Mvulana aliyezaliwa na miguu minne iliyokuwa ikining'inia kutoka kwenye tumbo lake

Onyo:Baadhi ya picha na maelezo yaliyojumuishwa katika ripoti hii yanaweza kuwafadhaisha wasomaji.
Nilipokutana na Mohit Kumar kwa mara ya kwanza, alikuwa ameshika sehemu ya mbele ya shati lake kwa mikono miwili. Mohit amekuwa akifanya hivi kwa miaka 17 iliyopita.
Lakini sasa hana haja ya kufanya hivyo tena.
Hadi siku chache zilizopita, Mohit alikuwa na miguu minne kwenye mwili wake.
Alifanyiwa upasuaji mwezi uliopita kuondoa miguu miwili ya ziada.
Upasuaji huu nadra ulifanywa na madaktari katika Taasisi ya All India ya Sayansi ya Tiba (AIIMS) huko Delhi.
Mohit bado haamini kwamba miguu miwili ya ziada iliyoning'inia kutoka kwenye matumbo lake, ambayo alikuwa akiyabeba wakati anatembea, imeondolewa.
Mohit alisema kwa furaha, "Nilikuwa na miguu minne na nilifikiri haitawahi kuondolewa. Lakini sasa madaktari wameiondoa. Niliogopa sana nilipokuja hospitalini, lakini sasa ninahisi nafuu kweli. Uzito umepungua kutoka kwenye tumbo langu."
Katika lugha ya tiba ya sayansi, kesi kama hizo huitwa 'parastic twins'.
Mohit alikuwa na miguu miwili ya ziada iliyounganishwa kwenye mshipa wa kifua chake. Sehemu hii ya ziada ya mwili wake ilikuwa na uzito wa kilo 15.

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Timu ya madaktari wakiongozwa na Dk. Asuri Krishna, Profesa wa Ziada, Idara ya Upasuaji, Hospitali ya AIIMS, walitenganisha miguu ya Mohit baada ya upasuaji wa saa mbili mnamo Februari 8.
Akizungumzia kuhusu 'parasitic twins', Dk. Asuri Krishna aliambia BBC kuwa 'yai na mbegu za kiume zinapokutana katika mwili wa mama, 'zygote' hutengenezwa.'
Kawaida yai hili linakua polepole kuwa mtoto. Wakati mwingine hutokea kwamba hugawanyika katika sehemu mbili mwanzoni kabisa. Hii inasababisha watoto mapacha.'
Hata hivyo, wakati mwingine hali hutokea ambapo hawajatenganishwa kabisa na kubaki kushikamana na kila mmoja."
Katika hali hii, mtoto mmoja hukua kikamilifu, lakini mwingine husalia akiwa bado hajakamilika.
Kulingana na yeye, katika kesi ya Mohit, mtoto mmoja alikuwa ameumbwa kikamilifu, lakini mwingine alibakia kushikamana naye akiwa bado hajakamilika.
Kulingana na wao, sehemu isiyo kamili iliyounganishwa na mtoto aliyekamilika sio tu inapata damu bali pia lishe.
Jambo la kuzingatia hapa ni kwamba sehemu hii ambayo haijakamilika, iliyounganishwa na aliyekamilika, pia huhisi maumivu, kuguswa, na mabadiliko ya mazingira.
Dk. Krishna aliiambia BBC kwamba ni kesi 40 hadi 50 pekee za watoto mapacha wa aina hiyo ambazo zimeripotiwa kote ulimwenguni, na hata katika visa hivi, watoto hao hufanyiwa upasuaji.

Timu ya madaktari waliomfanyia upasuaji huo walisema kwamba ukuaji wa Mohit mwenyewe ulikuwa unaathiriwa na miguu yake yote miwili kuunganishwa kwenye tumbo lake.
Kulingana na madaktari, miguu hii ya ziada inaweza kuharibu sehemu zingine za mwili, kwa hivyo upasuaji ulionekana kuwa muhimu.
Uchunguzi wa CT scan wa Mohit ulifichua kuwa kuna 'pacha ambaye hajakamilika' aliyekuwa ameunganishwa naye na alikuwa ameshikamana naye na alikuwa akipokea damu kutoka kwenye mshipa mkuu wa damu kifuani mwake.
Kwa mujibu wa Dk. Krishna, "Mara tu sehemu ya ziada ilipoondolewa wakati wa upasuaji, mwili wa Mohit ulipoteza mara moja asilimia 30 hadi 40 ya kiasi cha damu yake, ambayo ilisababisha shinikizo la damu la mgonjwa kushuka kwa kiasi kikubwa."
Kulingana na yeye, "Tulikuwa tayari kwa hali hii na mara moja tuliimarisha shinikizo la damu." Kulingana naye, 'Wakati huu, tulipaswa kuhakikisha kwamba hakuna kiungo au tishu za Mohit zimeharibiwa.'
Baada ya hayo, madaktari waliondoa uvimbe ndani ya tumbo lake.
Kikundi cha madaktari waliofanya upasuaji huo kilijumuisha mtaalamu wa radiolojia, daktari wa ganzi, na daktari wa upasuaji wa kubadilisha umbo.
Mohit aliruhusiwa kwenda nyumbani baada ya siku nne.
Mohit alikuwa na umri wa miezi minne tu wakati mama yake alipoaga dunia, na baada ya hapo, baba yake, Mukesh Kumar Kashyap, amekuwa akimtunza tangu utotoni.
Kuwa na miguu minne kulimaanisha kwamba Mohit hakukabiliwa na matatizo ya kimwili tu bali pia changamoto katika ngazi ya kijamii.
Baba Mukesh Kumar anasema, "Tulipompeleka shuleni, Mohit aliniambia kuwa Baba, watoto wananisumbua na kila mmoja ananitania kwa kusema 'miguu minne, miguu minne."'
Kisha, alipofika darasa la nane, Mohit alilazimika kukatisha masomo yake. Baada ya matibabu yake, Mohit sasa anafikiria kusahau yaliyopita na kuanza upya maisha yake.
"Ninahisi kama mzigo umeondolewa," anasema. "Sasa ninaonekana kama watoto wengine."
Imefasiriwa na Asha Juma








