Jeshi laidhibiti Myanmar baada ya kumshikilia Aung San Suu Kyi

Aung San Suu Kyi at a coronavirus vaccination clinic in January, Naypyitaw, Myanmar

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Kiongozi wa Myanmar Aung San Suu Kyi

Jeshi la Myanmar limethibitisha kulidhibiti taifa hilo baada ya kumuweka kizuizini kiongozi wa taifa hilo Aung San Suu Kyi pamoja na wanasiasa wengine mapema hii leo.

Baada ya kumkamata kiongozi huyo kwa saa kadhaa, televisheni ya taifa imetangaza kuwa taifa lipo kwenye hali ya dharura kwa muda wa mwaka mmoja.

Aung San Suu Kyi, kiongozi wa Myanmar, ambaye chama chake cha National League for Democracy (NLD) kipo madarakani amekamatwa, msemaji wa chama amesema.

Aung San Suu Kyi, ameomba wafuasi wake "wasikubali hilo" na kutoa wito kwa raia "kuandamana dhidi ya mapinduzi".

Katika barua iliyoandikwa wakati tukio la kuzuiliwa kwake linaendelea, amesema hatua za kijeshi zinarejesha nchi hiyo nyuma katika enzi za udikteta.

Hatua hiyo inawadia wakati wa mvutano mkali kati ya raia na wanajeshi wakihofia jeshi kutawala.

Soldiers on the road in Nay Pyi Taw, Myanmar, 1 February 2021

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Wanajeshi wamepelekwa kuziba barabara mjini humo

Soma zaidi:

Katika uchaguzi uliofanyika mnamo mwezi Novemba, chama cha NLD kilishinda kura nyingi lakini jeshi likadai kuwa kura zilikuwa zimeibiwa.

Myanmar ambayo inajulikana kama Burma, ilikuwa ikiongozwa na jeshi hadi mwaka 2011. Kwa miaka mingi, Bi Suu Kyi alikuwa katika kifungo cha nyumbani.

Wanajeshi walikuwa mitaani katika mitaa ya mji mkuu wa Naypyitaw pamoja na mji wa Yangon.Huduma za simu na mtandao zilizimwa katika miji mikubwa wakati televisheni ya taifa inasema kwamba kulikuwa na hitilafu za kiufundi.

Mwanahabri wa BBC, Kusini Mashariki mwa Asia, Jonathan Head, amesema kuwa chini ya katiba jeshi lina nguvu ya kutangaza hali ya dharura lakini kuzuia viongozi wa kisiasa kama Bi. Suu Kyi ni tukio la kichokozi na hatari ambalo linaweza kupingwa vikali, mwanahabari wa BBC amesema.

Msemaji wa NLD Myo Nyunt amezungumza na shirika la habari la Reuters kwa njia ya simu na kusema kuwa Bi. Suu Kyi, Rais Win Myint na viongozi wengine wamekamatwa mapema asubuhi.

"Nataka kuwaambia watu wetu wasichukue hatua kwa haraka na ninawaomba muchukue hatua kwa kuzingatia sheria," msemaji amesema, akiongeza kuwa pia yeye anatarajia kukamatwa.

Wanajeshi pia walitembelea baadhi ya nyumba za mawaziri katika maeneo mbalimbali na kuwakamata, kulingana na familia zao.

Min Aung Hlaing

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Mkuu wa jeshi Min Aung Hlaing amechukua uongozi wa taifa hilo

Nini kilitokea katika uchaguzi?

Chama cha NLD kilishinda kwa asilimia 83 ya kura zote zilizopigwa Novemba 08, wakati kura za maoni zikiwa zinataka utawala wa kiraia.

Huu ulikuwa uchaguzi wa pili tangu kuondolewa kwa utawala wa kijeshi mwaka 2011.

Lakini jeshi lilikataa matokeo na kupeleka malalamiko yao mahakamani dhidi ya rais na mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi.

Huku kukiwa na hofu ya kutokea kwa mapinduzi baada ya kutishia kufanya hivyo kwa madai ya wizi wa kura. Tume ya uchaguzi ilikataa madai yao.

Kiongozi wa Myanmar Aung San Suu Kyi akizungumza katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) huko The Hague

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Aung San Suu Kyi mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel

Aung San Suu Kyi ni nani?

Aung San Suu Kyi ni binti wa shujaa wa uhuru wa Myanmar, jenerali Aung San.

Aliuawa wakati Aung akiwa na umri wa miaka miwili kabla ya Myanmar haijapata uhuru wake kutoka kwa utawala wa ukoloni wa Uingereza mwaka 1948.

Bi Suu Kyi alikuwa kinara wa kutetea haki za binadamu - mwanaharakati ambaye alijitoa mhanga kukabiliana na utawala wa kimabavu ambao ulidumu kwa miongo kadhaa nchini Myanmar.

Mwaka 1991, alitunukiwa Tuzo ya Amani ya Nobel, wakati akiwa katika kifungo cha nyumbani na alisifiwa kwa kuwa mfano mzuri wa kutetea wanyonge.

Bi. Suu Kyi alitumikia kifungo cha nyumbani kwa karibu miaka 15 tangu mwaka 1989 hadi 2010.

Mnamo mwezi Novemba mwaka 2015 alikiongoza chama cha National League for Democracy (NLD) kwenye mashindano ya kwanza ya wazi ya uchaguzi tangu miaka 25 iliyopita.

Katiba ya Myanmar ilimkataza kuwa rais kwasababu ana watoto ambao asili yao sio nchini humo bali ni wageni.

Lakini tangu awe kamishina wa Myanmar, utawala wake umeonekana kuwapendelea watu wa Budha walio wengi .

Mwaka 2017 mamia ya maelfu ya watu wa jamii ya Rohingya walikimbilia taifa la jirani la Bangladesh baada ya jeshi kufanya msako mkali uliopelekea kuwa na mashambulizi mabaya katika vituo cya polisi katika jimbo la Rakhine.

Wafuasi wa zamani wa kimataifa wa Bi. Suu Kyi walimshutumu kiongozi huyo kwa kushindwa kuzuia matukio ya ubakaji, mauaji n ahata mauji ya kimbari ambayo yangeweza kutokea kwasababu alikataa uwepo wa utawala wa kimabavu wa kijeshi au kukubali kuwa kuna ghasia kubwa.

Watu wachache walimuona kuwa mwanasiasa mwenye busara anayejaribu kuongoza taifa lenye changamoto za ukabila na historia ambayo ina misukosuko mingi.

Lakini utetezi wake dhidi ya hatua ambazo zinachukuliwa na jeshi katika kesi iliyosikilizwa na mahakama ya kimataifa mwaka 2019 huko Hague alionekana kuwa na sehemu ndogo ya kubadilisha katika sifa ya wadhifa wake kimataifa.

Ana wafuasi wengi katika taifa lake haswa wa jamii ya Buddha ambao ni wengi na wasio na huruma kwa jamii ya Rohingya.