Mapinduzi Myanmar: Marekani yatishia kuiwekea nchi hiyo vikwazo kwa kuzuiliwa kwa Aung San Suu Kyi

Chanzo cha picha, Reuters
Rais wa Marekani Joe Biden ametishia kuirejeshea Myanmar vikwazo baada ya jeshi kupindua serikali.
Jeshi la Myanmar lilimkamata Aung San Suu Kyi na viongozi wengine wa kisiasa wakiwashutumu kwa udanganyifu katika uchaguzi wa hivi karibuni ambao Suu Kyi alipata ushindi mkubwa.
Katika taarifa, Bwana Biden amesema "nguvu isiwahi kutumika kubadilisha maamuzi ya watu au kufuta matokeo ya uchaguzi uliofanyika kwa njia ya halali".
Umoja wa Mataifa na Uingereza pia zimeshutumu mapinduzi hayo.
Marekani ilikuwa imeiondolea nchi hiyo vikwazo zaidi ya muongo mmoja uliopita wakati ambapo Myanmar ilionesha kufuata demokrasia.
Bwana Biden amesema hatua hiyo itapitiwa tena kwa haraka na kuongeza: "Marekani itaunga mkono demokrasia kila itakapokuwa hatarini."
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres aliitaja hatua iliyochukuliwa na jeshi "pigo kubwa kwa mabadiliko ya kidemokrasia", huku baraza la usalama likijitayarisha kufanya mkutano wa dharura.
Umoja wa Mataifa imetaka kuachiliwa kwa watu wasiopungua 45 ambao wanazuiliwa na jeshi.
Nchini Uingereza, Waziri Mkuu Boris Johnson ameshutumu mapinduzi hayo na kuzuiliwa kwa Aung San Suu Kyi ambako ni "kinyume na sheria".
Viongozi wa Umoja wa Ulaya wametoa shutuma zao sawa na hizo.
China, ambayo awali ilipinga muingilio wa mashirika ya kimataifa kwa nchi ya Myanmar, ilitoa wito kwa pande zote mbili "kutatua tofauti zao".
Baadhi ya mataifa jirani yenye nguvu kama vile Cambodia, Thailand na Ufilipino, yamesema kwamba hilo ni "suala la ndani".
Kipi kilichotokea Myanmar?
Wanajeshi wanashika doria mitaani na kuwekwa amri ya kutotoka nje usiku pamoja na kutangazwa kwa hali ya dharura kwa mwaka mmoja.
Bi. Suu Kyi amewasihi wafuasi wake "kuandamana dhidi ya mapinduzi hayo ya jeshi".
Katika barua iliyoandikwa wakati amezuiliwa, alisema hatua za kijeshi zitarejesha nyuma nchi hiyo chini ya utawala wa kidikteta.
Tayari jeshi limetangaza mabadiliko katika nafasi kadhaa za mawaziri.

Chanzo cha picha, Reuters
Mitaani kati ya mji mkuu wa Yangon, watu walisema kuwa wanahisi juhudi zao za kupigania demokrasia zimeishia patupu.
Mkazi mmoja, 25, ambaye hakutaka kutajwa jina lake, ameiambia BBC kuwa: "Kuamka na kugundua kuwa dunia yako imebadilishwa kabisa kwa usiku mmoja tu haikuwa hisia nzuri, hisia ambazo nilidhani zimeshapitwa na wakati, na wala sikuwahi kufikiria kwamba iko siku nitahisi hivi tena."
Myanmar ambayo pia inajulikana kama Burma, ilitawaliwa na jeshi hadi mwaka 2011, pale mabadiliko ya demokrasia yaliokuwa yakiongozwa na Aung San Suu Kyi yalipotamatisha utawala huo wa kijeshi.
Alikamatwa kwa karibu miaka 15 kati ya mwaka 1989 na 2010.
Kimataifa alichukuliwa kama nembo ya demokrasia na kupokea Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka 1991.
Lakini sifa yake kimataifa ikaingia doa baada ya kutokea kwa msako uliotekelezwa na serikali dhidi ya kundi la walio wachache la Warohingya.
Wakati huo aliokuwa wakimuunga mkono, walimshutumu kwa kukataa kulaani vitendo vilivyotekelezwa na jeshi au kutambua madhila yaliyotekelezwa.
Mapinduzi ya kijeshi yalitokea vipi?
Majira ya asubuhi, mapema sana Jumatatu, kituo cha televisheni kinachomilikiwa na jeshi kilisema kuwa mkuu wa jeshi Min Aung Hlaing amechukua udhibiti wa nchi hiyo.
Bi. Suu Kyi, Rais Win Myint na viongozi wengine wa chama cha National League for Democracy (NLD) walikamatwa kufuatia misako kadhaa iliyotekelezwa na jeshi.
Hadi kufikia sasa, bado haijafahamika viongozi hao wanazuiliwa wapi.

Chanzo cha picha, Reuters
Hakuna matukio makubwa ya ghasia ambayo yameripotiwa.
Wanajeshi wamefunga barabara za mji wa Nay Pyi Taw, na mji mkuu wa Yangon.
Vyombo vya habari vya ndani na kimataifa ikiwemo kile kinachomilikiwa na serikali vyote vilizimwa.
Huduma za mtandao na simu zilizimwa.
Benki zimesema pia nazo zimelazimishwa kusitisha huduma zao.

Chanzo cha picha, EPA
Baadaye, jeshi likatangaza kuwa mawaziri 24 na manaibu wao wameondolewa huku wengine 11 wakitajwa kama mbadala wa mawaziri hao akiwemo wa afya, fedha, usalama wa ndani na mambo ya nje.
Pia kumetangazwa amri ya kutotoka nje kuanzia saa mbili usiku saa za eneo hadi kumi na mbili asubuhi.
Tukio la mapinduzi ya kijeshi limetokea kufuatia wiki kadhaa za wasiwasi kati ya jeshi na serikali baada ya uchaguzi wa ubunge ambapo upande wa upinzani uliokuwa unaungwa mkono na jeshi ulishindwa kwenye uchaguzi huo.
Upinzani ulikuwa umedai kurudiwa kwa zoezi la uchaguzi kwa madai kwamba ulikumbwa na udanganyifu lakini madai hayo yakatupiliwa mbali na Tume ya Uchaguzi.














