Kambi ya Urusi,mashambulizi ya ndege zisizokuwa na rubani na kutoroka; Jinsi Bashar al Assad alivyotoroka Syria hadi Moscow

Muda wa kusoma: Dakika 5

Katika taarifa yake ya kwanza tangu kuondoka Syria, Rais aliyeondolewa madarakani Bashar al-Assad alisema hakuwa na nia ya kuondoka nchini humo, lakini alilazimika kufanya hivyo baada ya jeshi lake kusalimu amri.

Taarifa hiyo ya Bashar al-Assad ilichapishwa katika akaunti ya Telegram inayosimamiwa na ikulu ya Syria, lakini ni vigumu kusema ni nani anayedhibiti akaunti hiyo au kama Bashar al-Assad mwenyewe aliandika taarifa hiyo.

Ikumbukwe kuwa tarehe 9 Disemba makundi ya waasi yalidhibiti mji mkuu Damascus na utawala wa miaka 24 wa Bashar Assad ulifikia kikomo.

Taarifa hiyo iliyohusishwa na Bashar al-Assad ikisema kwamba wakati Damascus ilipoangukia mikononi mwa waasi, alikuwa katika kambi ya kijeshi ya Urusi huko Latakia "kusimamia operesheni ya kijeshi," lakini wakati huo jeshi la Syria lilikuwa limeacha msimamo wake na kurudi nyuma.

Kulingana na Bashar al-Assad, kituo cha anga cha Urusi Hmeimim pia kilikuwa kinakabiliwa na "mashambulizi mazito ya ndege zisizo na rubani" na wakati huo Urusi iliamua kumpeleka Moscow.

Taarifa hii inayohusishwa na Bashar al-Assad imetolewa kwa lugha za Kiingereza na Kiarabu na inaelezea matukio ya Desemba 8, ikiwa ni pamoja na jinsi alivyokwama akiwa katika kambi ya Urusi.

"Kulipokuwa hakuna njia ya kutoka nje ya uwanja wa ndege, Urusi iliomba uwanja uhamishwe mara moja Jumapili jioni, Desemba 8, na watu waliokuwa hapo wasafirishwe hadi Urusi."

"Haya yote yalitokea siku moja baada ya Damascus kuangukia (mikononi mwa waasi), wakati jeshi la Syria lilipojiondoa katika maeneo lilipokuwa, na matokeo yake, taasisi zote za serikali zilidhibitiwa"

Taarifa hiyo iliongeza kuwa "wakati wa matukio haya, hakuna wakati ambao sikufikiria kuacha urais au kutafuta hifadhi, na hakuna mtu au chama chochote kilichotoa fursa kama hiyo kwangu hadi wakati huo."

"Lakini serikali ilipoangukia mikononi mwa magaidi na uwezo wangu wa kuchukua jukumu la muhimu ulipotoweka, basi uwepo wangu huko haukuwa na maana."

Wakati waasi wakiongozwa na upinzani wa Syria walipochukua miji na majimbo ya Syria katika muda wa siku 12 tu, Bashar al-Assad hakuonekana popote.

Hata hivyo, kulikuwa na uvumi wakati huo kwamba Bashar al-Assad aliikimbia nchi. Hata waasi walipoingia Damascus, waziri mkuu wa Bashar al-Assad mwenyewe hakuweza kuwasiliana nao.

Mapema Jumapili asubuhi, wapiganaji walipoingia katika mji wa Damascus bila upinzani, kundi la wanamgambo la Hayat Tahrir al-Sham na washirika wake walitangaza kwamba "mtawala dhalimu Bashar al-Assad ameondoka (Syria)."

Shirika la habari la Reuters, likiwanukuu maafisa wawili wakuu wa jeshi la Syria ambao hawakutaka kutajwa majina, liliripoti kuwa Bashar al-Assad alipanda ndege ya Syrian Air na kuondoka uwanja wa ndege wa Damascus Jumapili asubuhi.

Unaweza pia kusoma:

Mnamo Desemba 9, vyombo vya habari vya Urusi vilitangaza kwamba Bashar al-Assad amepewa hifadhi nchini Urusi, lakini hii bado haijathibitishwa rasmi.

Kwa nini Bashar al-Assad aliichagua Urusi baada ya kuondolewa madarakani

Jibu rahisi kwa swali hili ni kwamba Urusi iliibuka kuwa mshirika mkuu wa Bashar al-Assad wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoanza mwaka 2011, na Kremlin pia ina kambi mbili za kijeshi katika nchi hii ya Mashariki ya Kati.

Mnamo mwaka wa 2015, Urusi ilianzisha mashambulizi ya anga ya kumuunga mkono Bashar al-Assad, ambayo hatimaye yaligeuza vita vinavyoendelea nchini humo yakimuunga mkono, na makundi yanayopigana dhidi yake kushindwa mfululizo.

Kundi hilo lenye makao yake makuu nchini Uingereza linakadiria kuwa hatua za Urusi zimeua zaidi ya watu 21,000 katika kipindi cha miaka tisa, wakiwemo raia 8,700.

Hata hivyo, kwa kuzingatia kinachoendelea Ukraine, Urusi haikuwa tayari au haikuweza kumuunga mkono Assad katika mapambano dhidi ya waasi yaliyoanza mwishoni mwa Novemba.

Uhusiano wa kina wa Bashar al-Assad na Urusi, na haswa Moscow, sio siri.

Mnamo mwaka 2019, uchunguzi wa Financial Times ulionyesha kuwa familia ya Bashar al-Assad ilinunua nyumba 18 za kifahari katika mji mkuu wa Urusi, Moscow, ili kuchukua mamilioni ya dola nje ya nchi wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria.

Wiki iliyopita, gazeti la Urusi liliripoti kwamba mtoto mkubwa wa Bashar al-Assad mwenye umri wa miaka 22, Hafez al-Assad, kwa sasa anasomea PhD huko Moscow.

Huku kukiwa na machafuko huko Damascus, runinga ya serikali ya Urusi iliripoti kuwa mamlaka ya Urusi kwa sasa inawasiliana na wapinzani wenye silaha nchini Syria ili kuhakikisha usalama wa kambi mbili za kijeshi za Urusi na wanadiplomasia nchini humo.

Ujumbe wa mataifa yenye nguvu 'waanzisha mawasiliano ya kidiplomasia' na Syria

Makundi ya waasi wa Syria kwa sasa yanaunda serikali ya mpito nchini humo.

Kundi la waasi lenye nguvu zaidi nchini humo, Hayat Tahrir al-Sham, liliibuka mwaka 2011 chini ya jina la Jabhat al-Nusra na kutangaza uhusiano wake na Al-Qaeda mwaka huo huo.

Hata hivyo, shirika hilo lilivunja uhusiano na Al-Qaeda mwaka wa 2016 na kuunda Jeshi la Waarabu wa Syria kwa ushirikiano na makundi mengine mbalimbali.

Aidha Umoja wa Mataifa, Marekani, Uingereza na nchi nyingine kadhaa bado wanalichukulia kuwa kundi la kigaidi.

Kiongozi wa kundi hilo, Ahmed al-Sharaa (Abu Muhammad al-Julani), ametangaza kuwa atavivumilia vikundi vingine vya kidini na kijamii nchini Syria.

Hata hivyo, kundi lake pia lina historia ya kijihadi, ndiyo maana wengine wana mashaka na ahadi zake.

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa Geir Pedersen alikutana na Ahmed al-Sharaa siku ya Jumapili na kusema kuwa mabadiliko "halisi" ni muhimu nchini Syria.

Qatar ilifunga ubalozi wake nchini Syria miaka 13 iliyopita, lakini serikali yake kwa sasa imetuma wajumbe mjini Damascus kuanza shughuli za kidiplomasia nchini humo.

Nchi za Magharibi hazijatangaza kufunguliwa kwa balozi zake nchini Syria, lakini Marekani na Uingereza zinasema kuwa wajumbe wao wamewasiliana na Syria katika siku mbili zilizopita.

Hata hivyo, serikali ya Uingereza imeweka wazi kuwa licha ya kuanza kwa 'mawasiliano ya kidiplomasia', lakini hadhi ya Jamhuri ya Kiarabu ya Syria kama kundi la kigaidi bado haijabadilika.

Siku ya Jumatatu, mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Kaya Klass alisema kwamba Urusi na Iran "hazipaswi kuwa na jukumu katika mustakabali wa Syria."

Unaweza pia kusoma

Imetafsiriwa na Martha Saranga na kuhaririwa na Dinah Gahamanyi