Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kiongozi wa kundi la Wagner aapa kuwapindua viongozi wa kijeshi wa Urusi
Mkuu wa kundi la mamluki la Wagner nchini Urusi ameapa "kufanya kila awezalo" kupindua uongozi wa kijeshi wa Urusi, saa chache baada ya Kremlin kumshutumu kwa "uasi wa kutumia silaha".
Yevgeny Prigozhin alisema wapiganaji wake wa Wagner wamevuka mpaka kutoka Ukraine na kuingia katika mji wa Rostov-on-Don nchini Urusi.
Bw Prigozhin alisema wapiganaji wake watamuangamiza yeyote atakayejaribu kuwafungia njia.
Mkuu wa mkoa huo aliwataka wananchi kuwa watulivu na kusalia majumbani.
Bw Prigozhin alidai kuwa vikosi vyake viliidungua helikopta ya kijeshi ya Urusi ambayo "ilifyatulia risasi msafara wa raia". Hakutaja eneo na madai hayo hayajathibitishwa.
Kundi la Wagner ni jeshi la kibinafsi la mamluki ambalo limekuwa likipigana pamoja na jeshi la Urusi nchini Ukraine.
Mvutano umekuwa ukiongezeka kati yao kuhusu jinsi vita hivyo vinavyoendeshwa, huku Bw Prigozhin akikosoa uongozi wa kijeshi wa Urusi katika miezi ya hivi karibuni.
Siku ya Ijumaa, kiongozi huyo wa mamluki mwenye umri wa miaka 62 alishutumu jeshi kwa kuanzisha shambulio baya la kombora dhidi ya wapiganaji wake na kuahidi kuwa atawaadhibu. Hakutoa ushahidi.
Mamlaka imekanusha madai hayo na kumtaka kusitisha "vitendo vyake haramu".
Bw Prigozhin alisema "uovu" katika uongozi wa kijeshi wa Urusi lazima ukomeshwe na kuapa "kupigania haki".
"Waliowaua vijana wetu, na maelfu ya wanajeshi wa Urusi [katika vita vya Ukraine] wataadhibiwa," alisema katika ujumbe wa sauti uliowekwa katika mtandao wa kijamii wa Telegram.
"Nawaomba msipinge. Yeyote atakayefanya hivyo atachukuliwa kuwa tishio na kuangamizwa. Hiii inajumuisha vizuizi vyovyote na usafiri wa anga kwenye njia yetu.
"Nguvu ya rais, serikali, polisi na walinzi wa Urusi watafanya kazi kama kawaida.
"Haya si mapinduzi ya kijeshi, bali ni maandamano ya haki. Hatua zetu haziingilii wanajeshi kwa njia yoyote ile."
Rais wa Urusi Vladimir Putin anapokea taarifa za kila saa kuhusu hali hiyo, msemaji wake alisema.
Usalama mjini Moscow uliimarishwa siku ya Ijumaa usiku katika maeneo muhimu mjini Moscow, yakiwemo majengo ya serikali na vyombo vya usafiri, shirika la habari linalomilikiwa na serikali ya Urusi TASS lilisema.
Gavana wa eneo la Lipetsk nchini Urusi pia anawaomba wakaazi wasisafiri kuelekea kusini.
Lipetsk iko karibu kilomita 280 (maili 175) kaskazini-mashariki mwa mpaka wa Ukraine, na zaidi ya kilomita 500 kaskazini mwa Rostov.
Katika chapisho kwenye mtandao wa Telegram, Igor Artamonov alisema hatua za usalama katika eneo hilo zinaimarishwa, kwa kuzingatia hasa kulinda vifaa muhimu vya miundombinu.
Katika ujumbe wa Twitter mwishoni mwa Ijumaa, Wizara ya Ulinzi ya Ukraine ilisema kwa urahisi: "Tunayaangalia."
Ikulu ya White House ilisema inafuatilia hali hiyo na itashauriana na washirika wa Marekani.
Jenerali Sergei Surovikin, naibu mkuu wa vikosi vya Urusi nchini Ukraine, ambaye uongozi wake Bw Prigozhin ameusifu siku za nyuma, alimtaka "kusitisha msafara wa wapiganaji wake na kuwarejesha kwenye vituo vyao".
"Sisi ni damu moja, sisi ni wapiganaji," alisema kwenye video. "Haupaswi kufanya masihara na adui wakati ambao ni mgumu kwa nchi yetu."
Vyombo vya habari vya serikali ya Urusi viliripoti kwamba FSB, idara ya usalama ya Urusi, imefungua kesi ya jinai dhidi ya Bw Prigozhin, ikimtuhumu kwa "kuitisha uasi wa kutumia silaha" na kujaribu kuanzisha vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Urusi.
FSB pia inaripotiwa kuwataka wapiganaji wa Wagner kutotii amri yake na kuchukua hatua za kumkamata.
Wizara ya ulinzi ya Urusi ilisema katika taarifa yake kwamba "ripoti zote za Prigozhin zilizoenea kwenye mitandao ya kijamii" za mashambulizi ya Urusi dhidi ya kambi za Wagner "si za kweli ni uchochezi ".
Haya yanajiri baada ya ujumbe wa video mwezi Mei ambapo Bw Prigozhin alisimama akiwa amezungukwa na miili ya wanajeshi wake na kumkashifu waziri wa ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu - pamoja na Mkuu wa Majenerali Valery Gerasimov - kwa kutowapa silaha za kutosha.
Siku ya Ijumaa, alitangaza kwamba vita nchini Ukraine vilikuwa vimeanzishwa "ili Shoigu aweze kuwa kiongozi wa ngazi ya juu wa vikosi vya kijeshi ".