Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je, ni kweli mashambulizi ya anga yalilenga raia huko Tigray?
Na Peter Mwai
BBC Reality Check
"Nilikuwa nikitazama runinga na watoto wangu wakati ghafla shambulio la anga lilitupiga na kutuzika."
Takriban watu wanane waliripotiwa kufariki, huku makumi ya wengine wakijeruhiwa katika shambulizi la anga kwenye mji wa Adi Daero katika eneo la kaskazini mwa Ethiopia la Tigray, mwishoni mwa Septemba.
Adi Daero alikuwa karibu na vitani wakati huo kati ya Tigray People’s Liberation Front (TPLF), ambao wanadhibiti eneo hilo, na jeshi la Ethiopia na vikosi vya Eritrea vinavyowaunga mkono.
Ufikiaji wa eneo kwa wanahabari ni mdogo sana, kwa hivyo tumejaribu kuthibitisha kilichotokea kwa kutumia ushuhuda wa watu waliojionea, picha za video na picha za setilaiti za eneo hilo.
Nini kimeripotiwa kuhusu shambulio hilo?
TPLF inasema jeshi la anga la Eritrea lilishambulia kwa mabomu eneo la makazi ya watu huko Adi Daero.
Wanasema "ilirusha mabomu... na kuua raia, huku wengine zaidi wakijeruhiwa na kufanya nyumba za makazi kubadilika na kuwa majivu".
Afisa mkuu wa Tigray, Kindeya Gebrehiwot, anadai kuwa ndege ya Eritrea MiG-29 ilihusika shambulizi hilo.
"Walipokuja kuchimba ili kututoa, niliwaomba kuwaokoa watoto kwanza" alisema mwanamke mmoja katika ripoti kwenye kituo cha televisheni cha Tigray.
"Binti yangu mjamzito Beyenesh alitolewa nje akiwa hana fahamu huku anavuja damu. Waliniambia mjukuu wangu Michiwti amefariki dunia papo hapo."
Serikali ya Ethiopia imesema ndege zake zilishambulia mji huo, lakini inasisitiza kuwa ziligonga tu shabaha za kijeshi zinazohusishwa na TPLF.
Taasisi inayounga mkono serikali ya Ethiopia ya Uchunguzi Kuhusu Masuala ya Sasa imeishutumu TPLF kwa kutoa "madai potofu" kwamba raia walikuwa wanalengwa.
"Vikosi vya Ulinzi vya Kitaifa vya Ethiopia vinahakikisha kuwa mali za kijeshi zimetengwa na raia kabla ya kuchukua hatua," taarifa kwenye Twitter inasema.
Ushahidi ni upi?
Kanda za video za shambulizi hilo zimeibuka, baadhi zikiwa zimechapishwa mtandaoni na timu ya televisheni ya eneo la Tigray.
Video moja inaonekana kuonyesha wakati eneo hilo lilipigwa mnamo 27 Septemba huko Adi Daero.
Pia kuna video iliyotolewa na vituo vya televisheni vya Tigray siku iliyofuata - 28 Septemba - inayoonyesha watu waliovaa kiraia wakitafuta manusura huku kukiwa na vifusi vya majengo yaliyoporomoka.
Wanawake na watoto wanaweza kuonekana kwenye video - wakati mmoja, mwanamke anachimbwa ili kutolewa nje ya kifusi.
Kuna wanaume wawili waliovalia kiraia kila mmoja akiwa na bunduki, lakini hatujui ni akina nani.
Wale waliohojiwa katika video hiyo wanaelezea siku tulivu wakati wa tamasha la kidini la Meskel, ambalo linaashiria kupatikana kwa msalaba ambao Yesu alisulubishwa, kulingana na mila ya Wakristo wa Orthodox.
"Hatukufikiria hili lingetokea. Hakuna shughuli za kijeshi hapa. Hiki ni kitongoji cha watu maskini," mwanamke mmoja aliiambia televisheni ya Tigray.
Kuna vidokezo katika video, ambavyo vilitusaidia kuthibitisha ilikuwa kutoka kwa Adi Daero.
Video moja inaonyesha safu ya kipekee ya vilima kwa nyuma, ambayo inalingana na kilima kilicho magharibi mwa mji kama inavyoonekana kwenye Ramani za Google.
Kwenye kamera ya mtu anayepiga picha, mnara wa msikiti unaweza kuonekana kwa muda mfupi.
Hii inalingana na mnara unaoonekana kwenye picha za Adi Daero zilizochapishwa kwenye Ramani za Google mapema mwaka huu.
Msikiti huo uko kaskazini mwa eneo ambalo lilishambuliwa na linaweza kutambuliwa kwenye Google Earth na kuba la kijani kibichi.
BBC pia imeangalia picha za satelaiti za eneo hilo kabla na baada.
Hizi zinaonyesha wilaya ya makazi iliyojengwa ya mitaa yenye ulinganifu iliyo na majengo, na kwenye picha za satelaiti kutoka 1 Oktoba, uharibifu wa eneo moja unaonekana wazi.
Picha kutoka mwanzoni mwa mwaka wa mtandao huo wa barabara hauonyeshi dalili yoyote ya uharibifu.
Je, serikali ya Ethiopia imesema nini?
Tumewauliza viongozi wa Ethiopia ni nini kililengwa na wanajeshi katika eneo la Adi Daero wakati huo, lakini hatujapata jibu.
Tarehe 17 Oktoba, taarifa rasmi ilitolewa ikisema jeshi "linajitahidi kuepuka operesheni za kivita katika maeneo ya mijini ili kuzuia majeruhi ya raia."
Na inaishutumu TPLF kwa kutumia raia kama ngao za binadamu na vifaa vya kiraia kwa vituo vya kijeshi.
"Serikali ya Ethiopia inajutia sana madhara yoyote ambayo yanaweza kuwa yamefanywa dhidi ya raia...na itachunguza matukio kama hayo, "inasema.
Mashambulizi ya angani yamekuwa yakitokea katika maeneo mengine ya eneo hili, lakini kukatika kwa mawasiliano hali ambayo bado inaendelea kushuhudiwa kumefanya iwe vigumu sana kuthibitisha maelezo.
Kamati ya Kimataifa ya Uokoaji inasema mfanyakazi anayefanya kazi na shirika hilo aliuawa tarehe 14 Oktoba wakati wa shambulio katika mji wa Shire, kusini mwa Adi Daero.
Madai ya kuuawa kwa raia katika matukio mengine pia yameibuka, lakini imekuwa vigumu kuthibitisha haya.