Wafanyakazi wa Al Jazeera wadai unyanyasaji na uonevu haukupewa kipaumbele

Kamahl Santamaria, mwanahabari mkongwe wa televisheni, alikuwa na siku 32 tu katika kazi yake katika kituo kikuu cha utangazaji cha New Zealand TVNZ alipojiuzulu.

Mshangao ulileta mshtuko huku madai kuhusu tabia yake isiyofaa katika chumba cha habari yakiibuka.

Hivi karibuni wafanyakazi wenzake wa zamani wa Al Jazeera, ambako alikuwa amefanya kazi kwa miaka 16, walianza kuzungumza.

Uchunguzi wa BBC - ukizingatia mahojiano na wafanyikazi kadhaa wa sasa na wa zamani wa Al Jazeera, na ushahidi wa maandishi wa ujumbe usiofaa na malalamiko ya wafanyikazi - umegundua madai kadhaa ya unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya Bw Santamaria katika chumba cha habari cha shirika la utangazaji Doha.

Wengine wanasema hakuwa peke yake.

Pia wanashutumu shirika hilo kwa kukuza utamaduni mbaya wa kazi ambapo malalamiko ya unyanyasaji, ubaguzi wa kijinsia, uonevu na ubaguzi wa rangi kwa kiasi kikubwa hayapatiwi ufumbuzi.

Waliozungumza na BBC walitaka kutotajwa majina yao kwa sababu walihofia kuwa ingeathiri kazi zao.

Majina yao yamebadilishwa.

Bw Santamaria hakujibu moja kwa moja BBC.

Lakini alitoa taarifa kwa umma ambapo alikiri madai yaliyoripotiwa hapo awali, akisema baadhi ni "kweli, mengine hayana muktadha muhimu, baadhi ni ya uongo wa wazi na kuandika upya historia".

Kujibu madai yaliyotolewa na BBC, alikiri na kuomba msamaha kwa "tabia ambayo inaweza kuwa ilimfanya mtu yeyote akose raha" na kile alichokiona kuwa "kutaniana, urafiki kupita kiasi, kupiga domo kidogo tu, au tu kuwa ndani ya mipaka inayokubalika katika utamaduni uliopo wa chumba cha habari, kwa kweli, haikuwa hivyo".

BBC iliitumia Al Jazeera orodha ya kina ya madai 22 ambayo ilikuwa imefichua, lakini shirika hilo la utangazaji halikuzishughulikia kibinafsi, badala yake lilisema "inawachukulia wafanyikazi wake ulimwenguni kote kama uti wa mgongo na msingi wa shirika - usalama wao na ustawi wao ni wa umuhimu wa hali ya juu".

Iliongeza: "Kama shirika la kimataifa lenye zaidi ya mataifa 95, tunajitahidi daima kujenga mazingira mazuri ya kazi kwa wote".

Wafanyikazi pia waliambia BBC wanatatizika kuzungumzia masuala hayo nchini Qatar, jimbo dogo lenye utajiri wa gesi katikati mwa Ghuba ambalo limekosolewa kwa rekodi yake kuhusu haki za binadamu na usawa wa kijinsia.

Wengi walionyesha tofauti kati ya kuondoka kwa Bw Santamaria kutoka Al Jazeera – ujumbe wa Twitter ambao uliashiria mwisho wa mafanikio ya miaka 16 - na kuondoka kwake kwa haraka kutoka TVNZ, inaonekana kulazimishwa kutokana na msururu wa madai.

'Ilinibidi kufuta mate yake usoni mwangu'

Bw Santamaria, ambaye alianza kazi yake kama ripota wa TV nchini New Zealand, aliajiriwa na Al Jazeera mwaka wa 2005 kama mtangazaji katika idhaa ya lugha ya Kiingereza huko Doha.

Alipanda vyeo haraka, akiangazia masuala ya ulimwenguni kote kama vile uchaguzi wa rais wa 2020 wa Marekani na programu kuu.

Wale waliomfahamu wanasema alikuwa mtu aliyependa urafiki na wengine, "mtangazaji wa kipekee".

Tory alikuwa mtayarishaji vipindi kijana katika shirika la Al Jazeera aliposema alianza kumjali asivyotakiwa.

Anasema angemtumia ujumbe kwenye Twitter akisema anapatikana kwa kumbembeleza na kumuuliza kwa nini hakuwa amemwalika kwenye likizo yake.

BBC imeona ushahidi wa ujumbe usiofaa ambao Bw Santamaria alitumia wenzake kwenye Twitter, Whatsapp na barua pepe ya ndani ya Al Jazeera.

"Kisha likaja suala la kugusa wengine ofisini," Tory anasema.

"Mkono begani, kumbatio la ajabu, na mbaya zaidi: busu kwenye shavu. Kwa zaidi ya tukio moja nililazimika kwenda bafuni kufuta mate ya Kamahl kutoka kwa uso wangu."

Tory anasema alijadili tabia ya Bw Santamaria na mfanyakazi mwenzake mmoja na meneja wa ngazi ya kati, ambao wote wamethibitisha kwa BBC mazungumzo haya yalifanyika.

“Mwanaume mtaalamu katika chumba cha habari makini hatakiwi kuambiwa, zaidi ya mara moja, asimtumie mwenzake ujumbe kuhusu jinsi anavyopendeza au kuangazia ‘matiti’ yake au kumwalika kumbembeleza hata akidhani kuwa ni ‘marafiki’", Tory anasema.

Zaidi ya mtu mmoja ameambia BBC kwamba Bw Santamaria alitoa maoni kuhusu matiti ya wafanyakazi wenzake.

Wenzake kadhaa wa sasa na wa zamani wanadai kuwa tabia ya Bw Santamaria ilikuwa na mashahidi zaidi ya tukio moja.

Mfanyikazi wa kiume ambaye kwa sasa anafanya kazi katika shirika la Al Jazeera alisema Bw Santamaria alimbusu mdomoni, bila kualikwa, kwenye chumba cha habari.

Mhariri wa habari, ambaye sasa ni kiongozi mkuu, katika kituo hicho inadaiwa alishuhudia.

Mtayarishaji mwingine wa zamani alisema Bw Santamaria alimbusu shingoni akiwa kazini - mbele ya watu wengi.

"Nilijisikia aibu na kufadhaika na kuwa na wasiwasi sana kwamba watu wangefikiria nilijihusisha naye au kujaribu kuwa karibu naye - bado nilikuwa natafuta marafiki, sikuwa na mtu yeyote katika usimamizi ambaye ningeweza kuzungumza naye," alisema.

Wengi wao walielezea tabia ya Bw Santamaria kuwa ya ushupavu, lakini wanasema hawakuwahi kuripoti kwa sababu walimwona kama nyota katika kujuana na wengine wengi, wakati walikuwa wakianzia maisha Mashariki ya Kati.

Fiona, ambaye alikuwa mfanyakazi huru wa Al Jazeera kwa miaka minne, alisema Bw Santamaria alijaribu kumkumbatia katika chumba cha habari, kutoa maoni ya ngono na kutuma ujumbe usiofaa - tabia aliyoiita "utumiaji wa lugha ya ngono".

Hakulalamika rasmi, lakini anasema aliripoti juu ya tabia yake kwa meneja wa ngazi ya kati ambaye alisema, "Loo, usiniambia bado anaendelea na tabia hiyo?".

Anasema aliulizwa kama alitaka kuwasiliana na ofisi ya rasilimali watu yaani HR lakini hakutaka kwa sababu alikuwa kwenye mkataba wa muda mfupi.

Anasema, kisha alishauriwa kumpuuza Bw Santamaria.

Aliacha kuongea naye baada ya hapo, anaongeza, lakini aliwaonya wafanyikazi wapya juu yake.

Madai hayo yalipojulikana mapema mwaka huu, anasema alipatwa na hofu.

"Nilimripoti miaka sita iliyopita, na hakuna hatua iliyochukuliwa", anasema.

"Amefanyia hivi watu wangapi zaidi tangu wakati huo?"

'Niliogopa kazi yangu'

Fiona na wengine wanauliza kwa nini malalamiko yao dhidi ya Bw Santamaria hayakupelekea Santamaria kuanza kuchunguzwa - tofauti na TVNZ, ambayo ilipitia upya uajiri wake mara tu madai yalipoibuka.

TVNZ iligundua kuwa mchakato wa kuajiri haukutosha kuajiri watangazaji "muhimu" na mkuu wa habari ambaye alimuajiri Bw Santamaria akajiuzulu.

Sasa hivi inaonekana kuna kitu kinachoendelea katika shirika la Al Jazeera, ambapo BBC imegundua kuwa madai hayo ni zaidi ya Bw Santamaria na chumba cha habari.

Mtayarishaji wa zamani na mwandishi wa habari anasema takriban wanaume wawili isipokuwa Bw Santamaria walimnyanyasa.

Anasema mmoja alikuwa mkuu ambaye angemwomba aende naye nyumbani kwake wakati mke wake hayupo nyumbani, na mwingine alikuwa mkuu wake wa kazi moja kwa moja.

"Niliogopa sana kwamba kama ningekataa madai yake, angeweza kumaliza kazi yangu," alisema.

Wanawake na wanaume wengi katika idara nyingine huko Al Jazeera pia wamedai unyanyasaji dhidi ya wakuu wa ngazi ya kati.

"Amesema mambo yasiyofaa zaidi - aliwauliza wafanyakazi wa kiume wanapata lini mke wa pili au ikiwa wamepoteza ubikira wao. Alizungumza kuhusu ngono wakati wa Ramadhani na kuwauliza waliovaa hijabi nywele zao ni za rangi gani," mmoja wa wanawake hao alisema.

Alisema mmoja wa wafanyakazi wenzake amejiuzulu kwa sababu hii.

BBC ilizungumza na mfanyakazi mwingine ambaye alithibitisha kushuhudia unyanyasaji na mtu huyu.

Mtu huyu sasa ameondoka Al Jazeera, kulingana na watu wa idara yake - miezi kadhaa baada ya madai dhidi yake kuibuka.

'Sote tulinyamaza'

"Watu wana hasira juu ya kila aina ya mambo na hawahisi kuwa wanaweza kuzungumza katika shirika la Al Jazeera na hasa Qatar," David, mfanyakazi wa zamani ambaye anasema alijiuzulu kwa sababu ya uonevu na unyanyasaji.

Anasema yeye na wengine walidhalilishwa hadharani.

Anasema mwanamke huyo pia "alimdharau" na mara nyingi tu kila wakati "alikemea" wenzake wakuu kwenye mikutano.

Kila mtu kwenye timu, pamoja na watayarishaji wa vipindi wakuu, "walimuogopa", kulingana na David, kwa sababu ya "utawala" wake na "ufidhuli".

Lakini, anaongeza, wachache walilalamika juu yake kwa sababu alikuwa karibu na meneja mkuu.

"Sote tulinyamza", mfanyakazi mwingine wa sasa alisema.

"Maneno ya uchungu yanatolewa na wafanyakazi wa zamani na wa sasa."

Wafanyakazi kadhaa wamekuwa wakinyanyaswa na kuonewa kwa "miaka na miaka na miaka", kulingana na Liam, ambaye anafanya kazi katika chumba cha habari cha Doha.

BBC pia imefahamu kuhusu madai ya uonevu katika chumba cha habari cha Al Jazeera mjini London.

Na takriban watu wawili walielezea tukio katika ofisi nyingine, ambapo mkuu wa ofisi wa kiume alimsukuma mwandishi mdogo wa kike na kusababisha kuanguka.

"Kamahl ndiye alikuwa kichocheo," David anasema.

Wafanyikazi wa sasa wanasema kwamba tangu madai hayo katika TVNZ kuibuka, usimamizi umefanya mikutano pamoja na HR - lakini Liam aliyataja kuwa "upuuzi", akiongeza kuwa bado hakuna uchunguzi wowote uliotajwa.

Kila mtu BBC ilizungumza naye alisema wanaogopa kuzungumza kwa sababu kila nyanja ya maisha yao inahusishwa na kazi zao.

Mfumo wa kuajiri nchini Qatar unaunganisha visa ya kazi, shule ya watoto, nyumba na manufaa mengine kwa kampuni maalum - hivyo wafanyakazi wanatatizika kuacha kazi za unyanyasaji, alisema Marti Flacks, mfanyakazi mkuu katika Kituo cha Mafunzo ya Kimkakati na Kimataifa.

Pia wanasitasita kuripoti tabia ya matusi na isiyofaa, aliongeza Bi Flacks, kwa sababu wanakabiliwa na "changamoto za kupata suluhisho madhubuti, kama vile fidia".

Wakati Al Jazeera inasema ni huru, inafadhiliwa na Emir wa Qatar na waandishi wake wa habari hawaripoti kila nyanja ya serikali.

Sheria za mitaa pia huzuia uhuru wa kujieleza.

'Kila mtu alijua kuhusu Kamahl'

Wafanyikazi wanasema wana imani kidogo kwamba madai hayo yatasababisha mabadiliko katika shirika la Al Jazeera, ambapo wanashutumu wakuu kwa kutochukua hatua kwa miaka.

"Usimamizi na ofisi ya Raslimali watu hakika walijua kuhusu suala la Kamahl Santamaria," alisema Katie Turner, mhariri wa zamani wa habari katika Al Jazeera huko Doha.

Hakuwahi kulengwa lakini amekuwa akiongea kuhusu kile alichokishuhudia huko Al Jazeera.

Ofisi ya Raslimali watu ya Al Jazeera ilikuwa imepokea malalamiko ya unyanyasaji katika chumba cha habari, kulingana na yeye.

Wakati wa mahojiano yake ya kuondoka, aliposita kabla ya kumtaja Bw Santamaria, anasema mkuu wa HR aliuliza ikiwa ni kiongozi mwingine mkuu.

"Ni wakati huo ndipo nilipogundua kuwa kulikuwa na shida kubwa," anaongeza.

BBC imeona barua pepe kutoka mwaka 2016 ikiashiria unyanyasaji wa kijinsia, uonevu, upendeleo na tabia mbaya - iliyotumwa kwa mhariri wa habari, ambaye sasa ni meneja mkuu.

Alijibu akisema angeichukua juu zaidi, na kuongeza "Natumai itafika kwa Sheikh," akimaanisha uongozi wa juu.

Lakini wafanyakazi wasiopungua 10 waliiambia BBC mkurugenzi wa habari alikuwa anajua, na waliendelea kumpa Bw Santamaria fursa ya kuendelea kutangaza.

Wafanyikazi ambao BBC ilizungumza nao wanasema kwamba mameneja wakuu hawakuwa na vifaa vya kutosha kukabiliana na uonevu na unyanyasaji, na kwamba sera ya HR haikuwa wazi.

David anasema alipolalamikia uonevu na unyanyasaji katika chumba cha habari, aliambiwa uongozi ulichunguza malalamiko yake, na hatimaye kumhamisha mshtakiwa katika idara tofauti, pamoja na majukumu yake yote kama kawaida.

"Ni wakati tu nilipojiuzulu na kuwa na mahojiano ya kuondoka ndipo niligundua HR haikuwa imehusika katika mchakato huo," David alisema.

Kujibu ombi la BBC la kutoa maoni, Al Jazeera ilisema: "Sera zetu za kupinga unyanyasaji ziko wazi, pana, na ni kwa wafanyikazi wote. Kama inavyoonekana katika visa kadhaa vya hivi karibuni, kila malalamiko rasmi ya wafanyikazi wetu yanazingatiwa kwa uzito mkubwa na hatua stahiki zilizochukuliwa baada ya uchunguzi wa kina wa madai yanayotolewa."

Waathiriwa wanasema kupuuzwa kwa sera, "utamaduni wa kusamehe" na ulinzi wa "watu wanaochukuliwa kuwa juu ya sheria" ni jambo la kukatisha tamaa sana mnamo mwaka 2022 - haswa katika chumba cha habari cha kimataifa kama cha Al Jazeera, na haswa kufuatia harakati za vuguvugu #MeToo movement, mtandao uliiripoti hilo kwa upana.

"Mnamo mwaka 2022, kuna kikomo cha juu cha kile wasimamizi wakuu wanaweza kujiepusha nacho," mfanyakazi wa sasa alisema.

"Katika shirika la Al Jazeera, hakuna kikomo cha juu."

Majina ya waathiriwa wote yamebadilishwa kwa ombi ili kulinda utambulisho wao.