Ridge Alkonis: Mwanajeshi aliyechochea chuki ya Wajapan dhidi ya Marekani

tt

Chanzo cha picha, SUPPLIED

Maelezo ya picha, Picha ya Ridge Alkonis anayetabasamu akiwa ameketi na familia yake kwenye gari baada ya kuachiliwa
    • Author, Nicholas Yong & Ian Tang
    • Nafasi, BBC News

Hadithi ya Ridge Alkonis ilipoibuka kwa mara ya kwanza tarehe 29 Mei 2021, mwanzoni haikuvutia watu wengi nchini Japan.

Afisa huyo wa Jeshi la Wanamaji la Marekani aliwaua raia wawili wa Japan katika ajali ya barabrani akiwa safarini kuelekea Mlima Fuji - waathiriwa walikuwa mwanamke mwenye umri wa miaka 85 na mkwe wake, mwenye umri wa miaka 54.

Baada ya kukiri kosa la kuendesha gari kiholela, Alkonis alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela mnamo Oktoba 2021. Katika utetezi wake, madaktari wa Jeshi la Wanamaji wa Marekani walisema alikuwa akiugua ugonjwa mkali wa milima wakati wa ajali hiyo. Alihamishiwa chini ya ulinzi wa Marekani Desemba mwaka jana.

Alkonis, aliyezuiliwa katika kituo cha jeshi la wanamaji la Yokosuka kusini mwa Tokyo, alikuwa mtumishi wa hivi punde zaidi wa Marekani aliyekumbana na matatizo ya kisheria. Tangu Makubaliano ya Hali ya Majeshi ya Marekani na Japan (SOFA) yatiwe saini mwaka wa 1960 - kuwezesha kupelekwa kwa vikosi vya kijeshi vya Marekani nchini - kumekuwa na mamia ya visa vya uhalifu vinazohusisha wanajeshi wa Marekani.

Lakini tarehe 13 Januari, ujumbe wa Twitter wa mtangazaji wa CNN Jake Tapper - iliyoambatana na picha ya Alkonis anayetabasamu, 36, akiwa na mke wake na watoto watatu - kuhusu "habari kuu na muhimu" ilisisimua umma wa Japan.

Tapper aliandika: "Leo asubuhi tume ya msamaha ya Marekani iliamuru kuachiwa mara moja kwa Luteni Ridge Alkonis wa jeshi la wanamaji bila masharti ."

Wafuasi wa Ridge Alkonis nchini Marekani

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wafuasi wa Ridge Alkonis nchini Marekani, wakiongozwa na mkewe waliendesha kampeni ya kushinikiza aachiwe huru

Ni watu wachache nchini Japan walijua kwamba mke wa Alkonis Brittany na watetezi wake walikuwa wameongoza kampeni ya kushinikiza aachiliwe huru nchini Marekani. Rais wa Marekani Joe Biden alimkumbatia Brittany Alkonis katika hotuba ya Jimbo la Muungano mwaka 2022, huku Makamu wa Rais Kamala Harris akiwasilisha kesi hiyo na Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida.

Seneta wa Utah Mike Lee pia alimshawishi Alkonis, akimtambulisha Bw Kishida katika tweets nyingi. Alipoachiliwa, aliandika kwenye Twitter: "Japani inadaiwa na familia - na Marekani - kuomba msamaha."

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Ghadhabu ya hatua hiyo ilisambaa mtandaoni nchini Japan. "Kwa nini unasherehekea?" aliuliza mmoja.

Mwingine aliandika kujibu tweet ya Bw Lee: "Je, yeye na familia yake waliomba msamaha (kwa) familia za waathiriwa hao wa Kijapan kwanza?"

Licha ya hasira ya umma na taarifa hiyo kuangaziwa katika vyombo vya habari vya Japani, hakuna afisa wa serikali iliyetoa maoni hadharani kuhusu kesi hiyo. Prof James D Brown wa Chuo Kikuu cha Temple aliambia BBC kwamba hakuna motisha kwa wanasiasa wa Japan au vyombo vya habari vya kawaida kuendeleza kesi hiyo.

"Kufanya hivyo kutakuwa kuzidisha uhasama kati ya Marekani na Japan wakati ambapo kuna utambuzi mkubwa nchini Japan kwamba, licha ya uovu wake, muungano na Marekani bado ni muhimu kwa usalama wa Japan," alisema na kuongeza kuwa kesi kama hiyo "bila shaka itakuwa na athari mbaya".

Licha ya "kuchanganyikiwa wazi" juu ya matokeo ya kesi ya Alkonis, Jeffrey Hall wa Chuo Kikuu cha Mafunzo ya Kimataifa cha Kanda aliongeza: "Kuna hisia ya kukata tamaa miongoni mwa Wajapan kwamba washirika wao wenye nguvu wa Marekani hawawachukulii kama watu sawa na hawatawahi kamwe kufanya hivyo. Tukio la Alkonis linasisitiza kwamba hata vyama na marais wanapobadilika nchini Marekani, hali hii ya ukosefu wa usawa inaendelea."

Uhusiano usio na usawa

Maandamano ya kudai kuondolewa kwa kambi za Marekani ni jambo la kawaida katika Okinawa

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Maandamano ya kudai kuondolewa kwa kambi za Marekani ni jambo la kawaida katika eneo la Okinawa

Hasira inayozidi kuongezeka juu ya uwepo wa jeshi la Marekani nchini Japan ni suala la muda mrefu ambayo ilianza na uvamizi wa kijeshi wa Japan baada ya Vita vya pili vya Dunia. Mwishoni mwa vita, wakaaji wa Marekani waliandika tena katiba ya Japan kwa ile ya kupinga amani na kumpunguza Mfalme kuwa mtu wa mfano.

Kuna takriban wanajeshi 54,000 wa Marekani walio katika vituo 120 kote Japani, 32 kati yao wakiwa Okinawa. Wilaya hiyo pia ina takriban wanajeshi 30,000, wakati ukaribu wake na Taiwan unaifanya kuwa muhimu katika suala la Marekani kuweza kukabiliana na uvamizi wowote wa Wachina kwenye kisiwa hicho kinachojitawala.

Hakuna mahali popote nchini Japan ambapo kutoridhika kwa uwepo wa jeshi la Merika ni wazi zaidi kuliko huko Okinawa, ambapo uvamizi wa Marekani uliisha mnamo 1972 - miongo miwili baada ya Japan iliyobaki. Ghasia za 1970 za Koza, ambapo maelfu ya wakazi wa Okinawa walipambana na wanajeshi, hata huadhimishwa katika jumba la makumbusho.

Takashi Asato aliyestaafu, mwenye umri wa miaka 70, ana kumbukumbu nzuri za maisha ya Okinawa akiwa mtoto katika miaka ya 1960 , huku ndege za kivita zikiruka mara kwa mara na vifaru na lori za kijeshi zikifunga barabara. "Nyingi za fukwe nzuri za mchanga zilikuwa kwa ajili ya matumizi ya kipekee ya jeshi la Marekani - hakuna watu wanaoruhusiwa kuingia ndani. Makazi ya kigeni yalizungukwa na uzio na yalikuwa na nyasi kubwa kwa familia za wanajeshi wa Marekani."

Bw Asato, ambaye mara nyingi aliwapeleka wanajeshi wa Marekani kwenye vituo kama dereva wa basi, aliongeza: "Kulikuwa na mahusiano mengi magumu ya kiuchumi na kiutamaduni kati ya watu wa Okinawa na wanajeshi wa Marekani, lakini ulikuwa uhusiano wenye manufaa kwa pande zote."

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi