Jinsi VVU vilivyoongezeka kwa zaidi ya 1000% katika taifa hili dogo la pasifiki

    • Author, Gavin Butler
  • Muda wa kusoma: Dakika 7

Miaka Kumi: huu ni umri wa mtoto mdogo aliye na Virusi Vya Ukimwi (VVU) ambaye Sesenieli Naitala aliwahi kumwona.

Alipoanzisha mtandao wa Survivor Advocacy Network huko Fiji mwaka 2013, yule mvulana bado hajazaliwa. Sasa yeye ni mmoja wa maelfu ya Wafiji ambao wameambukizwa virusi vinavyoenezwa kwa damu katika miaka ya hivi karibuni, wengi wao wakiwa na umri wa miaka 19 au chini, na wengi kupitia matumizi ya dawa za kujidunga kwa sindano.

"Wazee wengi wanaanza kutumia dawa," alisema Bi. Naitala, ambaye shirika lake hutoa msaada kwa wafanyikazi wa ngono na watumiaji wa dawa huko Suva, mji mkuu wa Fiji. "Yeye (yule mvulana) alikuwa miongoni mwa wale vijana walioshiriki sindano mitaani wakati wa Covid."

Katika miaka mitano iliyopita, Fiji taifa dogo katika Pasifiki Kusini lenye watu chini ya milioni moja limekuwa mahali ambapo mojawapo ya milipuko ya VVU yenye kuongezeka kwa kasi duniani imechukua kasi.

Mwaka 2014, nchi hiyo ilikuwa na watu wasiozidi 500 walio na VVU.

Kufikia 2024 idadi hiyo ilipanda hadi takribani 5,900 ongezeko la mara kumi na moja.

Mwaka huo huo, Fiji iliripoti visa vipya 1,583 ongezeko la mara kumi na tatu kulinganisha na wastani wake wa miaka mitano.

Takwimu kama hizo zilimfanya waziri wa afya na huduma za matibabu nchini humo kutangaza mlipuko wa maambukizi ya VVU mwezi Januari.

Wiki iliyopita, waziri msaidizi wa afya Penioni Ravunawa alionya Fiji inaweza kurekodi zaidi ya watu 3,000 walioambukizwa VVU ifikapo mwisho wa 2025.

"Hili ni janga la kitaifa," alisema. "Na haipunguzi."

BBC ilizungumza na baadhi ya wataalamu, mawakili na wafanyikazi walio mstari wa mbele kubaini ongezeko hilo la maambukizi ya virusi limetokana na nini.

Wengi walisema kwamba, kadiri uelewa wa jinsi VVU vinanavyozwa na unyanyapaa unavyopungua, watu wengi wamekuwa wakijitokeza na kupima.

Wakati huo huo, walibaini kuwa idadi kubwa ya watu wengi hawajajumuishwa kwenye takwimu rasmi, hii ikimaanisha kwamba kiwango cha halisi cha maambukizi kinaweza kuwa kikubwa zaidi kuliko hata idadi zilizovunja rekodi zinavyoashiria.

'Kuchangiana damu'

Msingi wa mlipuko wa VVU Fiji ni kuongezeka kwa matumizi ya dawa, ngono isiyokuwa salama, kugawana sindano na "bluetoothing".

"Bluetoothing," pia huitwa "hotspotting", ni tabia ambapo mtumiaji wa sindano apiga dawa, kuvuta damu baada ya sindano, kisha kuinyunyiza katika mtu mwingine yule mwingine anaweza kufanya hivyo kwa mtu wa tatu, na kadhalika.

Kalesi Volatabu, mkurugenzi wa NGO Drug Free Fiji, amewahi kuona tukio hilo mwenyewe.

Mwezi Mei uliyopita, alipokuwa akitembea mapema asubuhi katika Suva kuwapa elimu na msaada watumiaji wa dawa mitaani, alipokuwa kwa kona, aliona kundi la watu saba au nane wakiwa wamekusanyika.

"Niliona sindano ikiwa na damu ilikuwa mbele yangu," anakumbuka. "Mwanamke huyo mdogo, tayari alikuwa amechomwa sindano na alikuwa anatoa damu na kisha umeona wasichana wengine, watu wazima, wakisubiri kuja kuchomwa kwa sindano hiyo.

"Sio sindano pekee wanazogawana wanashiriki damu pia."

Bluetoothing pia imeripotiwa huko Afrika Kusini na Lesotho, nchi mbili ambazo zina baadhi ya viwango vya juu vya VVU duniani.

Fiji, tabia hiyo imekuwa maarufu katika miaka michache iliyopita, kulingana na bi Volatabu na bi Naitala.

Sababu moja ya umaarufu wake ni gharama ndogo: watu wengi wanaweza kushiriki kugawia gharama ya sindano moja na kila mmoja apate sehemu ya "kick" (athari ya dawa). Sababu nyingine ni urahisi wa kutumia sindano moja.

Hizi sindano ni vigumu kupata Fiji; maduka ya dawa, chini ya shinikizo la polisi, mara nyingi hutaka barua ya daktari kabla ya kutoa sindano, na hakuna programu za sindano safi na vifaa vya sindano.

Ingawa kukubalika kwa programu kama hizo kunazidi kuongezeka, ambazo hutoa vifaa safi vya sindano kwa watumiaji wa dawa ili kupunguza maambukizi ya virusi kupitia damu kama VVU.

Hata hivyo utekelezaji wake katika nchi inayoheshimu dini na yenye mitazamo ya kihafidhina imekuwa changamoto.

Volatabu anasema kuna "upungufu mkubwa" wa maeneo ya kupata sindano safi, ambayo inachochea vitendo hatarishi kama kugawana sindano na bluetoothing na kuacha NGO ziongeze juhudi za kusambaza sindano na kondomu.

Agosti 2024, Wizara ya Afya na Huduma za Matibabu ya Fiji ilitambua bluetoothing kama mojawapo ya sababu zinazoendesha ongezeko la visa vya VVU nchini humo.

Sababu nyingine ilikuwa chemsex, ambapo watu hutumia dawa mara nyingi methamphetamine kabla ya na wakati wa ngono.

Huko Fiji, tofauti na nchi nyingi duniani, crystal meth hutumiwa kwa sindano ya kutolewa ndani ya mwili (intravenous injection).

Wizara pia iligundua kwamba kati ya visa vipya 1,093 vilivyorekodiwa katika miezi tisa ya kwanza ya 2024, 223 karibu asilimia 20% vilitokana na matumizi ya dawa kwa sindano.

Utumizi wa meth miongoni mwa watoto

Fiji imekuwa kituo kikuu cha kusafirisha crystal meth ndani ya maeneo ya Pasifiki kwa miaka 15 iliyopita.

Sehemu kubwa ya hili ni kutokana na eneo la kijiografia kati ya Asia ya Mashariki na Amerika baadhi ya maeneo makubwa ya kutengeneza dawa na Australia na New Zealand soko lenye malipo ya juu.

Katika kipindi hicho, meth imeenea ndani ya jamii za ndani, na ikawa shida ambayo, kama VVU, hivi karibuni ilitangazwa "hali ya dharura ya kitaifa".

Na kulingana na wale wanaofanya kazi mitaani, umri wa watumiaji unashuka chini zaidi.

"Tunaona vijana wengi zaidi," anasema Volatabu. "umri unaendelea kupungua."

Takwimu za kitaifa za hivi karibuni za VVU nchini Fiji zinaonyesha matumizi ya dawa kwa sindano kama njia maarufu zaidi inayojulikana ya maambukizi, ikichangia asilimia 48% ya visa.

Maambukizi kwa njia ya ngono yalichangia asilimia 47%, wakati kuambukizwa kutoka kwa mama hadi mtoto wakati wa ujauzito na wakati wa kujifungua kulizungumziwa kama chanzo cha visa nyingi za watoto.

Wote waliozungumziwa na BBC wanakubaliana kwamba ukosefu wa elimu ni sababu kuu ya mlipuko huu.

Bi Volatabu na Naitala wanajitahidi kubadilisha hali hiyo na Bi. Naitala anasema kwamba kadri uelewa kuhusu hatari za VVU unapoongezeka katika jamii, bluetoothing imeanza kupuuzwa katika nchi yake.

Watu wengi zaidi wanajiandikisha kupimwa na kutafuta matibabu kwa VVU, jambo ambalo limefanya data kuwa nguvu zaidi kuhusu ukubwa wa mzozo.

Lakini bado kuna woga kwamba idadi rasmi ya visa ni kidogo tu ya tatizo lote na woga wa kile kilicho halisi.

Poromoko la tumaini

José Sousa‑Santos, mkuu wa Kituo cha Usalama wa Kanda ya Pasifiki katika Chuo Kikuu cha Canterbury, New Zealand, anasema "dhoruba kamili inajikusanya".

"Waswasi ni kwa ngazi zote jamii na serikali kuhusu mzozo wa VVU wa Fiji si tu kilichotokea sasa, bali kila utakavyokuwa katika miaka mitatu ijayo na kushindwa kwa rasilimali za Fiji," anasema kwa BBC. "Vyombo vya msaada kama vile uuguzi, uwezo wa kusambaza au kupata dawa za matibabu ya VVU havipo kwa kiwango kinachotosha."

"Hicho ndicho kinachotutisha sisi, watu wanaofanya kazi katika eneo hili: Fiji haiwezi kukabiliana na hili."

Baada ya kutangaza mlipuko Januari, serikali ya Fiji imeanza kuboresha ufuatiliaji wa VVU na kuongeza uwezo wake wa kushughulikia uwezekano wa visa ambavyo haviripotiwi rasmi.

Shirika la Global Alert and Response Network, lililoombwa kutoa msaada huo, limesema katika ripoti ya hivi karibuni kwamba "kuzishughulikia masuala haya yenye dharura kwa njia ya mtazamo wa kitaifa uliofanana ni muhimu kurejesha mwelekeo wa mlipuko wa VVU Fiji".

Ripoti hiyo pia ilitaja kwamba upungufu wa wafanyakazi, matatizo ya vifaa vya maabara na upungufu wa vitu muhimu kama vipimo vya haraka vya VVU na dawa, vinasababisha ucheleweshaji wa uchunguzi, utambuzi na matibabu.

Ukusanyaji wa data ni polepole, mgumu na mara nyingi wenye makosa jambo linalokwamisha juhudi za kuelewa wingi wa mlipuko wa VVU na ufanisi wa hatua zinazoingizwa.

Hii inawaacha wataalamu wengi, mamlaka, na Wafiji wengi bila taarifa kamili. Na Bwana Sousa‑Santos anatarajia "mrundiko mkubwa" wa maambukizi bado unatokota.

"Tunachoona kwa sasa ni mwanzo wa mrundiko huo, lakini huwezi kuizuia, kwa sababu maambukizi tayari yanatokea sasa, au tayari yamekutokea tu hatutauona watu wanapimwa kwa miaka miwili hadi mitatu ijayo," asema.

"Hakuna kitu ambacho tunaweza kufanya kwa sasa kukomesha idadi ya maambukizo ambayo tayari yametokea katika mwaka uliopita, na ambayo yanatokea sasa. Hilo ndilo jambo la kutisha sana."

Soma pia:

Imetafsiriwa na Mariam Mjahidi na kuhaeieiwa na Ambia Hirsi