Tetesi 5 kubwa za soka jioni hii: Kevin De Bruyne athibitisha kuondoka Man City

Kevin De Bruyne

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 3

Kevin De Bruyne amethibitisha kwamba ataondoka Manchester City mwishoni mwa msimu huu baada ya miaka 10 katika Uwanja wa Etihad. Mbelgiji huyo ndiye mchezaji aliyeshinda mataji mengi zaidi katika historia ya klabu hiyo, akiwa ameshinda medali 19 tangu alipojiunga kutoka Wolfsburg mwaka 2015.

Mkataba wa nahodha huyo wa City unamalizika mwishoni mwa Juni. Katika chapisho la mitandao ya kijamii lililoanza na maneno "Manchester City", De Bruyne aliandika: "Hii itakuwa miezi yangu ya mwisho kama mchezaji wa Manchester City.

Mwezi Juni mwaka jana, De Bruyne, ambaye anapokea takriban pauni 400,000 kwa wiki, alidokeza kuwa angeweza kufikiria kuhamia Saudi Arabia. "Katika umri wangu, unapaswa kuwa wazi kwa kila kitu," alisema. "Unazungumzia kiasi cha fedha kisicho cha kawaida ambacho kinaweza kuwa cha mwisho katika maisha yangu ya soka. Wakati mwingine unapaswa kufikiria hilo. Nikicheza huko kwa miaka miwili, nitaweza kupata pesa nyingi sana. Kabla ya hapo, ilibidi nicheze soka kwa miaka 15 kupata kiasi hicho." (the Guardian)

Liverpool na Chelsea zinamtaka Marc Guehi wa Crystal Palace

Marc Guehi

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Marc Guehi

Liverpool na Chelsea wanaripotiwa kuwa miongoni mwa vilabu vinavyoongoza katika mbio za kumsajili beki wa Crystal Palace, Marc Guehi, majira haya ya joto.

Kwa mujibu wa TBR Football, klabu hizo mbili zinataka kuimarisha safu zao za ulinzi, huku beki huyo wa kimataifa wa England akiwa moja ya malengo makuu ya usajili.

Kuna tetesi kwamba Guehi yuko tayari kuondoka Crystal Palace iwapo atapokea ofa nzuri kutoka kwa timu kubwa.

Carragher: Liverpool inahitaji wachezaji sita wapya ili kushindana tena msimu ujao

liver

Chanzo cha picha, Getty Images

Jamie Carragher amekiri kwamba Liverpool huenda wakahitaji kusajili wachezaji sita ili kuendelea kubadilika na kuwa bora zaidi, licha ya kutawala Ligi Kuu ya England. Arne Slot hakuwa na ushawishi mkubwa katika dirisha lake la kwanza la usajili, lakini sasa anatarajiwa kusimamia ujio wa wachezaji kadhaa ifikapo Julai.

Liverpool wameendelea kung'ara na kikosi kilichojengwa na Jurgen Klopp, huku wachezaji wake wengi wakielekea kushinda taji lao la pili la ligi kuu, wakiongeza kwenye lile waliloshinda mwaka 2020. Hata hivyo, bado kuna mapungufu kwenye kikosi chenye wachezaji kadhaa wenye umri mkubwa.

Carragher amesisitiza haja ya kuongeza wachezaji wawili kwenye safu ya ulinzi: mmoja kushindana na Andy Robertson, ambaye ameshikilia nafasi yake kwa karibu muongo mmoja, na beki mpya wa kati ili kupunguza mzigo kwa Virgil van Dijk na Ibrahima Konaté.

Mchambuzi huyo wa Sky Sports pia anataka Liverpool waongeze viungo wawili wapya, mmoja kusaidia Ryan Gravenberch na Alexis Mac Allister, na mwingine kwa nafasi ya kiungo mshambuliaji . Carragher pia amependekeza kusajili washambuliaji wawili wapya ili kuimarisha safu ya mbele na kumsaidia Mohamed Salah.

Man United Wamtaka 'Peter Crouch Mpya' kwa Pauni Milioni 25

.

Chanzo cha picha, getty/Goal

Maelezo ya picha, Crouch (kushoto) na kulia ni Lucca

Manchester United wanaripotiwa kumweka kwenye orodha yao mshambuliaji anayefananishwa na 'Peter Crouch mpya', huku Mashetani Wekundu hao wakifikiria kumsajili mshambuliaji huyo wa Italia, Lorenzo Lucca, mwenye thamani ya pauni milioni 25.

Kwa mujibu wa The Sun, mshambuliaji wa Udinese mwenye urefu wa futi 6 na inchi 7, anayefananishwa na mchezaji wa zamani wa Liverpool na England Peter Crouch, ameibuka kuwa chaguo madhubuti kwa klabu ya Old Trafford, ambayo ipo katika mchakato wa mageuzi makubwa chini ya kocha Ruben Amorim.

Lucca, mwenye umri wa miaka 24, amevutia kwa kiwango chake bora katika ligi nya Serie A, akiwa amefunga mabao 18 katika misimu miwili iliyopita.

Eriksen kutemwa Man United majira ya kiangazi

a

Chanzo cha picha, Getty Images

Christian Eriksen anaonekana kuwa njiani kuondoka Manchester United mwishoni mwa msimu huu, kwa mujibu wa Football Insider. Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 33 amekuwa gumzo katika tetesi za usajili, huku ripoti zikidai kwamba kocha Rúben Amorim ametoa idhini ya kuondoka kwake.

Kwa kuwa mkataba wa Eriksen unamalizika majira ya kiangazi, Manchester United wanaripotiwa kuwa wameamua kutompa mkataba mpya wa kuendelea kusalia klabuni hapo.