Waliteswa hadi kufa: Mauaji ya watu wengi Myanmar yafichuliwa

Walioteswa na kuuawa walizikwa kwenye makaburi yenye kina kifupi
Maelezo ya picha, Walioteswa na kuuawa walizikwa kwenye makaburi yenye kina kifupi

Jeshi la Mynmar lilitekeleza msururu wa mauaji ya raia wengi mwezi wa Julai, ambayo yalisababisha vifo vya wanaume takriban 40, kulingana na Uchunguzi wa BBC.

Walioshuhudia pamoja na manusura wa mauaji hayo, wanasema wanajeshi, baadhi yao wakiwa vijana wadogo wenye umri wa miaka 17 waliwazingira wanavijiji kabla ya kuwatenga wanaume na kuwauwa.

Video na picha za matukio hayo zinaonekana kuonyesha wengi waliouliwa waliteswa kwanza na kuzikwa kwenye makaburi mafupi.

Mauaji hayo yalifanyika katika mwezi wa Julai, katika matukio manne tofauti katika mji wa Kani - ambao ni ngome ya upinzani katika wilaya ya Sagaing iliyopo katikati mwa Myanmar.

Jeshi limekabiliana na upinzani kutoka kwa raia tangu liliponyakuwa udhibiti wan chi katika mapinduzi ya mwezi wa Februari, na kuing'oa madarakani serika iliyochaguliwa kwa njia ya demokrasia iliyoongozwa na Aung San Suu Kyi.

m

Chanzo cha picha, Getty Images

BBC ilizungumza na mashahidi 11, katika mji wa Kani na kulinganisha Ushahidi wao na picha za video za simu ya mkononi, picha zilizokusanywa na mashahidi wa Myanmar, pamoja na taarifa za shirika lisilo la kiserikali lenye makao yake Uingereza ambalo linachunguza ukiukaji wa haki za binadamu nchini Myanmar.

Mauaji makubwa zaidi yalifanyika katika kijiji cha Yin, ambako wanaume wapatao 14 waliteswa na kupigwa hadi kufa na miili yao ilitupwa katika msitu.

Walioshuhudia tukio hilo katika kijiji cha Yin - ambao majina yao yamebanwa ili kulinda utambulisho wao, waliiambia BBC kuwa wanaume hao walifungwa kwa Kamba na kupigwa kabla ya kuuawa.

"Hatukuweza kustahimili kutazama, tuliinamisha vichwa vyetu chini, tukilia ," alisema mwanamke mmoja, ambaye kaka na shemeji yake waliuawa.

"Tuliwaomba wasifanye hivyo. Hawakujali. Waliwaomba wanawake , 'Je kuna wame zenu miongoni mwao? Kama ni wame zenu, muwaage mara ya mwisho'."

Mwanaume mmoja ambaye alifanikiwa kutoroka mauaji alisema kwamba wanajeshi waliwatesa wanaume hao kwa namna ya kutisha kabla ya kufa.

"Walifungwa, wakapigwa mawe na kuteswa kwa namna mbali mbali kwa siku nzima ," alisema manusura.

"Baadhi ya wanajeshi walionekana wenye umri mdogo, labda miaka 17 au 18, baaadhi walikuwa ni wazee sana. Kulikuwa pia na mwanamke aliyekuwa pamoja nao."

m

Katika kijiji jirani cha Zee Bin Dwin, mwishoni mwa mwezi wa Julai, miili 12 ' iliyokatwa viungo ilipatikana imezikwa kwenye makaburi yenye vina vifupi, akiwemo mtoto mdogo mvulana, na mwili wa mlemavu. Baadhi ilikuwa imekatwa viungo.

Mwili wa mwanaume mwenye miaka sitini na ushee hivi, ulipatikana ukiwa umefungwa Kamba kwenye mti.

Picha za maiti yake, zilizotathminiwa na BBC, zinaonyesha wazi alama za mateso.

Familia yake ilisema kwamba mtoto wake wa kiume na mjukuu walikuwa wametoroka wakati wanajeshi walipoingia kijijini, lakini yeye alikuwa amebaki, akiamini kuwa umri wake ungemlinda dhidi ya madhara.

Mauaji yalionekana kuwa ni adhabu ya jumla kwa ajili ya kulipiza kisasi cha mashambulio ya raia dhidi ya makundi ya wananajeshi katika eneo hilo, ambao wanadai kurejeshwa kwa demokrasia nchini.

Mapigano baina ya jeshi na makundi ya kiraia -People's Defence Force - jina la pamoja la makundi ya wanamgambo raia yameimarika katika eneo hilo kwa miezi kadhaa kabla ya mauaji ya pamoja, yakiwemo makabliano ya ghasia karibu mji wa Zee Bin Dwin.

Ni wazi kwa ushahidi wa video na picha na ushahidi uliokusanywa na BBC kwamba wanaume ndio waliokuwa hasa wanalengwa, kutokana na tathmini iliyofanywa kote Mynmar katika miezi ya hivi karibuni kote nchini ambapo wanavijiji wanaume walionekana wakikabiliwa na adhabu ya jumla kwa makabiliano baina ya kikosi cha ulinzi cha watu- People's Defence Forces anna jeshi la Myanmar.

Familia za wale waliouawa zilisisitiza kuwa wanaume hao hawakuhusika katika mashambulizi dhidi ya wanajeshi.

Mwanamke mmoja aliyempoteza kaka yake katika mauji katika kijiji Yin alisema aliwaomba sana wanajeshi , akiwaambia kuhusu kaka yake "hakuweza hata kuvumilia kushika nati".

Alisema mwanajeshi alijibu, "Usiseme lolote. Tumechoka. Tutakuua."

Waandishi wa habari wa kigeni wamezuiwa kuripoti taarifa kutoka ndani ya Myanmar tangu yafanyike mapinduzi, na vyombo vingi vya habari ambavyo sio vya taifa,vimefungwa, na hivyo kufanya utangazaji wa taarifa kutoka kwenye maeneo mbali mbali kuwa jambo lisilowezekana.

BBC ilipomuuliza naibu Waziri wa habari na msemaji wa jeshi la Myanmar, Jenerali Zaw Min Tun kuhusu madai hayo, hakukana kuwa jeshi lilifanya mauaji ya watu wengi .

"Inaweza kutokea," alisema. "Unapotuchukulia sisi kama maadui, tunayo haki ya kujilinda ."

Umoja wa mataifa kwa sasa unachunguza madai ya ukiukaji wa hali za binadamu uliotekelezwa na jeshi la Myanmar.