Waislamu wa Japani: ‘Hatuwezi kupata makaburi ya kuzika wafu wetu’ - Mwathiriwa

Jumuiya ya Waislamu nchini Japani ni wachache: kuna Waislamu 200,000 pekee katika nchi yenye zaidi ya watu milioni 120.

Asilimia 99 ya raia wa Japani huchoma miili ya wapendwa wao kulingana na desturi za Wabudha au Shinto. Lakini waislamu hawawezi kufanya hivyo. Kuchoma maiti ni marufuku katika Uislamu, na pia ni lazima wazike wafu wao ndani ya masaa 24.

Baadhi ya familia hulazimika kusafirisha maiti zao mamia ya kilomita ili kutekeleza desturi na ibada ya Kiislamu ipasavyo. "Ninapofikiria kwamba huenda nikachoma mwili wa mpendwa wangu, sipati usingizi," anasema Tahir Abbas Khan, ambaye alikuja Japani kwa mara ya kwanza mwaka wa 2001 kwa ajili ya tasnifu yake ya udaktari.

Abbas Khan, mwalimu wa chuo kikuu aliyezaliwa Pakistani, kwa sasa ni raia wa Japan na mwanaharakati wa jamii ya Kiislamu. Hapa alianzisha Jumuiya ya Waislam ya Beppu.

Vita vya muda mrefu

Kwa mujibu wa Dk Khan, hana wasiwasi kuhusu nini kitatokea kwa mwili wake baada ya kifo chake, lakini anasikitika kuona mateso ya wengine.

"Ibada ya mwisho ndio jambo la mwisho kwa binadamu. Ikiwa siwezi kumzika jamaa au rafiki yangu ipasavyo, siwezi kuishi maisha ya kawaida."

Msikiti wa kwanza ulijengwa mwaka wa 2009 katika Mkoa wa Oita, kusini mwa Kisiwa cha Kyushu, lakini makaburi ya hadi Waislamu 2,000 bado yanapangwa.

Mohammad Iqbal Khan alikuja Japani kutoka Pakistani na mke wake mwaka wa 2004. Alianza biashara ya kuuza magari karibu na Tokyo na baadaye akahamisha kituo chake hadi wilaya ya jirani ya Fukuoka.

Mtoto wake alipozaliwa akiwa amekufa mwaka 2009, hakukuwa na makaburi ya Waislamu katika eneo alilokuwa akiishi.

"Tuliuweka mwili kwenye kisanduku kidogo, tukauweka kwenye gari na kuelekea Yamanashi, ambayo ni zaidi ya kilomita 1000," anasema Iqbal.

Makaburi ya Yamanashi katika sehemu ya kati ya Japani hutumiwa na Waislamu na Wakristo. Wakristo ndio madhehebu mengine makubwa ya kidini nchini Japani, ambayo ni zaidi ya 1% ya watu wote.

"Nilitaka kuwa na mke wangu wakati wa shida kama hiyo, lakini haikuwezekana," anasema Iqbal. "Ilikuwa vigumu."

Shirika la Dk. Khan lilinunua ardhi karibu na makaburi ya Wakristo huko Beppu. Majirani walimwambia kwamba "hakuna pingamizi", lakini jumuiya ya karibu, umbali wa kilomita 3, ilipinga.

“Walisema miili iliyozikwa inachafua maji ya chini ya ardhi pamoja na maji ya ziwa yanayotumika kwa umwagiliaji,” alisema Dk Khan.

Hakuna kilichobadilika katika miaka saba. Kama matokeo, timu ililazimika kutafuta njia tofauti.

Kulingana na Dk. Khan, baadhi ya wahamiaji Waislamu walirudisha miili ya watu wa familia zao katika nchi yao. Wale wanaougua saratani wanapendelea kutumia siku zao za mwisho katika nchi yao ya kuzaliwa, anaongeza.

Hata hivyo, kupeleka mwili nyumbani kunahitaji nyaraka nyingi na pia huchelewesha mazishi.

Lakini hali haikuwa hivi kwa Ryoko Sato, Mwislamu wa Kijapani anayeishi katika kisiwa cha Kyushu.

"Usipofuata sheria za Wajapani, wanasema, rudi nchini kwako. Wengine wanasema, peleka mwili katika nchi jirani ambapo mazishi yanaruhusiwa.

Mume wangu alitumia zaidi ya nusu ya maisha yake huko Japani. Alipata uraia wa Japani muda mrefu uliopita na anatimiza wajibu wake wa kodi kama vile Mjapani wa huko.

Familia yake inaishi Japan, unafikiri mwili wake unapaswa kuzikwa wapi baada ya kufariki?"

Kulingana na Sato, upinzani wa kupata mahali pa kuzika unatokana na "ushirikina wa kitamaduni".

"Baadhi ya watu wanafikiri kuwa kuzika ni jambo la kutisha au lisilo la asili, lakini vizazi vichache vilivyopita, mazishi yalikuwa ya kawaida sana nchini Japan," Sato alisema.

Alishiriki katika uchomaji maiti nyingi, lakini baada ya kifo chake aliamua kujizika mwenyewe.

"Ikiwa hamu ya kuzika inaitwa ubinafsi, basi kuwa na ubinafsi na mwili wako mwenyewe."

Lakini kulingana na Shinji Kojima, profesa wa sosholojia katika Chuo Kikuu cha Ritsumeikan Asia-Pacific, ambako Dk. Khan anafanya kazi, sababu ni ngumu zaidi ya mtu anavyofikiria. Alitafiti suala hili na akashauri Jumuiya ya Waislamu ya Beppu.

"Jambo la kuamua sio kama wewe ni Mwislamu au la. Ni jinsi siasa za jamii za mitaa zinavyofanya kazi na kuwa na mtandao sahihi wa binadamu au miunganisho ambayo huamua matokeo," Dk Kojima aliambia BBC.

Suluhisho linalowezekana

Kwa mujibu wa Dk. Khan, kuna maeneo ya makaburi 13 ya Waislamu nchini Japani, mojawapo likiwa limejengwa hivi karibuni huko Hiroshima, takriban saa tatu kutoka hapo.

Iqbal aliongozana na waombolezaji. "Hiroshima ina mambo yote yanayotufaa. Kuna vyoo, jamii ya eneo hilo hutupatia chakula cha halali," alisema.

Dk. Khan alitoa wito kwa wabunge, wizara zenye shauku ya hili na mamlaka za mitaa kutatua tatizo hilo.

Sasa serikali ya mtaa imetenga ardhi kwa ajili ya maeneo ya makaburi 79 kwa jamii ya Waislamu wa Beppu.

"Hili si suala la kidini tu, ni haki ya msingi ya binadamu," anasema. "Hatuombi chochote bure. Tuna furaha kulipia, lakini ni muhimu kupata kibali cha kuweza kufanya maandalizi."

Kulingana na yeye, vikundi vingine vidogo kama Wayahudi na wahamiaji Wakristo waliowasili hivi karibuni kutoka Brazili pia wanateseka.

"Suluhisho bora ni kuwa na eneo moja la makaburi kwa ajili ya imani nyingi katika kila mkoa nchini Japani."

Hata hivyo, serikali kuu haiwezi kuingilia suala hili, kwa sababu imeliwacha mikononi kwa mamlaka za mitaa.

Lakini Dk. Khan hakati kukata tamaa. "Hatutachoma maiti. Hili halitafanyika. Tutafanya kila tuwezalo kuwazika wafu."