Emmerson Mnangagwa ashinda urais Zimbabwe

Emmerson Mnangagwa

Chanzo cha picha, Reuters

Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa amechaguliwa kwa muhula wa pili baada ya ushindi wa 52.6% ya kura zilizopigwa katika uchaguzi mkuu, kwa mujibu wa tume ya uchaguzi.

Hatahivyo upinzani umedai kwamba kumekua na udanganyifu mkubwa na waangalizi wa kimataifa wanasema uchaguzi huo haukukidhi viwango stahiki vya demokrasia.

Mnangagwa ni rais wa tatu wa Zimbabwe. Mapinduzi ya 2017 dhidi ya kiongozi mkongwe Robert Mugabe yalimpatia nafasi ya kuiongoza nchi.

Raia wa Zimbabwe bado wanakabiliwa na kupanda kwa gharama ya maisha, umaskini na wimbi la hofu.

Alipoidhinishwa kuwa rais kwa mara ya kwanza, Mnangagwa – ambaye pia anajulikana kama "Mamba" aliahidi mwanzo mpya kwa raia wa nchi yake.

Lakini Zimbabwe ni nchi mojawapo iliokabiliwa na mfumko wa bei wa kiwango cha juu duniani mwezi uliopita – bei za bidhaa Julai zilipanda kwa 101.3% tangu mwaka uliopita.

Bado kuna ukosefu wa ajira wakati ni 25% ya wananchi walio na kazi rasmi.

Ahadi ya Mnangagwa kuhakikisha haki za binaadamu pia inaonekana kutokuwa na mashiko, huku kukiwa na mageuzi kidogo tangu kuondoka kwa Mugabe.

Wapiga kura Zimbabwe

Chanzo cha picha, Reuters

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Wakosoaji wanasema kiongozi huyo wa miaka 80 amenyamazisha na kukandamiza upinzani kuelekea uchaguzi huo ambao alitarajiwa pakubwa kushinda.

Tume ya uchaguzi Zimbabwe (ZEC) inasema mpinzani mkuu wa Mnangagwa mgombea kutoka chama cha Citizens' Coalition for Change (CCC) Nelson Chamisa, alijinyakulia 44% ya kura.

Mnangagwa alijipatia zaidi ya kura milioni 2.3, naye Chamisa akijipatia kura milioni 1.9, kwa mujibu wa ZEC. Idadi ya watu waliojitokeza kupiga kura katika nchi ilio na jumla ya raia milioni 16 ilikuwa ni 69%, tume hiyo imesema.

Upinzani unadai kulikuwa na udanganyifu, lakini mahakama ya katiba imeidhinisha matokeo hayo.

Msemaji wa chama cha CCC aliandika katika mtandao X – uliofahamika awali kama Twitter – kwamba chama hicho kimekataa " matokeo yoyote yaliokusanywa kwa haraka pasi kuhakikiwa".

Promise Mkwananzi, msemaji wa chama hicho ameliambia shirika la habari la AFP kwamba chama hicho hakikutia saini matokeo ya mwisho ya "uongo" na "hakiwezi kukubali matokeo hayo".

Amesema chama hicho kitatangaza hatua inayofuata.

Waangalizi kutoka Umoja wa Ulaya, Jumuiya ya madola na jumuiya ya SADC yenye nchi wanachama 16 wamesema walikuwa na malalamiko kadhaa kuhusu uchaguzi huo ikiwemo kupigwa marufuku upinzani kuandaa mikutano ya kisiasa, matatizo katika daftari ya wapiga kura, vyombo vya habari kuangazia uchaguzi huo kwa upendeleo na unyanyasaji wa wapiga kura.

Hapakushuhudiwa ghasia katika siku kuelekea uchaguzi huo, lakini wanachama wa CCC walishtakiwa kwa wanachokitaja kuwa ni mashtaka ya uongo yalionuiwa kukidhalilisha chama hicho. Chama hicho kinasema polisi ilipiga marufuku mikutano yao kadhaa tangu Julai na takriban mikusanyiko 100 tangu chama hicho kuundwa Januari mwaka jana.

Mapema mwezi huu wafuasi 400 wa CCC akiwemo mgombea wa kiti cha ubunge, walikamatwa wakiwa wanafanya kampeni katika mji mkuu Harare.

Mauaji ya hivi karibuni ya mfuasi wa CCC ambayo yanatuhumiwa kutekelezwa na wafuasi wa chama cha Mnangagwa Zanu-PF yalizidisha malalamiko kuhusu haki za binaadamu.

Wakosoaji wanaendelea kukamatwa na kufikishwa mahakamani kwa kumtusi rais – makosa ambayo mtuhumiwa anaweza kuadhibiwa kwa kufungwa mwaka mmoja gerezani au kutozwa faini au kukabiliwa na adhabu zote hizo mbili.

Mnangagwa aliwahi kuhudumu kama Waziri wa usalama wa taifa - na alisimamia shirika la kijasusi nchini lililoshirikiana na jeshi kukandamiza wafuasi wa chama cha Zapu kilichopambana na chama cha Mugabe Zanu PF katika vita vya wenyewe kwa wenyewe miaka ya 80.

Maelfu ya raia wengi wao kutoka kabila la Ndebele, walioonekana kama wafuasi wa Zapu waliuawa katika kampeni iliojulikana kama Gukurahundi kabla ya vyama hivyo baadaye kuungana na kuunda chama cha Zanu-PF.

Mnangagwa amekana kuhusika katika mauaji hayo. Kama rais amejaribu kuidhinisha uwiano. Baadhi wanahisi kwamba matamshi yake hayana uzito kwa vidonda vya Matabeleland, lakini jitihada za kufukua miili na kuyazika upya zimekubaliwa.

Uchaguzi mkuu huo ulitarajiwa kufanyika Jumatano, lakini ulibidi kuongezwa siku hadi Alhamisi katika baadhi ya maeneo kutokana na kuchelewa kuwasilishwa makaratasi ya kupiga kura.

Uchaguzi wa Mnangagwa una maana kwamba chama cha Zanu-PF kimeiongoza Zimbabwe kwa miaka 43 tangu nchi hiyo ipate uhuru kutoka kwa Uingereza mnamo 1980.