Talaka inayotishia kutikisa ufalme wa Wazulu

    • Author, Farouk Chothia
    • Nafasi, BBC News
  • Muda wa kusoma: Dakika 8

Mahusiano ya kimapenzi ya Mfalme wa jamii ya Wazulu kutoka Afrika Kusini yamezua mjadala nchini humo – huku gumzo linalohusiana na maisha yake ya kibinafsi likisambaa kwa kasi kama moto wa nyikani katika jamii hiyo ambayo inakumatia utamaduni wake. Mfalme wa Zulu anasemakana kuvunja kanuni za kitamaduni kwa kutaka kutoa talaka, jambo ambalo haliendani na itikadi za jamii hiyo.

Mume kuwa na wake wengi ni mojawapo ya masuala yanayokubalika katika jamii ya Wazulu, lakini Mfalme Misuzulu kaZwelithini amefanya uamuzi ambao sio wa kawaida kwa kuwasilisha kesi mahakamani ya kutaka kumtalaki mke wake wa kwanza, Malkia Ntokozo kaMayisela.

"Kila mmoja ameshangazwa. Watu hawakutarajia kwamba yangefikia kiwango cha kutaka kuotoa talaka,' alisema Profesa Gugu Mazibuko ambaye ni mtaalamu wa utamaduni katika chuo kikuu cha Johannesburg huko Afrika Kusini.

'Katika utamaduni wa jamii ya Wazulu, hakuna talaka. Haupaswi kumfukuza mke wako,' alisema.

Mfalme wa Jamii ya Wazulu anayefahamika kama 'Simba wa taifa,' ndiye mwenye kuhifadhi tamaduni za jamii hii ambazo ni za jadi. Tamaduni hizi zimedumisha ndoa na hususan ndoa ya wake wengi kama jambo kubwa kabisa la mafanikio ya ufalme.

Na japo majukumu yake nchini Afrika Kusini ni ya kitamaduni na hayana uzito katika sheria za nchi hiyo, kiongozi huyu wa jamii anasalia kuwa na ushawishi mkubwa katika jamii huku ofisi yake ikipokea ufadhili wa mamilioni ya dola za Kimarekani kutoka kwa serikali kuu.

Mfalme huyo ambaye alikulia katika taifa jirani la Eswatini , alipata masomo yake nchini Marekani na kukabidhiwa wadhifa wa uongozi mnamo 2021. Aidha amekuwa akikabiliwa na utata tangu awali.

Kukabidhiwa kwake mamlaka kulipingwa mahakamani na kaka yake mkubwa – ambaye ni wa mama mwingine – aliyetaka kupokezwa ufalme huo.

Ndoa yake ya pili, imegonga vichwa vya habari, na jaribio lake kuoa mke wa tatu limegongwa mwamba huku kukiwa na ripoti kwamba ana uhusiano kwa kando na mwanamfamle wa kike.

Hata hivyo, kashfa inayozunguka maisha ya kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 50 imekuwa ikijadiliwa chini kwa chini – hadi pale alipotangaza azma ya kumtalaki mke wake na kuwasilisha ombi rasmi mahakamani mwezi Desemba.

Profesa Madibuko amekiri kwamba kumbukumbu za historia ya Wa Zulu zinaonyesha kwamba kuna mfalme ambaye katiak karne ya 20 alimtalaki mmoja wa wake zake , ' ila hilo lilifanyika kimya kimya na kuwa siri kubwa katika familia hiyo ya kifalme,' ikizingatiwa kwamba talaka katika ufamle wa zulu sio jambo la kawaida.

'Ikiwa uhusiano utavunjika, basi mke huyu ataendelea kuishi katika boma la mfalme. Atapewa eneo lake kando, na hatakuwa na uhusiano an mfalme , ila yeye na watoto wake watatunzwa.'

Ilikuwa muda kabla ya kupokezwa ufalme – punde tu baada ya kifo cha ghafla cha baba na mama yake miaka minne iliyopita – kwamba mwanamfalme (wakati huo) Misuzulu alipomuoa Ntokoto Mayisela.

Wawili hao walikuwa tayari kwenye uhusiano wa kimapnenzi na walikuwa tayari ni wazazi wa Watoto wawili , ila kwa mujibu wa mtaalamu mwingine wa utamaduni wa jamii ya Zulu, Prof Muza Xulu kutoka chuo kikuu cha Zululand, uamuzi wa kufunga ndoa ulionekana kuharakishwa.

'Ilionekana kwamba mwanafalme hangeweza kuwa mfalme ikiwa hakuw ana mke,' alioambia BBC.

Malkia kaMayisela alitokea familia ya kawaida – kama wake wengine wa wafalme wa Kizulu – kutoka mji mdogo wa uchimbaji madini katika jimbo la KwaZulu – Natal.

'Malkia alimvutia Mfalme katika mgahawa mmoja kwenye mji wa pwani wa Durban alipokuwa akifanya kazi kama muimbaji,'alisema Prof Xulu.

Hadhi yake katika familia iliwekwa wazi wakati wa kutawazwa kwa mfalme mnamo Desemba 2022 alipoketi kando yake.

Ila nafasi yake sasa inatishika , anapotaja Mume wake kwamba wawili hao hawajaishi pamoja kama mume na mke kwa mwaka mmoja uliopita na kwamba ndoa yao imevunjika.

Kasri ya mfalme ilifuatilizia matamshi yake kwa kutuma mualiko wa ndoa ya Mfamle kwa mke mwingine, Nomzamo Mayeni mwishoni mwa mwezi Januari . Mahari ya bibi harusi inayofahamika kama LOBOLA kwa lugha ya kizulu imeshalipwa – huku ng'mbe wanaothaminiwa sana katika jamii hiyo wakitolewa kama mahari.

Malkia kaMayisela hajapokea haya yote vyema, akitaja kwamba huenda akawasilisha malalamishi ya kutaka ndoa hiyo kutofanyika , hali iliyosababisha ndoa hiyo kuahirishwa.

Ameiambia mahakama kwamba , mfalme ambaye anatambulika miongoni mwa jamii hiyo kama "ingonyama", kumaanisha simba, angekuwa anavunja sheria za ndoa kwa kufunga ndoa ya pili japo mke wa kwanza yupo. Anasema pia kwamba hatua hiyo inafanyika chini ya ndoa iliyofanyika katika ofisi ya mwanasheria mkuu ambayo haikubaliwi kuwa na wake wengi na kwamba kabla ya kuendeela mbele anapaswa kubadilisha ndoa yake ya kwanza kuwa ya kitamaduni kama inavyofanyika chini ya tamaduni za jamii ya wazulu.

Jaji alitupilia mbali ombi hilo kwa kusema kwamba ,malkia huyo alikuwa nabadili maoni yake baada ya kukubali kwamba mume wake angekuwa na wake zaidi ya mmoja awali.

Alisema kwamba mfalme alikuwa tayari ameshaoa mke wa pili – Nozizwe kaMulela ambaye ni mkurugenzi mkuu wa benki ya Eswatini mnamo 2022.

Prof Mazibuko ameseka kwamba ndoa yenye wake wengi haikuwa jambo ambalo lilifanyika sana katika jamii ya WaZulu, kwani wafalme wawili wa kwanza hawakuwahi kuoa.

Ila ndoa yenye wake wengi ilikumbatiwa na wafalme waliofuatia – Mfalme Misuzulu ndio wat isa katika jamii ya WaZulu – na hali hiyo imekubalika katika jamii hiyo.

'Hivyo ndivyo tunavyojenga familia, hususan familia ya kifalme,' alisema Prof Mazibuko.

Malkia kaMulela anatokea familia yenye umaarufu mkubwa nchini Eswatini, huku ndoa yao ikisemekana ilipangwa kwa ajili ya kuboresha uhusiano mwema kati ya familia mbili za kifalme.

Na japo haipo wazi ikiwa wawili hao bado wana uhusiano, kwa kuwa mfanyakazi huyo wa benki ya Eswatini hajaonekana hadharani katika hafla za kitamaduni za jamii ya Zulu kwa muda sasa – wengi wakisema kwamba itifaki kadhaa za kitamaduni katika ndoa yao hazijakamilishwa.

Mfalme wa sasa amekumbwa na matatizo kadhaa ya kindoa , jambo ambalo wengi wanasema limetokana na kanuni za kitamaduni kutofuatiliwa ipasavyo.

Katika ndoa ya mke wa kwanza, mfalme aliamua kufunga ndoa ya kisasa bila ya kufanya ndoa ya kitamaduni.

'Ili ndoa itambulike vuema chini ya tamaduni za Kizulu, ni lazima jamii ikusanyike katika hafla iliyojaa muziki na densi, ' alisema Prof Xulu.

'Wewe kama bibi harusi, ni sharti uwatumbuize waliofika kwa wimbo huku mabinti wanaokusindikiza wacheze nawe, kisha unapaswa kubeba mkuki ambao utampa Mfalme – na baada ya hilo, hakuna kurejea nyuma.'

Hili limemuwacha Malkia kaMayiela bila ya ulinzi wa utamaduni wa jamii – huku akipokea pendekezo la kupewa dola 1,100 za kimarekani kwa mwaka mmoja, japo anakisiwa kutaka zaidi kabla ya kurejea maisha ya kawaiada , ' alisema Prof Xulu.

Kumhusu mke wa pili, Profesa amesema kwamba mahari yaani LOBOLA ilitolewa Januari 2022 ila mfalme alihisi kwamba waliokwenda kulipa mahari hiyo hawakuwa na idhini ya kufanya hivyo – akiongezea kwamba ndoa hiyo haijatangazwa rasmi kama hafla ya umma.

Hatima ya mke wa tatu, Nomzamo Myeni haijulikani kwani mfalme hakufunga ndoa naye mwezi Januari kama ilivyopangwa na japo mahakama ilitoa idhini kwa ndoa hiyo kuendelea.

Prof Xulu amesema kwamba katika utamaduni wa jamii ya Zulu ' ndoa iliyoahirishwa ' wakati mwingi haifanyiki kabisa.

Na japo Myeni bado anaonekana hadharani ya Mfalme, akiandamana naye kwenya hafla ya kitaifa wiki jana ambako alitambuliwa kama Malkia, hali hii inaashiria kwamba ndoa yao huenda ikafanyika pindi tu talaka ya mfalme na mke wa kwanza itakapokamilika.

Na kama mtu wa kawaida, hana uahswishi mkubwa – hali ambayo baadhi ya wafanyakazi wa kasri wameeleezea vyombo vya Habari nchini humo kwamba kuna Malkia matarajiwa – Sihle Mdluli ambaye anatokea familia ya kifalme kutoka kwa jamii ndogo nchini Afrika Kusini.

Mfanyakazi aliyezungumza na BBC amesema kwmaba huenda akapewa jina la 'mama wa Jamii' – hadhi ambayo inamfanya kuwa mke mkuu wa mfamle huku Watoto wake wakiwa warithi wa mfalme.

Prof Xulu amesema kwamba hatashtuka ikiwa ndoa haitafanyika , kwani mahusiano yote ya mfalme yanakumbana na matatizo.

'sina uhakika ikiwa yupo tayari kuongoza kama mfalme, na ikiwa ana washauri wazuri , ' alisema Profesa.

Alitaja kwamba mfalme amekuwa akifanya maamuzi yenye utata katika maisha yake ya hadharani , akiwafuta kazi maafisa wake wakuu.

Mbali na haya, alijitangaza kama mwenyekiti wa bodi ya wakfu ya adrhin yenye utajiri mkubwa, ambapo pia yeye ndio mweka amana mkubwa.

Wakfu huo ulibuniwa katika hali tatanishi muda mfupi kabla ya Afrika kusini kupata uhuru wa Kidemokrasia mnamo 1994, hali iliyopia wakfu hiyo udhibiti wa hekta milioni 2.8 za ardhi huko Kwa Zulu Natal.

Mfalme Misuzulu amewasimamisha kwa muda wanachama wote wa bodi hiyo na kumuzia mmoja kwa madai kwamba hakuwa anashirikiana vyema naye.

Alfanya uamuzi huu kinyume na ushauri wa serikali kuu , iliyotaja kwamba kama mwenyekiti alihitajika kuieleza bunge la taifa kuhusu operesheni za wakfu huo- jambo ambalo haliambatani na wadhifa wake kama mfalme anayetambulika kwenye katiba ya taifa hilo.

Mzozo huo bado hautatatuliwa, hali inayoipa serikali kuu changamoto inapojaribu kuzuia makabiliana moja kwa moja na mfalme huyo.

Prof Xulu anasema kwamba hatapata mshtuko ikiwa wakati mmoja mrengo mmoja wenye nguvu ndani ya familia ya mfalme utawasilisha hatua jipya la kutaka kumuondoa madarakani, kwa kuiambia mahakama kwamba hana uwezo wa kuongoza jamii kama mfalme.

Ndugu yake wa kambo – Mwanamfalme Sinmakade Zulu ambaye nim toto mkubwa kabisa wa babake mfalme aliyefariki – amekuwa akiimezea mate kiti cha ufalme, ila wanaomuunga mkono wamekuwa wakishindwa katika mikakati na wendani wake Mfalme Misuzulu kwenye mijadala kuhusu ni nani mrithi wa Mfalme.

Rais Ramaphosa alimpa cheti cha utambulisho mfalme Misuzulu , hali iliyofungua milango ya mfalme huyo kupokea ufadhili kutoka serikali kuu.

Ila wafuasi wa Mwanamfalme Simakade hawakufa moyo – kuelekea mahakamani kuitaka kutawazwa kwake kama 'kinyume na sheria ' , kesi walioyoishinda.

Mahakama ilisema kwamba Rais Ramaphosa hakufuata sheria , inayomhitaji kufanya uchunguzi wa pingamizi ziliotolewa kumhusu Misuzulu.

Hali imesalia kama ilivyoamuru mahakama, huku kesi iliyowasilishwa katika mahakama ya rufaa ikisubiriwa kuamuliwa.

Hali hizi tatanishi zinatishia kupunguza nguvu zake mfalme ikiwa atakabiliwa na jaribio lingine la kumuondoa mamlakani.

Na japo Prof mazibuko amesema kwamab kumekuwa na mashindano makali kwa wanaotaka kuwa wafalme katika jamii ya Zulu – siku hizi mashindano hayo yanapiganiwa mahakamani tofauti na katika uwanja wa vita kama awali.

''Yeye sio mfalme wa kwanza kupitia mengi,' alisema. 'Ninatumaini kwamba ataponea na kila kitu kitulie.''

Imetafsiriwa na Leillah Mohammed