Je kuhesabu kalori ni hatari?

Ni wakati huu wa mwaka ambapo baadhi yetu hufanya maazimio. Kupunguza uzito ili kupata umbo bora ni miongoni mwa maazimio maarufu yanayowekwa na wengi kila mwaka mpya.

Ili kufikia hilo mara nyingi tunaamua kudhibiti ulaji wetu wa chakula na kuongeza mazoezi yetu. Kwa vile nishati iliyo katika chakula hupimwa kwa kalori, wengi wetu hufikiri kwamba tukihesabu na kupunguza ulaji wetu wa kalori, tutafikia lengo letu la kupunguza uzito. Lakini je, hiyo ndiyo njia sahihi, au ni wakati wa kufikiria upya?

Wataalamu wengine hawasemi tu kuhesabu kalori ni njia iliyopitwa na wakati lakini pia wanasema ni hatari, tunapochunguza hapa kupitia historia ya kalori.

Kalori ni nini na neno hilo lilitoka wapi?

Kalori ni nishati, mara nyingi hutumiwa kuelezea thamani ya lishe ya vyakula. Neno hilo linatokana na neno la Kilatini calor, ambalo linamaanisha joto na limetumika kwa zaidi ya karne moja.

"Nicholas Clément alifafanua kalori kama kiasi cha joto kinachochukuliwa kuongeza 1C ya lita moja ya maji katika usawa wa bahari," Dk Giles Yeo, profesa wa neuroendocrinology ya molekuli katika Chuo Kikuu cha Cambridge anaiambia BBC.

Mwanasayansi wa Ufaransa Clément alikuwa wa kwanza kutumia neno hilo katika mihadhara juu ya injini za joto mwanzoni mwa Karne ya 19. Kwa hivyo ufafanuzi wa leo wa kamusi unaosema kalori ni sawa na nishati ya joto inayohitajika kuongeza joto la 1kg ya maji kwa 1C, na sawa na kalori ndogo elfu moja: kilocalorie.

Ugunduzi wake ulikuwa na mchango gani duniani kote?

Uwezo wa kisayansi wa kupima kwa usahihi kalori kwenye chakula ilikuwa jambo la kipekee. "Tumetoka ghafla kutoka kwenye ulimwengu ambao lishe ya mtu fulani iliaminika kuwa inahusiana moja kwa moja na rangi yao, hali ya hewa ambayo waliishi, tabaka lao la kijamii na bila shaka kwa jinsia yao na hakuna lishe mbili zinazoweza kulinganishwa. Lakini ghafla, zililinganishwa," anaelezea Nick Cullather, profesa wa historia na masomo ya kimataifa katika Chuo Kikuu cha Indiana, Bloomington.

Dhana yetu kuhusu chakula ilipitia mabadiliko makubwa. Watu walianza kuona chakula kama muunganiko wa vitu vingi kama protini, wanga, micronutrients, mafuta na kadhalika.

"Mwili huo sasa ulionekana kama injini na chakula kama mafuta yalibadilisha jinsi watu walivyotazama chakula," anasema Cullather.

Katika Karne ya 20 kalori zilianza hata kushawishi sera ya umma. Katika miaka ya 1920 na 1930, Jeshi la Wanamaji la Japan lilitekeleza viwango vya lishe kwa mabaharia wake, kwa kile walichokiona kama kuwafanya kuwa kwenye viwango vinavyolingana na viwango vya Ulaya.

Ngano, nyama, na hasa nguruwe na kuku viliongezwa kwenye chakula cha mabaharia na kutangazwa kwa umma mkubwa wa Wajapani. Bila shaka, chakula cha Kijapani ambacho wengi wetu tunafurahia leo kimetokana na mabadiliko haya ya lishe.

Kwa miongo kadhaa Marekani imetumia kuhesabu kalori ili kubaini ni kiasi gani cha msaada wa chakula kilihitajika kupeleka kwa nchi zinazokabiliwa na ukame, kulingana na Mkataba wa Versailles mwishoni mwa Vita vya Kwanza vya Kidunia . Ulichunguza lishe, kuweka kiwango cha kimataifa mwaka 1935, kupendekeza mtu mzima anapaswa kuwa na kalori 2,500 kwa siku. Sasa kiwango kinachokubalika sana ni kalori 2,500 kwa mwanaume na kalori 2,000 kwa mwanamke kwa siku.

Kwa nini wataalam wengine wanasema kuhesabu kalori kumepitwa na wakati?

Wataalam wengine wanasema kuhesabu kalori kumepitwa na wakati na hii ndio sababu yao wanaoyoisimaia.

Hata kama vyakula tofauti vyenye thamani sawa ya nishati, vinaweza visitoe faida sawa za kiafya au virutubisho vya lishe. Kwa mfano - glasi ya maziwa ina kalori 184 na glasi sawa ya bia ina chini, kwa kalori 137.

"Kwa kweli hatuli kalori; tunakula chakula na kisha mwili wetu kufanya kazi ilikupata kalori kutoka kwenye chakula. Kulingana na aina ya chakula unachokula, karoti, donati au nyama mwili wetu unapaswa kufanya kazi kwa viwango tofauti ili kutoa kalori,” asema mtaalamu wa chembe za urithi Giles Yeo.

Lebo tunazoona katika vyakula vinavyouzwa kwenye maduka makubwa (supermarkets) hutufahamisha kuna kiwango gani cha kalori kwenye chakula lakini hazitakupa dalili ya kiasi gani mwili wetu utaweza kunyonya au kupata kalori hizo kutoka kwneye chakula hicho.

"Kwa kila kalori 100 za protini tunazokula, mwili utachukua kalori 70 pekee," anaongeza. "Mafuta kwa upande mwingine yana nishati nyingi sana na ni hifadhi yenye ufanisi sana ya mafuta. Kwa kila kalori 100 za mafuta tunazokula, tunapata kalori 98 hadi 100 za mafuta," anasema Yeo.

Kw akifupi ni kwamba ikiwa unakula kalori 100 za chips utapata kalori nyingi zaidi kuliko ikiwa unakula kalori 100 za karoti. Yeo anasema kuhesabu kalori kama mpango wa lishe hauna maana, isipokuwa muhimu ni kuzingatia aina ya chakula unachokula.

Kuhesabu Kalori ni hatari?

"Ushughulikiaji huu wa kalori huwaathiri watu," anaonya Adrienne Rose Bitar, mtaalamu wa historia na utamaduni wa chakula na afya wa Marekani katika Chuo Kikuu cha Cornell, New York, ambaye anapinga kuhusu watu kufuatilia kupindukia kuhusu kalori mwili na kujiingiza kwenye mipango ya kupunguza kalori kunaweza kuleta matatizo.

"Tofauti na mlevi ambaye anaweza tu kuacha, huwezi kuacha kula chakula. "Matatizo mengi ya kula kama vile anorexia, bulimia, orthorexia huanza na programu ya kuhesabu kalori isiyo na madhara," Bitar anasema.

Anasema baadhi ya programu hata hushauri watu kuhusu kula vyakula vyenye viwango vya chini vya kalori.

Nini mbadala?

Nje ya tasnia ya chakula, nishati hupimwa sio kwa kalori, lakini kwa joules. Baadhi ya makampuni ya chakula sasa yanatoa thamani ya chakula kwa kwa kutumia kipimo kinachoitwa 'kilojuli'.

Lakini kalori zimeteka mawazo ya umma kiasi kwamba hata wale ambao hawajui maana yek ni nini, wanaweza kuelewa kuwa ulaji wa kalori nyingi ni hatari kwa afya yako.

Baadhi ya wataalam kama Bridget Benelam kutoka British Nutrition Foundation wanatuonya tusiache kula kalori. Anasema licha ya dosari zake zote, kalori ina mchango mkubwa mwilini.

"Unene wa kupindukia pengine ni suala kubwa zaidi la afya ya umma ambalo tunakabiliana nalo sasa. Na hivyo, kuelewa ni nini kinasababisha watu kuwa na uzito mkubwa na unene ni muhimu," anasema Benelam.

Kwa baadhi ya watu wanaopenda kupunguza uzito anasema kuhesabu kalori kunaweza kusaidia sana kupanga lishe ya kupunguza uzito.

"Ni muhimu kuelewa watu wanatumia nini na kalori hizo zinatoka wapi. Kwa hivyo, kwa mfano, tunapoangalia ikiwa watu wanakula vyakula vya mafuta mengi, tunahesabu kuona kalori ngapi wanapata kutoka kwenye mafuta. Kwa hivyo, kwa mtazamo wa kisayansi haya ni mambo muhimu ya kupima na jambo muhimu kuelewa, "anasema.

Nchini Uingereza mamlaka ya Kitaifa ya huduma za Afya (NHS) inasema watu wanapaswa kula kwa viwango stahili vya nishati na aina ya nishati anayotumia na kusema usijali ikiwa mara kwa mara utaishia kula sana, ikipendekeza: "Tumia nishati kidogo siku zinazofuata. "