Urusi inapanga kuichosha Ukraine kwa mashambulizi ya muda mrefu-Zelensky

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Ukraine anasema Urusi inapanga kampeni ya muda mrefu ya mashambulio ya ndege zisizo na rubani kwa nia ya kuivunja moyo Ukraine.
Volodymyr Zelensky alisema amepokea ripoti za kijasusi zinazopendekeza kwamba Moscow itaanzisha mashambulizi hayo kwa kutumia ndege zisizo na rubani za Shahed zilizotengenezwa na Iran.
Haya yanajiri baada ya Ukraine kufanya shambulio ambalo ilisema liliwaua mamia ya wanajeshi wa Urusi katika eneo la Donbas.
Katika hali nadra sana ya kukubali hasara kwenye uwanja wa vita, Urusi ilisema shambulio hilo liliua wanajeshi wake 63.
Akizungumza kutoka Kyiv katika hotuba yake ya usiku, Bw Zelensky alisema Urusi inapanga "kuichosha" Ukraine na wimbi la muda mrefu la mashambulizi ya ndege zisizo na rubani.
"Lazima tuhakikishe - na tutafanya kila kitu kwa hili - kwamba lengo hili la magaidi linashindwa kama wengine wote," alisema. "Sasa ni wakati ambapo kila mtu anayehusika katika ulinzi wa anga anapaswa kuwa muangalifu sana."
Mashambulizi ya ndege zisizo na rubani za Urusi dhidi ya Ukraine yanaonekana kuongezeka katika siku za hivi karibuni, huku Moscow ikianzisha mashambulio kwenye miji na vituo vya umeme kote nchini katika muda wa siku tatu zilizopita.
Bw Zelensky alisema idara ya ulinzi wa anga ya Ukraine tayari imeangusha ndege zisizo na rubani 80 zilizotengenezwa na Iran katika siku za mwanzo za mwaka wa 2023.
Urusi imekuwa ikilenga miundombinu ya nishati ya Ukraine kwa miezi kadhaa, ikiharibu vituo vya umeme na kuwatumbukiza mamilioni gizani wakati wa baridi kali nchini humo.
Kwingineko, Ukraine imethibitisha kuwa ilifanya shambulio katika eneo linalokaliwa la Donetsk, ambalo awali ilidai kuua wanajeshi 400 wa Urusi.
Maafisa wa Urusi walipinga takwimu hiyo, wakisema ni wanajeshi 63 pekee waliouawa. Hakuna dai lolote ambalo limethibitishwa, na ni vigumu kulifikia eneo la shambulio hilo .

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Shambulizi la Ukraine katika Siku ya Mwaka Mpya lilipiga jengo moja katika mji wa Makiivka, ambapo vikosi vya Urusi viliwekwa.
Ni nadra sana kwa Moscow kuthibitisha hasara yoyote kwenye uwanja wa vita.
Lakini hili lilikuwa shambulio baya sana, anasema mhariri wa BBC wa Urusi Steve Rosenberg, kwamba kukaa kimya pengine halikuwa chaguo.
Ni idadi kubwa zaidi ya vifo vilivyotambuliwa na Moscow katika tukio moja tangu vita kuanza miezi 10 iliyopita.
Katika taarifa yake siku ya Jumatatu, wizara ya ulinzi ya Urusi ilisema kuwa vikosi vya Ukraine vilirusha roketi sita kwa kutumia mfumo wa roketi uliotengenezwa na Marekani wa Himars kwenye jengo linalohifadhi wanajeshi wa Urusi. Wawili kati yao walipigwa risasi, iliongeza.
Igor Girkin, mchambuzi anayeunga mkono Urusi, alisema mapema kwamba mamia ya watu waliuawa na kujeruhiwa, ingawa idadi kamili haikujulikana kwa sababu ya idadi kubwa ambayo bado haijapatikana.
Jengo lenyewe "lilikaribia kuharibiwa kabisa", alisema.
Aliongeza kuwa wahasiriwa walikuwa hasa askari waliosajiliwa - yaani, walioandikishwa hivi karibuni, badala ya wale waliojitolea kupigana. Pia alisema risasi zilihifadhiwa katika jengo moja na askari hao na kufanya uharibifu kuwa mbaya zaidi.
Girkin ni mwanablogu mashuhuri wa kijeshi, ambaye aliongoza waasi wanaoungwa mkono na Urusi walipoteka maeneo makubwa ya mashariki mwa Ukraine mwaka 2014. Hivi majuzi alipatikana na hatia ya mauaji kwa wajibu wake katika kuangusha ndege ya MH17 .
Licha ya msimamo wake mkali , mara kwa mara anakosoa uongozi wa kijeshi wa Urusi na mbinu zao.
Wabunge kadhaa wa Urusi pia wamewakosoa vikali makamanda wa kijeshi juu ya shambulio hilo, wakisema makamanda lazima wawajibishwe kwa kuruhusu wanajeshi kujilimbikizia katika jengo lisilo na ulinzi ndani ya safu ya roketi za Ukraine, ambapo risasi zinaweza pia kuwa zimehifadhiwa.
Sergei Mironov - mwenyekiti wa zamani wa Baraza la Seneti la Urusi - alisema ni dhahiri kwamba idara ya upelelezi na ile ya ulinzi wa anga hazikufanya kazi inavyostahili.
Kulingana na taarifa ya awali ya jeshi la Ukraine, 300 walijeruhiwa pamoja na wanaokadiriwa kufikia 400 waliouawa. Jeshi la Ukraine linadai, karibu kila siku, kuwaua makumi, wakati mwingine mamia ya wanajeshi katika mashambulizi.
Taarifa ya baadaye kutoka kwa mkuu wa jeshi la Ukraine ilisema "hadi vitengo 10 vya zana za kijeshi za adui" "viliharibiwa na kuangamizwa" katika shambulio hilo, na kwamba "hasara za wapiganaji wa wavamizi zinabainishwa".
Ukraine haijathibitisha mashambulio hayo yalifanywa kwa makombora ya Himars, ikidumisha mkakati wa muda mrefu wa kutotoa maelezo maalum kuhusu mashambulizi yake.










