitakachokipata kule – jinsi nitakavyohisi.

Tahadhari: Baadhi ya maelezo katika taarifa hii huenda yakawaathiri wasomaji.

Nimeishi na kiwewe cha akilini na hisia kutokana na matukio ya 1994, ambayo huchochewa wakati wowote, bila kujua.

Kama raia wengi wa Rwanda, Niliwapoteza baadhi ya jamaa zangu. Katika muda wa siku 100, watu laki nane (800,000) waliuawa na makundi ya wapiganaji wenye itikadi kali kutoka jamii ya Wahutu. Waliwalenga Watutsi, na vile vile wapinzani wao kisiasa, bila ya kujali kabila lao.

Vikosi vya kijeshi ambavyo vilijumuisha Watutsi wengi na vilivyochukuwa mamlaka baada ya mauaji hayo ya kimbari, vimeshutumiwa pia kwa madai ya kuwauwa maelfu ya Wahutu nchini Rwanda kama hatua ya kulipiza kisasi.

Hisia zilinijaa moyoni nilipotua katika mji mkuu Kigali. Furaha ya kuisikia lugha yangu ya Kinyarwanda ikizungumzwa kwa ufasaha kote karibu yangu, ilinijaa. Lakini pia, hali ya kutambua kwamba mara ya mwisho nilipoondoka mji huu, ilikuwa katika hali ya vurugu, na hali hiyo ilisheheni kwa muda, huku mamilioni ya watu wakikimbilia usalama wao ili kuokoa maisha yao.

Katika baadhi ya maeneo ambayo nilitamani kuyaona tena katika ziara yangu hii, nis hula ya msingi ambapo nilisomea na nyumba yetu tulipoishi mjini Kigali – ambapo nilikuwa nimekaa mezani tukila chakula cha jioni kwa Pamoja na jamaa zangu usiku huo wa Aprili 6 1994.

Hapa ndipo tulisikia taarifa kwamba ndege iliyokuwa imembeba Rais ilikuwa imeangushwa kwa kurushiwa kombora – Simu iliyopigwa ilibadilisha mkondo wa maisha yetu kabisa.

Lakini katika hisia zote za hofu nilizokuwa nazo, huzuni niliyojawa nayo nilipokosa kuipata nyumba ambayo familia yangu ilikuwa ikiishi ndani ilinijaa moyoni. Baada majaribio manee kuitafuta , nilikata tamaa na kumpigia mama yangu simu nchini Norway ili aniongoze kuipata.

Hatimaye, nilipofanikiwa na kufika pale. Nilidondokwa na machozi niliposimama mbele ya lango kuu lililokuwa limefungwa . Nilijawa na hisia nyingi nilipokumbuka jinsi tulivyoketi hapa nje nyakati za mchana, kuota jua na kuzungumza na kufurahia tu.

Pia, kumbukumbu za tulivyo ondolewa hapa kwa nguvu katika mazingira magumu ilinijia– nakumbuka tukitakiwa kubeba nguo tatu tu na kisha kuingia kwenye gari na kuanza safari ambayo hakuna mmoja kati yetu alitarajia au kuwazia ingetokea.

Sikumbuki, yeyote kati yetu akizungumza wala kulalamika, ingawa sisi watoto tulikuwa tumebanana na kujazana katika kiti cha nyuma – na hata njaa ilipotukabili vikali, jambo ambalo hatukuwa tumewahi kushuhudia awali.

Katika siku ya sita, tulifahamu fika kwamba hakuna eneo ambalo lilkuwa salama jijini Kigali, kwa hiyo, tukaamua kujiunga na wengine waliokuwa wakiondoka huko- wakijaribu kuuepuka vizuizi vya barabarani ambavyo vilisimamiwa na wapiganaji waliojihami kwa mapanga. Tulihisi kana kwamba mji mzima wa Kigali, maelfu ya watu – sote tukitembea kwa miguu, au kutumia baisikeli na pikipiki, magari, au malori – tulikuwa tunaondoka kwa wakati mmoja.

Tulikuwa tunaelekea kwa shamba la familia yetu lililopo Gisenyi, mji uliopo mpakani kati ya Rwanda na Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika mkoa wa Rubavu.

Wakati huu wa kurejea nyumbani, nilifunga safari hiyo, nikikumbuka jinsi tulivyofanya safari hiyo tukitafuta usalama wetu. Hali barabarani ilikuwa shwari, bila msongamano wa watu au magari, pia hakukuwepo na milio ya risasi au barabara zilizojaa watu wanaotoroka. Wakati huu, hali ilikuwa tulivu, jua lilikuwa limewaka na kwa jumla, siku ilikuwa nzuri.

Nilipata nyumba hii yenye vyumba vitatu vya kulala - ambayo ilikuwa hifadhi kwetu kwa miezi mitatu kwa Pamoja na watu wengine arobaini – ikisimama – japo imesalia mahame tangu tulipoondoka mwezi Julai 1994.

Na nilifanikiwa kukutana na baadhi ya jamaa zangu ambao walinusurika kifo, akiwemo binamu yangu Augustin, ambaye alikuwa mwenye umri wa miaka 10, mara ya mwisho tulipoonana naye mjini Gisenyi.

Nilipokumbatiana naye, nilihisi kana kwamba niko katika ndoto – ndoto ambazo unapoamka usingizini, unatabasamu, moyo ukiwa umejawa na furaha. Kumbukumbu zangu kumhusu ambazo hunipa furaha ni wakati ambapo tulicheza pamoja kwenye mashamba ya mboga yaliyo karibu, tukifurahia kilichoonekana kama wakati wa ziada wa mapumziko baada ya muhula wa kwanza shuleni – hatukuwa na ufahamu wa hatari iliyokuwa inatukodolea macho.

Tulitengana wakati ambapo familia yangu ilikimbilia taifa la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo,(DRC) wakati huo likifahamika kama Zaire.

‘Nilikimbia bila ya wazazi wangu, na kupitia vijijini huku wazazi wangu wakipitia mji wa Gisenyi na kuingia Goma – mji uliopo kwenye upande wa pili wa mpaka nchini DRC,’ alisema.

Siwezi kuwazia jinsi alivyohisi akiwa mtoto na peke yake alipofunga safari hiyo bila wazazi wake na kuishi bila wao katika kambi ya wakimbizi ya Kibumba. Kwangu mimi ,angalau nilikuwa na wazazi wangu tulipotoroka.

Kwa bahati nzuri, baadhi ya majirani ambao walikuwa nao wakati huo, walituma ujumbe kwa wazazi wake kuwaarifu alipokuwa – wakati ambapo simu za rununu hazikuwa zinatumika – nao wakakutana na kusalia katika kambi hiyo ya wakimbizi ya Kibumba kwa miaka miwili.

‘Katika siku za mwanzo, maisha yalikuwa mabaya sana. Kulitokea mlipuko wa kipindupindu na watu wakawa wagonjwa, maelfu wakafariki kutokana na hali mbaya ya usafi ma ukosefu wa lishe bora,’ alinieleza.

Taarifa yake kuhusu yaliyowapata inafanana na yaliyonipata mimi kiasi kidogo. Ninakumbuka wiki za kwanza kama mkimbizi huko Goma, ambapo miili ya watu ilianza kujaa kwenye barabara kabla ya familia yangu kuamuwa kupangia kueleka Kenya na kupata makazi mapya.

Lakini nchini Rwanda kulikuwa na msichana mwingine mwenye umri wa miaka 13 – Claudette Makurumanzi – ambaye alikuwa akiishi katika hali ngumu na kupitia maovu ya mashambulizi kadha katika muda wa siku chache.

Anasema kwamba ni miujiza kwamba walinusurika. Kwa sasa ni mama mwenye umri wa miaka 43, na bibi mwenye wajukuu. Alikubali kunieleza yaliyompata – kwa pamoja na waliotekeleza maovu hayo kwake na wenye kumuwacha na makovu.

Mojawapo ya mashambulizi yalitokea mita chache kutoka kwa eneo ambalo tulikutana la Nyamata – mji uliopo Kusini mashariki mwa Rwanda.

Hili lilikuwa kanisa katoliki ambapo maelfu ya watu walikimbilia kupata hifadhi lakini walishambuliwa na kuuawa, mara nyingi na watu waliokuwa na mapanga.

‘Alikuwa amesimama ndani ya kanisa aliponikata. Alikuwa akiimba aliponikatakata. Alinikata usoni na nihahisi damu ikitiririka usoni mwangu. Aliniamrisha kulala chini kwa tumbo langu. Kisha akanidunga kwa mshale mgongoni. Hadi leo niko na makovu hayo mwilini mwangu.’

Niliposikiza hayo, nilijipata nikijiuliza sisi tuliwezaje kunusurika na jinsi tulivyokuwa wadogo wakati ambapo maisha yetu yaliposambaratishwa.

“Ailinidunga kwa mshale kwa nguvu na kuniacha akidhania kwamba mshale huo ulikuwa umepita na kuingia ardhini, ‘aliendelea kusema.

Alinusurika na kukimbia na kufanikiwa kufikia mgongoni mwake na kuiondoa mshale ambao ulikuwa umeingia ndani kabisa ya mgongo wake.

Alitembea kwa matatizo makubwa, alifika katika nyumba ya Jirani wao, ambapo alidhani atakuwa salama.

Ila alikutana na Jean Claude Ntammbara, afisa wa polisi aliyekuwa wakati huo na umri wa miaka 26.

“Alikuwa akijificha katika nyumba ya mtu aliyetuita na kutufamisha kwamba kuna ‘Inyenzi ‘ kule.” Bwana Ntambara alinieleza.

Neno hili lina maana ya Mende na lilitumiwa na Wahutu wenye itikadi kali na hata katika matangazo ya redio na runinga kuwatambulisha watu kutoka jamii ya Watutsi.

“Nilimpata ameketi kitandani, akiwa na majeraha mabaya na mwili wake ukiwa umejaa damu. Nilipiga risasi kwenye bega ili kummaliza kabisa.”

“Tulikuwa na amri ya kuwamaliza na kutomuwacha yeyote;nilidhani kwamba nilikuwa nimemuuwa.’

Lakini, baada ya muda fulani, alifanikiwa kutoroka katika nyumba hiyo na kutembea peke yake hadi alipokutana na mtu aliyemfahamu ambaye alimtunza na kumtibu majeraha yake.

Wakiwa na makovu haya makubwa na ya ndani mno – yote yakiwa yanayoonkena na yasiyoonekana – watu wanaendelea vipi na maisha?

Bi Mkurumanzi na Bwana Ntambara ni miongoni mwa wale wachache ambao wamefanikiwa kupata njia, ya kukabiliana na hali hiyo vyema.

Nilipotembea kuelekea walipokuwa , nilishangazwa na jinsi walivyokuwa wakicheka pamoja chini ya kivuli cha mti mkubwa wenye majani mengi. Lakini kicheko chao kiliashiria pia jinsi juhudi hizi zimekuwa ngumu kufanikisha.

Nilipomuuliza afisa huyo wa polisi wa zamani, ikiwa alifahamu ni watu wangapi ambao aliwauwa wakati wa mauaji ya kimbari ya Rwanda, alitikisa kichwa chake kuashiria hajui ni wangapi.

Kijana huyu alikamatwa, kushtakiwa na kuhukumiwa kifungo cha miaka zaidi ya 10 gerezani, kwa kuhusika na mauaji hayo.

Badala ya kuhudumu kifungo gerezani, alitekeleza kifungo cha kutumikia jamii baada ya kuonyesha kwamba alikuwa anajutia matendo yake na uwezo wake wa kuomba msamaha.

Alimtafuta Bi Mukarumanzi. Hata hivyo, ilikuwa ni mara ya saba ya yeye kuomba kujadiliana naye ambapo Claudette alikubali kumsamehe.

‘Ilinibidi nikabiliane na matendo yangu, kutambua nilichokifanya kuchangia kwa mauaji ya halaiki na sio tu kwa sababu ya kufuata amri,’alisema.

Alexandros Lordos, mwanasaikolojia mwenye ujuzi wa kimatibabu, ambaye amewafaa wagonjwa nchini Rwanda, anasema kwamba, huhitaji hatua za kupona kwa jumla kwa wote ili kuwezesha kupona kwa mtu binafsi.

“Vurugu lilikuwa la karibu sana kwa watu, ambapo majirani waliwashambulia majirani wao na wanafamilia waliwashambulia jamaa zao. Kwa hilo, kuna hali ya kutojuwa ni nani wa kumuamini ,’ alinieleza.

‘Hali kamili ya kupona, ni kuanza kusahau kitambulisho cha muathiriwa na mtekeleza mauaji.’

Kwa Mukarumanzi, uamuzi wake umekuwa zaidi kuhusu kuiwazia familia yake.

‘Nilihisi kwamba ikiwa ningekufa, bila ya kumsamehe, kisha jukumu hilo lingewaangukia watoto wangu. Ningekufa na huku hisia za chuki zimegubika maisha yangu, basi hatungeijenga upya Rwanda ambayo ninaitakia watoto wangu, ingekuwa Rwanda ambayo nililelewa ndani. Siwezi kuwaridhisha watoto wangu hilo.’

Juhudi za aina nyingine za kutafuta msamaha, na maridhiano zimebuniwa. Mojawapo ni kupitia mfumo unaongozwa na wakristo ambapo aliyetekeleza maovu na muathiriwa wanaletwa pamoja kupitia mifugo – yaani ngombe, ambao ni muhimu sana katika jamii ya Rwanda.

Kwa kufuga ngombe mmoja kwa pamoja- na kujadiliana kuhusu msamaha na maridhiano – wanajenga maisha mema ya siku za usoni pamoja na siku moja, huenda wakafuga ngombe wengi.

Rwanda imepiga hatua ya kuleta pamoja jamii katika nchi hiyo ambayo wakati mmoja ilikuwa imegawanyika kwa misingi ya kikabila – kiasi kwamba, ni kinyume na sheria kuzungumzia masuala ya kikabila nchini humo.

Wakosoaji wamesema kwamba serikali ya sasa, haikubali ukosoaji au maoni yanayokinzana na yao na wanaoipinga, hujipata pabaya kisheria ambapo hufunguliwa mashataka ya kutokubali kwamba mauaji ya kimbari yaliyotokea.

Baadhi ya haki zinakokesana, jambo ambalo huenda likaathiri hali huko, wanasema.

Huenda kuna safari ndefu ili kukabiliana kikamilifu na kilichotokea, lakini hilo linafanyika – nilishuhudia hilo katika safari yangu.

Imechukuwa miongo mitatu, kwa Wanyarwanda kufikia hatua hii ya maridhiano.

Kwangu mimi kurejea, kwa Bi Mukarumanzi na Bwana Ntambara kuishi tena pamoja kama majirani.

Kwetu sote, kupata mahali pa kusitirka hasa kiwewe kinachotukabili kibinafsi na kijumla – eneo ambapo tunaweza kupona, kibinafsi na kijumla.

Kitambulisho kilichonistaajabisha kuhusu Rwanda, ni kwamba japo taifa hili litakuwa moyoni mwangu milele, sipahisi kama nyumbani tena.

Lakini nimetuliza moyo wangu, katika safari hii ambayo imenisaidia kupona makovu na kuniwezesha kukubali nilichokipoteza.

Victoria Uwonkunda ni mwandishi wa BBC na mtangazaji katika kipindi cha Newsday kwenye Idhaa ya BBC World.

  • Imetafsiriwa na Laillah Mohammed na kuhaririwa na Ambia Hirsi