Je, Kombe la Dunia linaweza kususiwa na mashabiki wa Ulaya?

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Rais wa FIFA Gianni Infantino ana uhusiano wa karibu na Donald Trump
Muda wa kusoma: Dakika 5

Rais wa zamani wa FIFA Joseph Blatter ameelezea kuunga mkono pendekezo la mashabiki kususia mechi za Kombe la Dunia mwaka huu, akielezea wasiwasi kuhusu mwenendo wa Rais wa Marekani Donald Trump na utawala wake.

Hafla hiyo itafanyika nchini Marekani, Canada na Mexico, kati ya Juni 11 na Julai 19.

Mnamo Jumatatu (Januari 26), Blatter, ambaye aliongoza FIFA kati ya 1998 na 2015 na kujiuzulu huku kukiwa na uchunguzi wa ufisadi, aliidhinisha kauli zilizotolewa na wakili wa Uswizi anayepambana na ufisadi Mark Pieth katika mahojiano na gazeti la Der Bund.

"Kuna ushauri mmoja tu kwa mashabiki: Kaeni mbali na Marekani! Mutaiona vizuri kwenye televisheni. Na, baada ya kufika, mashabiki wanapaswa kutarajia kwamba ikiwa hawatapendeza mamlaka, watawekwa moja kwa moja kwenye ndege inayofuata kurudi. Ikiwa wana bahati, "alisema Pieth.

Akishiriki mahojiano na X, Blatter aliandika: "Nadhani Mark Pieth yuko sahihi kuhoji Kombe hili la Dunia."

Pieth, ambaye aliongoza Kamati Huru ya Utawala ambayo ilisimamia mabadiliko ya FIFA muongo mmoja uliopita, alitaja kifo cha muandamanaji Renee Nicole Good, aliyepigwa risasi na wakala wa Uhamiaji na Utekelezaji wa Forodha (ICE) huko Minneapolis, kama moja ya sababu kwa nini mashabiki wasisafiri kwenda Marekani.

Usaidizi wa Blatter ulikuja baada ya kifo cha raia wa pili wa Marekani, Alex Pretti, mikononi mwa mawakala wa ICE.

"Tunachokiona ndani - kutengwa kwa wapinzani wa kisiasa, dhuluma na huduma za uhamiaji, na kadhalika. - si rahisi kuwahimiza mashabiki kwenda huko," Pieth aliiambia Tages-Anzeiger.

Shinikizo la kisiasa Ulaya

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Majadiliano kuhusu kususia Kombe la Dunia yaliongezeka baada ya Trump kusema nia yake ya kuchukua udhibiti wa Greenland, eneo linalosimamiwa na Denmark, akitoa sababu za usalama wa kitaifa.

Afisa kutoka Shirikisho la Soka la Ujerumani (DFB) alisema kuwa wakati umefika wa kufikiria kugomea Kombe la Dunia la 2026 ili kujibu hatua za Rais wa Marekani Donald Trump.

"Kwa kweli ninashangaa ni lini wakati utafika wa kufikiria na kuzungumza kwa dhati kuhusu hili [kususia]. Kwangu mimi, wakati huo tayari umefika," Oke Göttlich, makamu wa rais wa DFB, kwa Hamburger Morgenpost.

Katika kutetea nafasi yake, alitoa mfano wa Marekani kususia Michezo ya Olimpiki ya 1980 huko Moscow kufuatia uvamizi wa Umoja wa Kisovieti nchini Afghanistan.

"Katika tathmini yangu, tishio linalowezekana ni kubwa sasa kuliko ilivyokuwa zamani. Tunahitaji kuwa na mjadala huu."

Ujerumani ilitumbukia katika mzozo na FIFA katika Kombe la Dunia la 2022 nchini Qatar, wakati shirikisho la soka duniani lilitishia kuwaadhibu wachezaji wenye kadi za njano kwa kuvaa kitambaa cha OneLove wakati wa mechi.

.

Chanzo cha picha, Mike Egerton/PA Wire

Chama cha European Democratic Party (EDP) kimeonya kuwa kinaweza kuyaomba mashirikisho ya kitaifa kufikiria kujiondoa kwenye mashindano hayo ikiwa hakuna hakikisho la usalama kwa wageni wa Uropa.

Wakati huo huo, katika Bunge la Uingereza, wabunge 26 kutoka vyama vinne tofauti wanatoa wito kwa vyombo vinavyosimamia michezo kufikiria kuiondoa Marekani katika mashindano makubwa ya kimataifa.

Wanasema kuwa matukio haya "hayapaswi kutumiwa kuhalalisha ukiukaji wa sheria za kimataifa na mataifa yenye nguvu."

Waliotia saini wanasema wana wasiwasi kuhusu "kuongezeka kwa hatua za Marekani dhidi ya Venezuela," ikiwa ni pamoja na "kukamatwa kwa Rais Nicolás Maduro," ambayo itajumuisha "kuingilia moja kwa moja katika masuala ya ndani ya nchi huru."

Hoja hiyo pia inataja vitisho dhidi ya Denmark, Colombia, na Cuba, ambavyo "vinadhoofisha utaratibu wa kimataifa unaozingatia sheria."

Ingawa Ikulu ya Marekani bado haijajibu BBC kuhusiana na hoja hiyo kutoka kwa wabunge wa Uingereza, serikali ya Marekani ilikuwa tayari imesema kwamba kukamatwa kwa Maduro ni operesheni ya kutekeleza sheria dhidi ya kiongozi anayechukuliwa kuwa haramu na anayehusika na ulanguzi wa dawa za kulevya na ugaidi.

Sera ya kigeni ya Trump na Kombe la Dunia

Mnamo Desemba, Rais wa FIFA Gianni Infantino alimtunuku Trump "tuzo ya amani" ya kwanza ya shirika hilo wakati wa hafla ya droo ya Kombe la Dunia la 2026 huko Washington.

Infantino alisema rais wa Marekani "amechukua jukumu muhimu" katika kufanikisha usitishaji vita kati ya Israel na Palestina. Uamuzi huo ulikosolewa na Wafuasi wa Soka Ulaya na mashirika ya haki za binadamu.

Katika wiki zilizofuata, Marekani ilifanya vitendo vya kijeshi nchini Venezuela na Nigeria na kuashiria uwezekano wa operesheni mpya huko Greenland, Mexico - mwenyeji mwenza wa Kombe la Dunia - na katika nchi nyingine mbili zilizoshiriki: Colombia na Iran.

Katika taarifa za umma, Trump aliishinikiza Cuba "kufunga makubaliano" juu ya mauzo ya mafuta ya Venezuela "bila kuchelewa" na kusema kwamba hatua za kijeshi dhidi ya Colombia "zinanukia."

Kama ilivyo katika kesi ya Venezuela, alimshutumu Bogotá kwa kutofanya vya kutosha kukabiliana na ulanguzi wa dawa za kulevya. Rais wa Colombia Gustavo Petro aliiambia BBC kwamba anaamini sasa kuna "tishio halisi" la Marekani kuingilia kijeshi taifa lake.

Mexico nayo iliingia kwenye pambano hilo. Trump alisema kuwa dawa za kulevya zilikuwa "zikifurika" Marekani kutoka nchi jirani na akatangaza kwamba "kitu kitabidi kifanyike," huku kukiwa na ripoti kwamba timu yake ilikuwa imeanza kupanga kutumwa kwa wanajeshi.

Rais wa Mexico Claudia Sheinbaum alikataa pendekezo lolote la hatua za kijeshi katika eneo la kitaifa.

Zaidi ya hayo, Trump alikariri kwamba Marekani inahitaji kuchukua udhibiti wa Greenland kwa sababu za usalama wa kitaifa, bila kutumia matumizi ya nguvu, na kutangaza ushuru mpya dhidi ya washirika wanane wa Ulaya wanaopinga pendekezo hilo.

Eneo la Arctic, lenye madini mengi, linasimamiwa na Denmark-nchi mwanachama wa NATO-na linaweza kushiriki Kombe la Dunia ikiwa litafuzu.

Serikali ya Marekani pia inakabiliwa na maswali yanayoongezeka kuhusu uhalali wa mashambulizi ya anga dhidi ya meli zinazoshukiwa kuwa za ulanguzi wa dawa za kulevya katika Bahari ya Caribea na Pasifiki ya Mashariki.

.

Chanzo cha picha, Sam Corum/PA Wire

Maelezo ya picha, Rais wa Marekani Donald Trump alipokea tuzo hiyo kutoka kwa Infantino.

Je, FIFA inaweza kuchukua hatua?

FIFA imekataa kutoa maoni yake kuhusu hoja hiyo kutoka kwa wabunge wa Uingereza, na hakuna dalili kwamba inaweza kufikiria tena kutoa tuzo yake ya amani ya kila mwaka.

Hata hivyo, ni wachache wanaoamini kuwa shirika hilo litachukua hatua zozote dhidi ya nchi ambayo itakuwa mwenyeji wa mechi nyingi za Kombe la Dunia, hasa kwa kuzingatia uhusiano wa karibu ambao rais wa FIFA Gianni Infantino amekuza na Trump.

Uhusiano huu umesababisha shutuma kwamba FIFA imekuwa ya kisiasa, ingawa shirika hilo linasisitiza kuwa, kama mratibu wa mashindano, ina jukumu la kisheria kutoegemea upande wowote.

Hii si mara ya kwanza kwa FIFA kukabiliwa na shinikizo kutokana na hatua za kisiasa za nchi mwenyeji.

Mnamo mwaka wa 2018, mashindano hayo yalifanyika nchini Urusi, licha ya kunyakuliwa kwa Crimea miaka minne mapema. Urusi pia ilishutumiwa kwa mashambulizi ya mtandao, kuingilia uchaguzi wa Magharibi, na sumu ya wakala wa neva wa Novichok huko Salisbury.

Ulinganisho pia unafanywa na uamuzi uliofuata wa FIFA wa kupiga marufuku Urusi baada ya uvamizi wake mkubwa wa Ukraine mnamo 2022, vikwazo ambavyo bado vinatumika. "Tunataka uthabiti," Brian Leishman, mmoja wa wabunge waliotia saini hoja hiyo, aliambia Daily Mirror.

"Ni uvamizi wa taifa huru na kutekwa nyara kwa rais nchini Venezuela. Ninamkosoa sana Maduro, nataka kuweka wazi hilo, lakini tulichoona ni ukiukwaji wa sheria za kimataifa. Unapoona jinsi Urusi ilivyochukuliwa, ambayo ni sahihi kabisa, nataka tu kuwe na msimamo."

Baadhi ya wanachama wa FIFA wanaeleza kwa faragha kwamba Shirikisho la Soka la Urusi bado ni mwanachama na kwamba marufuku ya kucheza mechi za kimataifa ilitokana zaidi na timu nyingine za kitaifa kukataa kucheza dhidi yao na kwa sababu za usalama kuliko msimamo rasmi wa maadili wa shirika hilo.