'Nilishtuka na mwili kufa ganzi nilipohukumiwa kunyongwa'

    • Author, Veronica Mapunda
    • Nafasi, BBC Swahili
    • Akiripoti kutoka, Dar es Salaam

Akiwa na umri wa miaka 18 tu, Rose Yona Malle alikutana na mtihani mkubwa katika maisha yake baada ya kukamatwa mwaka 2012 na miaka kadhaa baadaye kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa.

Tukio hilo lilibadili maisha yake kabisa na kuua ndoto zake, katika umri huo alikuwa bado mwanafunzi wa chuo aliyekuwa akifukuzia ndoto zake.

“Yote hayo yalitokea na yamenifanya nisiishi katika ndoto zangu, leo hii nafanya kitu tofauti na kile nilichokuwa natamani” anasema Rose

Alitoka gerezani mwaka 2017 baada ya kukata rufaa dhidi ya hukumu yake na kushinda ikiwa ni baada ya kukaa gerezani tangu 2012.

Je Kesi yake ilikuaje?

Ilikuwa ni siku ya kawaida ya kuhudhuria masomo yake chuoni kama ilivyo siku zingine, Rose Malle alimpigia dereva wa bodaboda ampeleke chuo alichokuwa akisoma huko Moshi mkoani Kilimanjaro Kaskazini mwa Tanzania majira ya asubuhi.

Dereva wa bodaboda alifika kumchukua Rose na kumfikisha hadi chuoni kwake salama kabisa na kumuacha aendelee na masomo yake.

Bila kujua hili wala lile, siku ya pili alifuatwa na polisi na kutaarifiwa kuwa anashtakiwa kwa kumjeruhi dereva wa bodaboda ambaye alimpeleka chuo siku iliyotangulia.

“Kumbe siku ile baada ya kuniacha chuo kuna watu walikodi bodaboda yake na kumfanyia uhalifu huo, inasemekana walimjeruhi na kumnyang’anya bodaboda” Anafafanua.

Kwa vile Rose ndiye aliyeonekana wa mwisho kumpigia simu, moja kwa moja alikuwa mshukiwa wa tukio.

“Nilikuja kukamatwa nyumbani, walikuja askari wengi wakiwa na silaha, nilikamatwa kama jambazi mkubwa sana na kuleta taharuki kwa familia, na ilinipa uwoga ambao si wa kawaida”

Alishtakiwa kwa kosa la kujeruhi baada ya kukaa kwa zaidi ya wiki mbili kituo cha polisi, majeruhi alifariki hivyo alibadilishiwa kesi kutoka kesi ya kujeruhi na kuwa kesi ya mauaji ambayo haina dhamana.

Baada ya upelelezi kukamilika Rose alifikishwa mahakamani kujibu mashtaka hayo alikutwa na hatia na Disemba 28, 2015 alihukumiwa kunyongwa hadi kufa.

“Nilishtuka sana kwa sababu sikutarajia, nilisikia maumivu ambayo siwezi kuyasahau, sikufanya halafu nahukumiwa kunyongwa, mwili mzima ulikufa ganzi’ anaeleza huku akisikitika.

Rose alikata tamaa na kuhisi maisha yake ndiyo yameishia hapo, na asingewaona tena wazazi wake, ndugu na ndoto zake zingekufa.

Hivyo alitolewa gereza la Karanga Moshi na kupelekwa gereza la Isanga lilipo Dodoma katikakati mwa Tanzania kwa ajili ya kutumikia adhabu yake.

Maisha ya gerezani

Kabla ya kuhukumiwa alikuwa tayari amekaa mahabusu kwa takribani miaka mitatu hivyo alikuwa kiongozi wa vikundi vya kidini gerezani.

Hiyo ilimjengea imani ya kuamini kuwa Mungu anaweza kubadili kila kitu.

“Mimi nilikuwa faraja kwa wafungwa wenzangu gerezani, hivyo siku nahukumiwa kila mmoja alikata tamaa na kusema kama Rose kahukumiwa nani atabaki” anasema Rose

Anasema maisha ya gerezani yalikuwa ni hekaheka kila siku lakini kuna vitu ambavyo hawezi kuvisahau ikiwa ni pamoja na kulala saa kumi jioni na ikifika saa tatu hakuna kuongea tena.

Unaweza pia kusoma

Rufaa

Disemba 2017 hatimaye Rose Malle alishinda rufaa.

Alifanikiwa kukata rufaa baada ya kukaa mwaka na takribani miezi saba gerezani baada ya hukumu akisubiri kupatiwa mwenendo mzima wa kesi.

Anasema alifanikiwa baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kutembelea gereza.

“Siku moja aliingia Waziri Mkuu kusikiliza kero za wafungwa, nilisoma risala na baadaye aliniita na kuniuliza maana nilikuwa mdogo kuliko wote, hapo nikamuelezea, hivyo alimwambia mwanasheria wa gereza afuatilie”, alielezea.

Baada ya wiki moja aliletewa mwenendo mzima wa kesi na kuandika sababu za rufaa na ndani ya mwezi mmoja kesi yake ilipangwa kusikilizwa.

Uhuru

Baada ya miaka takriban sita gerezani aliyoitumikia akiwa mahabusu hadi alipoanza kutumikia hukumu yake, hatimaye akapata uhuru tena.

“Niliona miaka sita niliyokaa gerezani imekuwa siku moja, yale maumivu, huzuni niliyopitia kwa miaka sita nilisahau kwa wakati mmoja”, anaelezea kwa matumaini

Baada ya kutoka gerezani alikuta maisha yamebadilika, hakumkuta baba yake mzazi, aliyefariki dunia pia mama yake alianza kuugua shinikizo la damu.

Akutana na mume wake gerezani

Rose ni mke na mama wa watoto wawili kwa sasa. Na simulizi yake na mume wake nayo ina mengi.

“Siku ambayo mimi natoka tu mlango wa gereza alikuja kunipokea mtu ambaye kwa sasa ni mume wangu” anaeleza akiwa anatabasamu.

Rose Malle na mume wake Mohamed Ulotu walikutana gerezani ambapo mume wake alikuwa kiongozi wa wafungwa wenzake yaani ‘Nyampara’

Anadai mume wake alihukumiwa kimakosa kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la ujambazi wa kutumia silaha na wakati Rose anatoka alikuwa amemaliza kifungo chake.

“Tulikuwa marafiki gerezani lakini siku naachiwa huru alikuja na kuniambia ananipenda na ninafaa kuwa mke wake” anasema.

Septemba, 2019 Rose na Mohammed walifunga ndoa na kuanza maisha mapya ya ndoa.

Kiongozi wa Wafungwa

Rose Malle, 29, kwa sasa ni mkurugenzi mkuu wa taasisi ya Tanzania Ex-Prisoners Foundation ambayo inasaidia bure wafungwa kukaa sawa kisaikolojia.

“Mfungwa anapotoka gerezani kisaikolojia huwa hayupo sawa, tuna madaktari wa afya ya akili huwaweka sawa ili akubali kupokea maisha mapya bila visasi” anasisitiza Rose.

Anasema yeye binafsi alivyotoka gerezani jamii ilimpokea tofauti. Alikutana na unyanyapaa na kuoneshewa vidole lakini hakukata tamaa.

Anaeleza kuwa hii husababisha hata baadhi ya wafungwa kurudia tena makosa yao na kurudishwa tena gerezani.

“Asilimia 60 ya wafungwa gerezani ni wafungwa wa kujirudia rudia, mtu anamaliza kifungo lakini baada ya muda anarudi tena gerezani”

Mpaka sasa Rose ana jumla ya wafungwa wa zamani 17 aliowapokea na kuwapa msaada wa kisaikolojia ikiwa ni pamoja na kuwapatanisha na familia zao.

“Changamoto kubwa inayotukwamisha ni gharama za uendeshaji kwani tunatoa huduma bure, tunatamani kusaidia wengi na kuwafikia watu wengi zaidi” .

Wito kwa serikali

Anatoa wito kwa mamlaka hususani kwa viongozi kutembelea mara kwa mara magerezani ili kusikiliza kero za wafungwa kwani inaweza kusaidia baadhi kama ilivyotokea kwake.

“Lakini pia napenda kuomba mamlaka zijaribu kupeleka kesi kwa haraka, kusikiliza rufaa kwa haraka na watu wapewe mienendo ya kesi zao hii inaweza kupunguza msongamano magerezani” anaongezea Rose.

Mbali na yote hayo Rose pia ni muigizaji wa filamu na tamthilia na pia ni mshindi wa tuzo ya muigizaji bora wa kike mkoa wa Kilimanjaro.

Imehaririwa na Florian Kaijage

Unaweza pia kusoma

Imehaririwa na Florian Kaijage