Wanajeshi wa Myanmar wanaokataa kupigana

Chanzo cha picha, KEVIN KIM/BBC
Jeshi la Myanmar linakabiliwa na uasi kutoka kwa vikosi vyake na linapata shida kuajiri. Katika mahojiano ya kipekee, wanajeshi wapya walioasi wanaambia BBC kwamba jeshi la serikali, ambalo lilichukua mamlaka katika mapinduzi miaka miwili iliyopita, linajitahidi kukandamiza uasi wa demokrasia wenye silaha.
"Hakuna anayetaka kujiunga na jeshi. Watu wanachukia ukatili wao na vitendo vyao visivyo vya haki," anasema Nay Aung. Mara ya kwanza alipojaribu kuondoka kwenye kituo chake aligongwa na sehemu ya nyuma ya bunduki na kuitwa "msaliti".
Alifanikiwa kutoroka mara ya pili na kuvuka mpaka hadi Thailand akiungwa mkono na makundi ya upinzani.
"Rafiki yangu mmoja yuko kwenye upinzani," anasema. "Nilimpigia simu akawaambia watu hapa Thailand kunihusu. Nilifika hapa kwa msaada wao."
Sasa anaishi katika nyumba ya ulinzi pamoja na wanajeshi wengine 100 waliotoroka hivi karibuni na familia zao. Hawa watu waliokataa kupigana na watu wao sasa wamejificha kwa hiyo hatutumii majina yao halisi. Wanahifadhiwa na kulindwa na vuguvugu la upinzani waliloamriwa kupigana.

Chanzo cha picha, KEVIN KIM/BBC
Tangu jeshi lichukue mamlaka katika mapinduzi Februari 2021, zaidi ya wanajeshi na polisi 13,000 wamejitoa, kulingana na Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Myanmar (NUG) iliyo uhamishoni. Wanatoa motisha ya pesa taslimu na usaidizi ili kujaribu kupata askari na maafisa wa polisi zaidi kujiunga nao.
Maung Sein mwenye umri wa miaka 19, ndiye mdogo zaidi katika nyumba ya kuhifadhia watu. Alijiunga na jeshi alipokuwa na umri wa miaka 15 tu.
"Nilipendezwa na jeshi," Maung Sein anasema, na alitaka kuifanya familia yake ijivunie. Lakini ukandamizaji mkali wa jeshi dhidi ya uasi wa nchi nzima unaodai demokrasia umebadilisha sana mtazamo wa watu kuhusu wanaume waliovalia sare.
"Tuliona watu mtandaoni wakituita 'mbwa wa kijeshi'," anasema - neno la wanyama ni moja ya matusi makubwa nchini Myanmar. "Hilo lilinifanya nijute na kunisikitisha."
Maung Sein anasema askari kama yeye hawakuweza kukiuka "maagizo kutoka juu" ya "kuua raia na kuchoma vijiji".
Lakini pia aliondoka kwa sababu anadhani jeshi liko katika nafasi dhaifu.
Magenge ya kijamii yenye silaha katika maeneo ya mpakani pamoja na mtandao wa makundi ya wanamgambo wa kiraia, yaitwayo Jeshi la Ulinzi la Wananchi (PDF), yanaonekana kuwa na nguvu kubwa zaidi kuliko ilivyotarajiwa na jeshi la Myanmar limepoteza udhibiti wa maeneo makubwa ya nchi.
Katika Kitengo cha Magway na Kitengo cha Sagaing, maeneo ambayo hapo awali yalisajili vijana wengi jeshini sasa yamebadilika, vijana badala yake wanajiunga na wanamgambo wa kiraia.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kabla ya kufanikiwa kutoroka, kitengo cha Maung Sein kiliamriwa "kushambulia na kuharibu" kambi ya mafunzo ya PDF.
Oparesheni haikuenda vizuri. Wanajeshi wenzake saba waliuawa kabla ya kuamriwa kurudi nyuma. "Wao [PDF] wana mkakati bora," anasema, "ambayo inawafanya kuwa na nguvu."
PDF inafurahia kuungwa mkono na umma na wanakijiji hutoa taarifa za kijasusi kuhusu mienendo ya wanajeshi na kuwahifadhi wapiganaji wachanga wa wanamgambo.

Chanzo cha picha, ANDRE MALERBA/BBC
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kapteni Zay Thu Aung alihudumu miaka 18 katika jeshi la anga. Aliasi mwaka mmoja baada ya mapinduzi Februari 2022.
"Wanashambuliwa kote nchini," anasema, akitafakari hali ya jeshi la Myanmar, "na hawana wanaume wa kutosha wa kupigana."
Hii ndiyo sababu, anasema, jeshi linazidi kutumia jeshi la anga.
Katika miezi ya hivi karibuni jeshi limefanya mashambulizi mabaya ya anga kote nchini. Tangu Januari kumekuwa na ripoti zaidi ya 200 za mashambulizi ya anga. Shambulio baya zaidi la anga lilifanywa dhidi ya kijiji cha Pa Zi Gyi katika mkoa wa Sagaing mwezi Aprili, ambapi zaidi ya watu 170 waliuawa, wakiwemo wanawake na watoto kadhaa.
"Bila ya jeshi la anga, kuna uwezekano mkubwa kwamba jeshi litashindwa," Capt Aung anatabiri.
Kama waasi wengine, kila mtu katika familia yake alijivunia yeye alipochaguliwa kama kadeti ya jeshi la anga. Katika nyakati hizo, anasema, ilikuwa heshima kuwa sehemu ya jeshi la Myanmar. Mapinduzi hayo, anasema, "yalituvunjia hadhi".
"Wengi wa watu nilioishi nao katika jeshi la anga hawakuwa watu wabaya. Lakini tangu mapinduzi hayo, wamekuwa wakifanya kama wanyama wazimu."
Ni yeye pekee katika kitengo chake ambaye amejitenga. Baadhi ya marafiki zake "wameendelea kupigana dhidi ya watu wangu", anasema.

Chanzo cha picha, Getty Images
Licha ya jukumu muhimu la jeshi la Myanmar katika masuala ya nchi hiyo, ukubwa wake kamili haujulikani. Waangalizi wengi wanakadiria wakati wa mapinduzi walikuwa karibu 300,000 lakini idadi hiyo imepungua sana.
Upinzani umetumia teknolojia mpya kama vile michezo ya video pamoja na njia za jadi za kukusanya pesa kupata pesa, nyingi ikiwa ni michango ya mtu binafsi kutoka raia wanaoishi nje ya nchi.
Wameweza kuongeza kiasi kikubwa kwa njia hii lakini hawana silaha za zinazofikia kiwango cha kijeshi au ndege za kivita.
Serikali ya Umoja wa Kitaifa imejitolea kulipa $500,000 (£405,000) kwa marubani wa serikali au mabaharia ambao watahama kwa kutumia ndege ya kijeshi au chombo cha wanamaji, lakini hadi sasa hakuna aliyefanya hivyo.














