'Mafanikio' ya kundi la Wagner nchini Jamhuri ya Afrika ya kati

    • Author, Yemisi Adegoke
    • Nafasi, BBC News, Bangui

Mazingira ya kuvutia yanawakaribisha waumini wanaoingia ndani ya Kanisa la Orthodox la Urusi lililo kwenye barabara yenye mashimo mabaya katika mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR).

Ukiangalia kwa makini, hakuna jambo lisilo la kawaida kuhusu tukio hili la Jumapili asubuhi katika nchi hiyo yenye idadi kubwa ya waumini wa Kikristo.

Lakini kanisa la Saint-André-Apôtre, ambalo liko umbali wa kama dakika 20 kutoka katikati mwa mji wa Bangui, limekuwa likiashiria uhusiano wa kirafiki kati ya Urusi na Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR).

Padri Serguei Voyemawa, kiongozi wa Kanisa pekee la Orthodox la Urusi nchini humo, amevalia vazi jeupe refu lililofunikwa na joho la dhahabu lililopambwa. Anatembea huku na kule akisoma sala na kutikisa kichomea uvumba huku waumini wakifuatilia kila hatua.

Padri Voyemawa awali alisitasita kuhusu ziara yetu. Ilikuja miezi michache baada ya kifo cha mkuu wa Wagner Yevgeny Prigozhin, mwezi Agosti, ambayo imesababisha kuongezeka kwa uchunguzi na wasiwasi juu ya ushawishi wa Urusi unaokua CAR na haswa uwepo wa kundi la mamluki.

Jumla ya wakufunzi 200 wa kijeshi wa Urusi waliwasili CAR baada ya Rais Faustin-Archange Touadéra kuomba msaada wa kukabiliana na makundi ya waasi mwaka 2018.

Lakini kulingana na ripoti ya shirika la uchunguzi The Sentry, kuanzia wakati huo kundila Wagner limechukua fursa ya taasisi dhaifu na jeshi dhaifu kukamilisha "mpango wa kujikita ndani ya serikali".

"Tumewaona wakizingatia nguzo nne: kisiasa, kiuchumi, taarifa za kupotosha na propaganda - na kijeshi," Nathalia Dukhan, mpelelezi mkuu wa The Sentry ambaye kwa miaka kadhaa ameangazia masuala ya nchi, anaiambia BBC.

"Wamekuwa wakiingilia sekta hizi ili kuendeleza maslahi yao ya kifedha na kiuchumi. Katika sekta ya madini, Wagner wamekuwa akitumia jeshi la taifa kuondoa baadhi ya makundi yenye silaha yaliyokuwa yakidhibiti maeneo wanayolenga kwa maslahi yao."

Bi Dukhan anasema mamluki hao wanaendesha "operesheni dhidi ya ugaidi" na wamehusishwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu ikiwa ni pamoja na mauaji ya kiholela, mateso na ubakaji.

Mapema mwaka huu, Uingereza iliorodhesha mtandao huo kama kundi la kigaidi, huku Marekani ikiutaja kuwa "shirika la kimataifa la uhalifu".

Hata hivyo, kwa raia wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, baada ya miaka kumi ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, hali imekuwa ngumu zaidi.

Padri Voyemawa ana shauku ya kusema kwamba uhusiano wake na Urusi ulikuwepo hata kabla ya kuwasili kwa kundi Wagner nchini humo. Alianza kuchangisha fedha kwa ajili ya kanisa hilo mwaka wa 2010 na ujenzi ulianza 2015.

Kusita kwake kujadili siasa ni wazi: "Uhusiano wetu na Moscow ni wa kidini."

Hata hivyo, ananiambia ni kwa kiasi gani mambo yamebadilika tangu jeshi la kukodisha la Urusi lilipowasili: "Sisi Raia wa Jamhuri ya Afriksa ya Kati tuna furaha sana kwa sababu Warusi wako hapa leo na na wamechangia pakubwa kuleta amani na usalama a.

"Kuna amani Jamhuri ya Afrika ya Kati. Ni miaka mitano sasa tunaishi kwa amani, bila vita."

Hisia hii sasa imetoweka katikati mwa mji mkuu wa Bangui, ambapo sanamu ya wanajeshi wa Urusi wanamlinda mwanamke na watoto wake.

Miguuni mwao bouquets zinazofifia kuanzia Agosti hubaki na ujumbe wa "rafiki yetu mkubwa Yevgeny Prigozhin".

Miguuni mwao kuna madhada ya maua yaliyonyauka tangu yalipowekwa mwezi Agost zikiwa na ujumbe unaosema "rafiki yetu mkubwa Prigozhin".

Hisia zinazoiunga mkono Urusi hivi karibuni zimeenea Afrika Magharibi na Kati, ambapo kumekuwa na mapinduzi manane ya kijeshi tangu 2020.

Nchi hizo ikiwa ni pamoja na Mali, Niger na Burkina Faso, zinapinga Ufaransa mamlaka ya zamani ya kikoloni , ambayo wanasema imeshindwa kusaidia ipasavyo katika changamoto za usalama.

Raia wengi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wanaunga mkono hisia hizi.

"Tunahitaji ushirikiano wa kushinda. Ndio maana Warusi wako hapa... ili nchi hii pia iweze kufaidika na maendeleo ya siku zijazo," anasema Emery Brice Ganzaléis, mfanyabiashara wa Afrika ya Kati ambaye hivi karibuni alihamia Bangui baada ya kuishi Ufaransa kwa miongo miwili.

"Ikiwa Urusi itapitisha sera sawa na Ufaransa barani Afrika, hiyo haitafanya kazi."

Bambari, mji mkuu wa mkoa wa Ouaka takriban kilomita 400 (maili 250) kaskazini-mashariki kutoka Bangui, ilishuhudia baadhi ya vurugu mbaya zaidi wakati wa vita na inaonyesha jinsi usalama umeimarishwa polepole.

Njia pekee inayowezekana ya kufika mjini ni kwa ndege inayoendeshwa na Umoja wa Mataifa ambayo husafiri siku tatu kwa wiki. Kuendesha gari hakufai na kunaweza kuchukua siku kwa sababu barabara ni mbovu au hazipo.

Ni ishara wazi ya changamoto zinazoikabili nchi. Vile vile ni uwepo mkubwa wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa, unaojulikana kwa ufupi ka Minusca, na chapa ya biashara ya helmeti za bluu na magari meupe yanaonekana katika mji mzima.

Tangu 2014, Minusca imekuwa na jukumu muhimu la kulinda raia na kufanya kazi na mamlaka, lakini hawajaidhinishwa kuunga mkono upande wowote au kupigana.

Bambari bado ilikuwa chini ya udhibiti wa waasi miaka miwili iliyopita, lakini sasa inashuhudia shughuli nyingi - japo mabaki ya majengo yaliyoteketea bado yameenea katika mji huo.

Amani iliyopo imemruhusu Jovanie Renemeya mwenye umri wa miaka 15 - na maelfu ya watoto waliyoandikishwa kujiunga na makundi yenye silaha - kuwa na matumaini ya maisha bora ya baadaye.

Alitekwa akiwa msichana mdogo pamoja na bibi yake na kupelekwa kufanya kazi katika kambi ya waasi.

"Niliathiriwa na kiwewe kwa muda mrefu," Jovanie anasema kwa upole, akieleza jinsi alivyovumilia mateso mabaya ya kimwili na kuponea chupuchupu kulazimishwa kuolewa na mmoja wa waasi.

Baada ya mwaka mmoja yeye na bibi yake walifanikiwa kutoroka walipokuwa wakienda kuchota maji. Akiwa na wazazi wake, Jovanie sasa ameanza ufugaji wa nguruwe ili kupata pesa na ana ndoto ya kuwa daktari.

Kwa Victor Bissekoin, gavana wa Ouaka, kurudi huku kwa hali ya kawaida haingewezekana bila kuingilia kati kwa wapiganaji wa Wagner.

"Tulipoomba silaha na usaidizi kutoka kwa jumuiya ya kimataifa, walituwekea vikwazo," anaiambia BBC.

"Mnamo 2021 Urusi ilifika [hapa] na ndani ya miaka miwili ilitusaidia kudhibiti karibu nchi nzima, isipokuwa maeneo machache mipakani.

"Nyumba yako inapoungua na unapiga kelele: 'Moto! Moto!' Hujali kwamba maji unayopewa ni matamu au ya chumvi, unachojali ni kuzima moto.

Rais Touadéra anaunga mkono hili na kutetea uwepo wa Wagner nchini humo.

"Ilisemekana kwamba asilimia 80 ya eneo hilo lilichukuliwa na makundi yenye silaha. Leo, kutokana na ushirikiano huu, takwimu hizi zimebadilishwa kabisa," anaiambia BBC wakati wa mahojiano, yaliyotolewa baada ya siku kadhaa za mazungumzo, katika rais ikulu ya Bangui.

Rais huyo mwenye umri wa miaka 66, ambaye alishinda kura ya maoni iliyokumbwa na utata mapema mwaka huu ili kuondoa ukomo wa mihula ya urais, mara nyingi huzingirwa na vikosi vya Wagner, na ni mara ya kwanza tunaona mamluki wakiwa karibu.

Wakiwa wamevalia mavazi ya kijeshi huku nyuso zao zikiwa zimefunikwa, wanajeshi wachache wakiingia na kutoka nje ya jumba hilo.

Wakati wa mahojiano, rais anakiri bado kuna changamoto: "Tunatoa mafunzo kwa vikosi vyetu vya ulinzi ili viwe vikosi vya kitaaluma, tayari kutumwa kutoa huduma ya usalama kwa wananchi."

Alipokabiliwa na swali la madai kwamba mamluki wa Wagner walifanya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na mateso, ubakaji na mauaji ya kiholela, anasema kamati ya uchunguzi imeundwa ili kuthibitisha madai hayo.

Wakosoaji hawajashawishika.

"Ni hatari sana kwa sababu [Kundi la Wagner] liko katika nyanja ya kiuchumi, katika masuala ya usalama, na katika uwanja wa kisiasa, na sasa wanaongoza nchi," Waziri Mkuu wa zamani Martin Ziguele anaiambia BBC.

Hapo awali aliunga mkono ombi la msaada wa Urusi, lakini alikatishwa tamaa walipotuma mamluki a mtandao wa Wagner, "kundi la wahalifu".

"Wako huru kabisa kufanya wanachotaka, kwenda wanakotaka na kuamua wanachotaka," anasema.

Rais Touadéra hakutoa tarehe ya kujiondoa kwa Wagner, akisisitiza umuhimu wa kuzingatia amani kwanza.

Bi Durkhan anashikilia kuwa hii ni sehemu ya mkakati wa Wagner kujipenyeza, na kuifanya nchi kuwa tegemezi.

Ilifikiriwa kuwa uwezo wa Wagner barani Afrika ungefifia baada ya kushindwa kwa Prigozhin katika maasi yake dhidi ya Rais wa Urusi Vladimir Putin na kisha kifo chake, lakini kundi hilo halijasambaratishwa na wapiganaji wake bado hawajaingizwa kikamilifu katika jeshi la Urusi.

"Wamekuwa wakijipanga upya, wakituma watu wao na vifaa vyao," anasema Bi Durkhan. "Mwanzoni, wengine walitafsiri kwmba wanajiandaa kuondoka, lakini haikuwa hivyo. Ilikuwa ni kujipanga upya."

Na bila shaka hali inaendelea kama kawaida nchini CAR. Ishara ya kwanza ni kuonekana wanaume wawili wa Kirusi katika ikulu ya rais ingawa utambulisho wao haukufichuliwa, walisukumwa kwa haraka ili kumuona rais tunaposubiri mahojiano yetu.

Mmoja wao ni afisa wa ngazi ya juu wa Wagner Dmitry Syty, ambaye alionekana kando ya Prigozhin kwenye video ya mwisho aliyoichapisha kabla ya kifo chake na anasemekana kuwa kiongozi mpya wa kundi hilo.

Dalili nyingine ni ishara kote Bangui zinazotangaza Afrika Ti L'Or, bia mpya ya Kirusi.

Katika baa maarufu ya Cave jiji humo, ni dhahiri kuwa kampeni kali ya uuzaji tayari imewavutia baadhi ya wateja.

"Natamani kungekuwa na zaidi [yake] katika Jamhuri ya Afrika ya Kati," anasema Max Franklin wakati akiagiza bia yake ya Africa Ti L'Or, ambayo inachukuliwa kuwa yenye nguvu zaidi kuliko bia ya kienyeji.

Ripoti ya ziada ya Efrem Gebreab.

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi na kuhaririwa na Yusuf Jumah