Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Afghanistan: Mlenga shabaha wa Taliban ambaye sasa anafanya kazi ofisini
Wakati Taliban walipochukua mamlaka nchini Afghanistan Agosti iliyopita, maisha ya wakazi wengi yalibadilishwa.
Katika mwaka uliopita, makumi ya maelfu ya Waafghanistan wamehamishwa nje ya nchi, shule nyingi za sekondari za wasichana zimeamriwa kufungwa na umaskini unaongezeka.
Lakini kwa mara ya kwanza katika zaidi ya miongo minne nchi hiyo pia haijagubikwa na ghasia, huku ufisadi uliokuwa umekithiri hapo awali umepungua kwa kiasi kikubwa.
Mwandishi wa BBC Secunder Kermani alikuwa Afghanistan wakati wa unyakuzi huo, na amerejea kuwapata wale aliokutana nao mwaka jana.
Mdunguaji huyo wa Taliban akizoea maisha mapya
Wakati kundi la Taliban liliposonga mbele kote Afghanistan majira ya kiangazi yaliyopita, na kuteka eneo kutoka kwa serikali ya Afghanistan wakati majeshi ya kigeni yakijiandaa kuondoka, tulikutana na Ainudeen, mpiganaji shupavu wa Taliban, katika wilaya ya kaskazini ya Balkh.
Alikuwa na sura ya upole, yenye ucheshi machoni mwake tulipokuwa tukizungumza nae. "Tunafanya kila tuwezalo kutodhuru raia, lakini ni mapigano na watu watakufa," alisema, nilipomuuliza jinsi ambavyo angeweza kuhalalisha vurugu. "Hatutakubali mfumo mwingine wowote wa Kiislamu hapa Afghanistan."
Mazungumzo yetu yalikuwa mafupi, vita bado vinaendelea na kulikuwa na tishio la mara kwa mara la mashambulizi ya anga ya serikali ya Afghanistan.
Miezi michache baadaye, pamoja na serikali ya Taliban iliyoanzishwa upya, akiwa ameketi mezani kupata mlo wa samaki wa kukaanga karibu na mto Amu Darya unaogawanya Afghanistan na Uzbekistan, Ainudeen aliniambia alikuwa mpiganaji wa Taliban. Alikuwa amewaua makumi ya wanachama wa vikosi vya usalama vya Afghanistan, alikadiria, na alikuwa amejeruhiwa katika matukio 10 tofauti.
Hata hivyo baada ya Taliban kutwaa mamlaka, aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Ardhi na Maendeleo ya Miji katika jimbo la Balkh. Nilipokutana naye katika siku za mwanzo za utawala mpya, nilimuuliza ikiwa alikosa "jihadi" ambayo alikuwa amepigana kwa muda mrefu. "Ndiyo," alijibu kwa ukali.
Sasa, mwaka mmoja baadaye, akiwa ameketi nyuma ya dawati la mbao na bendera kubwa nyeupe na nyeusi ya Emirate ya Kiislamu kando yake, bado anaonekana kuzoea maisha yake mapya. Lakini anasema anatambua umuhimu wa jukumu lake. "Tulikuwa tunapigana na maadui zetu kwa bunduki zetu, shukrani kwa Mungu tuliwashinda, na sasa tunajaribu kuwatumikia watu wetu kwa kalamu zetu." Ainudeen anasema alikuwa na furaha wakati akipigana, lakini pia ana furaha sasa.
Bila kutaka kutambuliwa, wanachama wengine wa Taliban ambao walikuwa mstari wa mbele wanakubali kuwa wamechoshwa na majukumu yao mapya ya ofisi.
Wafanyakazi wengi wanaosimamiwa na Ainudeen waliajiriwa kwa mara ya kwanza wakati wa serikali iliyopita. Hata hivyo katika maeneo mwengine ya jiji hilo, tunasikia baadhi ya malalamiko ya wakazi kuchukuliwa kazi zao na wapiganaji wa zamani wa Taliban.
Ninamuuliza Ainudeen kama anafuzu katika nafasi hiyo.
"Tulipata elimu ya kijeshi na ya kisasa," anasema, "Ingawa tunatoka kijeshi na sasa tunafanya kazi katika uwanja huu, unaweza kulinganisha matokeo na serikali iliyopita, na kuona ni nani aliyetoa matokeo bora. "
Lakini, anaongeza, ikilinganishwa na ugumu wa vita vya msituni, "utawala ni mgumu kuliko mapigano vita vilikuwa rahisi, kwa sababu kulikuwa na uwajibikaji mdogo."
Ni changamoto katika harakati zote za Taliban, huku kundi hilo likihama kutoka kuwa waasi na kwenda kuwa watawala.
Kijiji kilicho kwenye mstari wa mbele kinashukuru kwa usalama bora
Ingawa milipuko mikali ya mabomu katika miji mikubwa ya Afghanistan ndiyo mara nyingi ilikua ikiangaziwa na vyombo vya habari, mzozo mwingi ulipiganwa pia katika maeneo mbalimbali ya vijijini.
Watu wa kawaida walikamatwa kati ya Taliban na Jeshi la Afghanistan, wakiungwa mkono na vikosi vya kimataifa. Wengine walikua na tofauti ndogo kati ya pande hizo mbili hamu yao kubwa ilikuwa tu kuwa na maisha ya amani zaidi.
Tulitembelea kijiji cha Padkhwab katika Mkoa wa Logar, Kusini Mashariki mwa Kabul, muda mfupi baada ya kuwa chini ya Taliban. Wakazi walikuwa na shauku ya kutuonyesha dalili za vita ambavyo hadi wiki chache zilizopita vilikuwa vimeyafunika kabisa maisha yao.
"Hali ilikuwa mbaya sana," alisema Samiullah, mtengenezaji wa vigae. "Hatukuweza kufanya lolote, hata kwenda kwenye maduka au sokoni. Sasa namshukuru Mungu, tunaweza kwenda kila mahali."
Katika vijiji kama Padkhwab maadili ya Taliban yanafanana kwa karibu zaidi na yale ya wakazi wa eneo hilo kuliko maeneo ya mijini. Hata wakati wa serikali iliyopita, wanawake kwa ujumla walifunika nyuso zao wanapokuwa hadharani, na mara chache walijitosa katika soko la ndani.
Tuliporejea wiki iliyopita, baadhi ya matundu ya risasi yanayotia makovu kwenye majengo katikati ya soko yalikuwa yamezibwa, na wakazi bado walionyesha shukrani kwa kuboreshwa kwa hali ya usalama.
"Kabla ya watu wengi, haswa wakulima, kujeruhiwa na kuuawa, wauzaji wa bidhaa za madukani wengi walipigwa risasi," alisema Gul Mohammad, fundi cherehani.
Lakini uchumi wa Afghanistan umekuwa ukiporomoka tangu Marekani ijiondoe nchini humo, kwani ruzuku za kigeni ambazo zilichangia karibu 75% ya matumizi ya umma zilipunguzwa na benki za kimataifa kwa kiasi kikubwa zilisitisha uhamishaji wa fedha, zikihofia kuwa zitakuwa zinakiuka sheria za vikwazo.
Kundi la Taliban linailaumu Marekani kwa kufungia akiba ya benki kuu ya Afghanistan. Wanadiplomasia wa Magharibi wakikosoa mara kwa mara sera za ukandamizaji za Taliban dhidi ya wanawake inamaanisha msaada wowote unaokusudiwa kwa watu wa Afghanistan lazima upite kwenye serikali yao.
Kutokana na mgogoro huo, hapo awali familia za watu wa tabaka la kati katika maeneo ya mijini zimeshuhudia mapato yao yakishuka kwa kiasi kikubwa, kwani wafanyakazi wa sekta ya umma hawakulipwa kwa miezi kadhaa na kisha kukatwa mishahara yao. Wale ambao tayari walikuwa wakiishi maisha ya mkono kwa mdomo wamepata shida zaidi ya kulisha familia zao.
Katika eneo la Padkhwab, kupanda kwa kasi kwa gharama ya bidhaa za kila siku na ukosefu wa kazi ni malalamiko ya kawaida. "Uchumi umeharibiwa, hakuna kazi," alisema Samiullah. "Kila mtu anategemea tu jamaa zao walio nje ya nchi."
"Watu hawawezi kumudu kununua unga, achilia mbali nyama au matunda," aliongeza Gul Mohammad.
Bado, Samiullah alisema, "ni kweli kulikuwa na pesa nyingi wakati huo, lakini tulikabiliwa na dhuluma nyingi," akimaanisha uwepo wa wanajeshi wa serikali ya Afghanistan katika kijiji hicho ambao anawashutumu kuwanyanyasa watu.
Ukosoaji wa wazi wa Taliban unazidi kuwa nadra nchini humo, lakini kwa baadhi, ushindi wao umesaidia kuboresha maisha yao. Wengine wengi, hata hivyo, wanahisi nchi waliyosaidia kujenga inatoweka mbele ya macho yao, na wana wasiwasi sana kuhusu kile ambacho kinabadilishwa.
Mtengeneza maudhui wa Youtube bado anatengeneza vídeo na kuvunja mipaka
Wakati wapiganaji wa Taliban walipoanza kuingia Kabul mwaka jana, wakazi wengi walikuwa na hofu. Kundi hilo kwa miaka mingi limekuwa likifanya mashambulizi ya kujitoa mhanga na mauaji yaliyolengwa mjini humo. Lakini Roeena - msichana ambaye anatengeneza video za YouTube za kijamii, aliamua kutoka na kuzungumza nao.
"Haki za wanaume na wanawake ni sawa," aliiambia BBC akiwa ni mwenye kujiamini mwezi Agosti mwaka jana. Lakini hakuweka wazi kama angeweza kuendelea kufanya kazi hiyo au la. Mwaka mmoja baadae, hali hiyo ya kutokuwa na utulivu bado inaendelea sio tu kwa Roeena, lakini kote nchini.
Kumekuwa na hali ya wasi wasi kimataifa, miongoni mwa Waafghanistan wengi na hata ndani ya safu ya uongozi waTaliban katika uamuzi wa uongozi wa kuamuru shule za sekondari za wasichana kubaki zimefungwa katika sehemu kubwa ya nchi.
Tofauti na wakati wa serikali ya mwisho ya Taliban iliyoanzishwa katika miaka ya 1990, wasichana wadogo wameruhusiwa kuhudhuria madarasa, na vyuo vikuu vimepewa ratiba mpya zinazotenganisha jinsia kuruhusu kundi la sasa la wanafunzi wa kike kuendelea na masomo yao. Lakini watu wenye ushawishi mkubwa na wenye msimamo mkali ndani ya uongozi wa Taliban wanaonekana kusita kuwaruhusu wasichana wachanga kurejea shuleni, na inaonekana maendeleo duni ya haki za wanawake yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 20 iliyopita yanasonga mbele.
Vile vile, wanawake wanaofanya kazi nyingi katika sekta ya umma zaidi ya elimu au sekta ya afya, wameambiwa wasirudi katika ofisi zao. Lakini, idadi ndogo ya wanawake wanaofanya kazi katika biashara binafsi wameweza kuendelea na kazi zao.
Roeena bado anatengeneza video, akisukuma kuondolewa kwa mipaka, akiacha uso wake wazi, lakini akifunika kichwa chake kwa kitambaa.
Anaposafiri kuzunguka Kabul, yeye huvaa kihafidhina zaidi kuliko hapo awali, akiwa amevalia abaya nyeusi inayotiririka kufunika mwili wake. Taliban wameamuru kwamba wanawake lazima wafunike nyuso zao hadharani. Lakini utekelezaji kwa sasa unaonekana kulegalega, na bado ni jambo la kawaida sana katika miji mikubwa kuona wanawake wakifunika nywele zao pekee.
Akizungumzia jinsi maisha yalivyo sasa, akiwahutubia Taliban, Roeena anachagua maneno yake kwa makini. "Wanawake na wasichana wanashika hijabu, wanapaswa kupewa uhuru wote uliohakikishwa na Uislamu. Haki zao zisichukuliwe, waruhusiwe kufanya kazi na kusoma."