'Mume wangu aliyeingizwa jeshini sasa amekufa': Jinsi vita vya Myanmar vinavyowaua raia

Chanzo cha picha, Getty Images
Mara ya mwisho Chaw Su kumuona mume wake ilikuwa mwezi Machi, alipoandikishwa kwa nguvu kupigania jeshi katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Myanmar.
Miezi minne baadaye, aligundua kuwa alikuwa ameuawa kwenye mstari wa mbele wa vita.
"Siku zote tulikuwa maskini na tulitatizika," anasema. "Lakini maisha yalikuwa rahisi zaidi pamoja naye."
Mjane huyo mwenye umri wa miaka 25, ambaye alimtegemea mume wake kama mlezi, sasa anawatunza watoto watatu.
*Majina yamebadilishwa ili kulinda utambulisho wa vyanzo.
Mnamo Februari, utawala wa kijeshi wa Myanmar, unaojulikana kama junta, ulitangaza kuandikishwa kwa lazima, ikimaanisha wanaume wote wenye umri wa miaka 18 hadi 35 na wanawake wenye umri wa miaka 18 hadi 27 walilazimika kuhudumu hadi miaka miwili kama wanajeshi.

Chanzo cha picha, Reuters
Tangu kuanzishwa kwa mapinduzi ya 2021 ambayo yaliipindua serikali ya Aung San Suu Kyi iliyochaguliwa kidemokrasia, junta imekabiliwa na uasi kutoka pande nyingi - ikiwa ni pamoja na Jeshi la Ulinzi la Watu wa kujitolea (People’s Defence Forces -(PDFs), na makundi ya kikabila yenye silaha. Uasi huo tangu wakati huo umeongezeka na kuwa vita kamili vya wenyewe kwa wenyewe.
Mwaka jana uliashiria mabadiliko, wakati jeshi liliposhuhudia wimbi jipya la mashambulizi kutoka kwa waasi ambayo yameifanya serikali ya kijeshi kufikia hatua ya kuvunjika. Matokeo yake, hadi theluthi mbili ya nchi, ambayo imekuwa na miongo kadhaa ya utawala wa kijeshi na ukandamizaji, iliangukia chini ya udhibiti wa makundi ya upinzani.
Wanajeshi wanaozidi kukabiliwa na hali ngumu walijibu kwa kwa kulazimisha usajiri wa lazima wa raia jeshini , licha ya onyo kutoka kwa wataalam kwamba hilo linaweza kuzidisha mzozo wa wenyewe kwa wenyewe nchini huo . Mafunzo ya kwanza yalianza Aprili.
'Nilirukwa na akili kabisa'

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kama wengine wengi, Chaw Su aliahidiwa mshahara kutokana na huduma ya mumewe, lakini alidai alipokea kyati 70,000 pekee (kama dola 21 hivi ) kutoka kwa afisa wa kijiji wakati mumewe alipoandikishwa jeshini kwa mara ya kwanza.
Baada ya malipo ya awali, miezi ilipita bila usaidizi wowote wa kifedha.
Jeshi linasema walioandikishwa wana haki ya kulipwa mshahara na fidia wanapokufa wakiwa kazini, kama ilivyo kwa askari wa vyeo kamili. Lakini msemaji wa junta Meja Jenerali Zaw Min Tun aliiambia BBC "kunaweza kuwa na kuchelewa ikiwa hati muhimu hazijakamilika".
Kote Myanmar, askari walioandikishwa - mara nyingi huwa hawajafunzwa na hawajajiandaa - wanatumwa kwenye maeneo yenye migogoro wakiwa na usaidizi mdogo. Familia zao mara nyingi huachwa gizani kuhusu mahali walipo.
Soe Soe Aye, mjane mwenye umri wa miaka 60, ameachwa bila kupata taarifa kutoka kwa mwanawe, ambaye aliandikishwa jeshini miezi sita iliyopita. Anasema hakuwa na hamu ya kutumikia jeshi.
"[Mwanangu] alijiunga na jeshi ili kumlisha mama yake," anaongeza kwa machozi. "Najuta kumuacha."
Sasa, anapambana na afya mbaya na anamtegemea binti yake mdogo kutunza familia yao. Lakini anajaribu kuendelea kuwa na matumaini.
"Nataka tu kumuona mwanangu. Sina nguvu za kutosha kukabiliana na hili."
'Nilichukia jeshi hata zaidi'

Chanzo cha picha, Kan Htoo Lwin hafuati mtu yeyote Autodesk_new
Vijana wengi wa Burma wamechukua hatua kali za kupinga agizo la kujiunga na jeshi.
Kan Htoo Lwin, mwenye umri wa miaka 20 kutoka kituo cha kibiashara cha Myannmar, Yangon, aliandikishwa na kupata mafunzo ya kijeshi kwa miezi mitatu pamoja na wengine 30.
Anasema mafunzo hayo yalikuwa ya kuchosha na walitishiwa kwamba iwapo mtu yeyote atajaribu kutoroka, nyumba zao zitachomwa moto.
"Baada ya mafunzo, nilichukia zaidi jeshi," anasema.
Wakati wa safari ya kuelekea mstari wa mbele wa vita katika eneo la mashariki mwa nchi, Kan Htoo alipata fursa ya kutoroka akiwa na watu wengine wawili wakati msafara wao uliposimama nusu njia.
"Tulikimbia mara giza lilipoingia, huku wakiwa na shughuli nyingi za ukaguzi wa usalama. Hatukusimama hadi usiku ulipoingia," anakumbuka. "Wakati fulani tulichoka na tukasimama ili kupumzika. Tulichukua zamu ya kulala na kukesha."
Kulipopambazuka, vijana hao watatu walipanda gari kutoka kwa dereva wa lori na kufika hadi Aung Ban, kitongoji cha kusini mwa jimbo la Shan. Hapa, Kan Htoo alijiunga na PDF, mojawapo ya vikundi vingi vya upinzani ambavyo vimekuwa vikikua huku vijana wengi, waliokatishwa tamaa na jeshi la kijeshi, wakichukua silaha.
Wanaume wengine wawili kwa sasa wamejificha, Kan Htoo anasema. Kwa sababu za usalama, hataki kufichua wanachofanya sasa.
'Ni vigumu kuelezea mapambano yangu'

Chanzo cha picha, Getty Images
Wakati wanaume wamekuwa lengo kuu la juhudi za kujiandikisha, wanawake pia wameathirika.
Zue Zue, mwenye umri wa miaka 20 kutoka Yangon, aliacha ndoto yake ya kuwa mfasiri wa Kichina ili kujiunga na Kikosi Maalum cha Operesheni (SOF), kitengo ndani ya PDFs.
"Sasa lengo langu ni kukomesha enzi hii ya udikteta wa kijeshi na kuleta amani kwa kizazi chetu," anaiambia BBC.
Wakati Zue Zue alichagua kubaki, wengine wameikimbia nchi.
Mhandisi Min Min aliondoka kuelekea Thailand wakati usajili ulipoanza. Sasa anaishi huko kwa visa ya elimu, lakini anadai amekuwa akihangaika kupata kazi ya kisheria inayolingana aliyosomea huko Bangkok.
Wengi wanaokimbilia Thailand, kama Min Min, wanaishia kwenye kazi zenye ujira mdogo. Mamlaka za Thailand pia zimekuwa kali katika kukamata wahamiaji haramu, na wengi sasa wanakabiliwa na kufukuzwa ikiwa watakamatwa.
Min Min anahofia kwamba muda wa visa yake utakapoisha, atalazimika kuishi nchini kinyume cha sheria.
"Nina wasiwasi kuhusu gharama za maisha," anasema kijana huyo mwenye umri wa miaka 28. "Sina chaguo ila kutafuta kazi za mikono."
Pia anasema kipaumbele kinatolewa kwa raia wa Thailand, ambao haki zao zinalindwa, wakati wamiliki wa biashara wa Thailand mara nyingi huwanyonya wahamiaji wanaofanya kazi kinyume cha sheria.
"Nimeona pia kwamba wahandisi wa Kiburma wanaofanya kazi kinyume cha sheria na wanalipa tu takriban baht 12,000 za Thai ($355), sawa na mshahara wa wafanyakazi wa mikono wahamiaji," anasema.
Huko Myanmar, Chaw Su sasa anafanya kazi zisizo za kawaida kijijini, na anapata mshahatra wa chini sana kulisha watoto wake.
"Ni vigumu kueleza watu wengine mapambano ninayopitia," anasema.
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi na kuhaririwa na Seif Abdalla












