Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Joto kali linavyoongeza hatari ya kujifungua mtoto mfu - utafiti
- Author, Tulip Mazumdar
- Nafasi, BBC
Kufanya kazi kwenye joto kali kunaweza kuongeza hatari ya kuzaliwa mtoto mfu na kuharibika kwa mimba kwa wanawake wajawazito, kulingana na utafiti mpya kutoka India.
Utafiti huo uligundua kuwa hatari kwa mama mtarajiwa ni kubwa zaidi kuliko ilivyofikiriwa hapo awali.
Wanawake mia nane wajawazito katika jimbo la kusini mwa India la Tamil Nadu walishiriki katika utafiti huo, ambao ulianzishwa mwaka 2017 na taasisi ya Sri Ramachandra Institute of Higher Education and Research (SRIHER).
Kakriban nusu ya wale walioshiriki walikuwa ni wafanyakazi ambao wanakabiliwa na viwango vya juu vya joto, kama katika kilimo, ufyatuaji wa matofali na kutengeneza chumvi.
Mbinu za Kuepuka
''Wanawake wajawazito nchini India wako mstari wa mbele katika kukabiliwa na mabadiliko ya tabia nchi," anasema Prof Hirst.
Wastani wa halijoto la dunia inakadiriwa kuongezeka kwa karibu digrii tatu mwishoni mwa karne hii, ikilinganishwa na nyakati za kabla ya viwanda.
Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) linaonya juu ya tishio kwetu sote huku wanawake wajawazito wakikabiliwa na madhara makubwa zaidi.
Tafiti za awali zimeonyesha kuhusu ongezeko la asilimia 15 la hatari ya mtoto kuzaliwa kabla ya wakati na kuzaa mtoto aliyekufa wakati wa joto kali, tafiti hizo zilifanywa katika nchi zenye mapato ya juu kama vile Marekani na Australia.
''Matokeo ya hivi karibuni kutoka India ni ya kutisha na yanatia wasiwasi,'' anasema Prof Hirst, ''na yana maana pana zaidi.''
Kwa sasa hakuna ushauri rasmi wa kimataifa kwa wanawake wajawazito wanaofanya kazi katika maeneo yenye joto.
Mwongozo ambao upo kwa ajili ya kufanya kazi katika hali ya hewa ya joto, unatokana na tafiti zilizohusisha mwanajeshi wa Marekani katika miaka ya 1960 na 70, akiwa na uzito wa 70-75kg na 20% ya mafuta ya mwili.
Kiwango cha juu cha joto salama kwa watu wanaofanya kazi nzito ni 27.5C, kulingana na tasisi ya Usalama na Afya Kazini ya Marekani.
Prof Hirst anatumai utafiti huu, na utafiti zaidi, utabadilisha hilo. Wakati huo huo, anasema wanawake wajawazito wanaofanya kazi kwenye joto wanaweza kujilinda kwa:
Kuepuka muda mrefu kukaa juani.
Kupumzika kwa kukaa kivulini.
Kuepuka kuchomwa na jua kwa muda mrefu.
Kunywa maji mengi.
Nadharia kuhusu chanzo
"Wanawake hawa mara nyingi hawana chaguo ila kufanya kazi juani - wanahitaji pesa," anasema Rekha Shanmugam, muuguzi wa zamani na mtafiti wa utafiti wa SRIHER.
Sababu ya kwa nini joto huathiri wanawake wajawazito na watoto wao wanaokua katika mazingira ya joto hazieleweki vizuri.
Utafiti wa awali nchini Gambia uligundua halijoto ya juu inaweza kuongeza mapigo ya moyo ya kichanga na kupunguza mtiririko wa damu kupitia kitovu.
Nadharia hiyo inasema mama anapopata joto sana, damu inaweza kwenda mbali na kijusi ili kumsaidia kumpoza mama.
Anasema utafiti mwingine uligundua sababu ni kuwa wanawake wengi wawapo makazini hawaendi kujisaidia na hivyo kuepuka kunywa maji na hilo hupelekea matatizo.
"Wanaogopa wadudu na nyoka vichakani, au wanaume kuwachungulia," anasema Shanmugam. ‘Hivyo hukaa na mkojo siku nzima na hatimaye kwenda chooni watakapofika nyumbani."
Kutafuta suluhu
Matokeo ya utafiti huo wa Tamil Nadu yanachukuliwa kwa uzito mkubwa, anasema Dkt. TS Selbavinayagam, mkurugenzi wa afya ya umma katika jimbo hilo.
"Tayari tunatoa fidia ya kifedha kwa wanawake wajawazito, lakini labda tunahitaji kuangalia chaguzi za kutoa ajira mbadala pia," anasema.
Serikali ya jimbo huwapa wanawake maskini zaidi ya pauni 170 wanapofikisha wiki 12 za ujauzito, ili kujaribu kupunguza baadhi ya shughuli zao za kutafuta fedha.
Hata hivyo, nguvu kubwa ya kuwalinda wafanyakazi hawa wanaolipwa mishahara midogo ni ya wakubwa wa sehemu za kazi.
Kwenye viunga vya Chennai, Thillai Bhasker - mmiliki wa tanuru ya matofali - ameweka paa kubwa kuzuia jua, ili kuwapa wafanyikazi wake kivuli kinachohitajika.
"Wamiliki wa biashara wanapaswa kuwa na akili ya kutosha kujua jinsi ya kuwafanya wafanyakazi wabaki kazini," anasema. "Ukiwatunza, watakutunza."
Pia anasema ana mpango wa kujenga vyoo vya wanawake pekee.
Mashirika mengine pia yanatoa vipindi vya elimu kuhusu hatua ambazo wanawake wanaweza kuchukua ili kujilinda vyema wakati wa joto.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah