Kwa nini Pakistan imeunda kamandi mpya ya kijeshi?

Muda wa kusoma: Dakika 4

Waziri Mkuu wa Pakistani Shahbaz Sharif ametoa tangazo kubwa usiku wa Agosti 13, siku moja kabla ya Siku ya Uhuru wa Pakistani kusherehekea miaka 78, akisema kamandi mpya imeanzishwa katika jeshi la Pakistani, ikipewa jina la 'Kamandi ya Kikosi cha Roketi cha Jeshi la Pakistani'.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, kamandi hii kitakuwa na zana za kisasa na kueleza kuwa ni 'hatua muhimu' ambayo itaimarisha zaidi uwezo wa ulinzi wa Pakistan.

Si Waziri Mkuu Shahbaz Sharif wala Jeshi la Pakistani, aliyetoa taarifa zaidi kuhusu kamandi hii mpya, waangalizi na wachambuzi wanaona kuanzishwa kwake ni matokeo ya vita vya hivi karibuni kati ya Pakistan na India.

Wachambuzi wanaamini makombora ya masafa mafupi hadi ya kati yamethibitisha kuwa silaha madhubuti katika vita vya Ukraine na Urusi, vita vya Israel na Iran, na vita vya hivi karibuni kati ya India na Pakistan.

Ikumbukwe kuwa mvutano kati ya India na Pakistan uliibuka mwezi wa Mei wakati Delhi ilipoilaumu Pakistan kwa mauaji ya makumi ya watalii huko Pahalgam yaliyofanywa na wanamgambo wenye silaha na India ikaamua kushambulia kwa mabomu maeneo kadhaa ya Pakistan, ingawa Pakistan ilikanusha madai ya India.

Wakati wa mzozo huu, baada ya Pakistan kudai kuidungua ndege ya kivita ya Jeshi la Anga la India, India ilirusha makombora ya balestiki katika kambi mbalimbali za anga, ikiwa ni pamoja na Nur Khan Air Base huko Rawalpindi, Mei 10, Pakistan pia ilijibu mara moja kwa kulenga shabaha mbalimbali ndani ya India.

Pakistan ilidai kuharibu kambi za anga za India na mifumo ya ulinzi wa anga kwa kutumia makombora ya Fateh One na Fateh Two. Baada ya kushambuliana Marekani ilitangaza usitishaji wa mapigano kati ya nchi hizo mbili.

Kwa kuzingatia mzozo huu, wachambuzi wa mambo wanaamini makombora haya, ambayo yanayolenga shabaha za masafa ya kati, ni ya gharama nafuu, ni hatari, na yana uwezo wa kufyatuliwa haraka, na yanaweza kurushwa zaidi ya moja kwa wakati mmoja.

Pia unaweza kusoma

Ni kamandi ya aina gani?

Mchambuzi wa masuala ya ulinzi Muhammad Ali anasema jeshi la Pakistan lina matawi mawili ya kamandi ya kijeshi, moja ni kwa ajli ya vita vya kawaida na jingine ni Kamandi ya Kimkakati, ambayo inajumuisha silaha za maangamizi na makombora yenye uwezo wa kubeba vichwa vya nyuklia.

Muhammad Ali anasema, "Jukumu la Kamandi ya Kikosi cha Roketi itakuwa tofauti na kamandi ya kawaida na ile ya kimkakati, na itaweza kulenga shabaha za adui wakati wa vita kwa kutumia makombora ya masafa ya kati bila kutoa taswira ya vita vya nyuklia."

Kwa mujibu wa vyanzo vya usalama, "kuanzishwa kwa kamandi hii haimaanishi kwamba vikosi vipya vinaundwa, bali ni mfumo mpya wa makao makuu na amri, unaoanzishwa ili kutumia silaha za masafa marefu kwa utaratibu na ufanisi zaidi."

Kombora la Fateh, ambalo linafika kilomita 150 hadi 400, vyanzo vya usalama vinasema "kuanzishwa kwa kamandi mpya kunamaanisha katika siku zijazo makombora haya yataweza kutumika chini ya maamuzi ya kati, yaliyoratibiwa na ya haraka."

Afisa wa zamani wa jeshi ameiambia BBC "uamuzi huu umechukuliwa ili kuongeza ufanisi katika jeshi la Pakistani, hasa kudhibiti matumizi ya roketi na makombora ambayo hutumiwa katika vita vya kawaida.

Kabla ya kuundwa kwa Kamandi ya Kikosi cha Roketi cha Jeshi nchini Pakistan, nchi nyingi za Asia zimeunda kamandi za roketi. Katika eneo la Asia, India, China, na Urusi zina kamandi hizo, na kila kamandi ya kila nchi ina muundo tofauti.