Fahamu Faida 9 za Kabichi Kiafya

Chanzo cha picha, Getty Images
Kabichi ina lishe bora na yenye vitamini C, nyuzinyuzi, na vitamini K. Watafiti wanapendekeza kwamba inaweza kuwa na manufaa ya kiafya ambayo ni pamoja na kusaidia usagaji chakula na afya ya moyo, miongoni mwa mengine.
Licha ya kuwa na virutubisho vyenye lishe ya kuvutia, kabichi mara nyingi hupuuzwa.
Ingawa inaweza kuonekana kama mboga za lettusi, kwa hakika ni aina ya mboga za Brassica, ambayo ni pamoja na broccoli na figili.
Huwa katika maumbo na rangi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na nyekundu, zambarau, nyeupe, na kijani, na majani yake yanaweza kujikunja au kuwa laini.
Mboga hii hulimwa duniani kote kwa maelfu ya miaka na inaweza kupatikana katika mapishi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na sauerkraut, kimchi, na coleslaw.
Zaidi ya hayo, kabichi imejaa vitamini na madini.
Nakala hii inafichua faida 9 za kiafya za kabichi, zote zikiungwa mkono na sayansi.
1. Kabichi imejaa virutubisho

Chanzo cha picha, Getty Images
Ingawa kabichi ina kalori chache sana, ina virutubishi vinavyovutia.
Kwa kweli, kikombe 1 tu, au gramu 89 (g), ya kabichi mbichi ya kijani ina lishe zifuatazo;
- Kalori: 22
- Protini: 1 g
- Nyuzinyuzi: 2 g
- Vitamini K: 56% ya (DV)
- Vitamini C: 36% ya DV
- Folate: 10% ya DV
- Manganese: 6% ya DV
- Vitamini B6: 6% ya DV
- Kalsiamu: 3% ya DV
- Potasiamu: 3% ya DV
- Magnesiamu: 3% ya DV
Kabichi pia ina kiasi kidogo cha virutubisho vingine, ikiwa ni pamoja na vitamini A, chuma, na riboflauini.
Kama unavyoona katika orodha iliyo hapo juu, ina vitamini B6 na asidi nyingi, zote mbili ni muhimu kwa michakato mingi muhimu mwilini, ikijumuisha Mabadiliko ya kemikali yanayotokea katika seli na utendakazi wa kawaida wa mfumo wa neva kwa mujibu wa wataalamu.
Kwa kuongezea, kabichi ina nyuzinyuzi nyingi na ina vioksidishaji vikali, ikijumuisha polyphenols na madini ya salfa.
Kabichi ina vitamini C nyingi,yenye nguvu inayosaidia kulinda mwili dhidi ya magonjwa ya moyo, aina kadhaa za saratani, na kupoteza uwezo wa kuona.
2. Inaweza kusaidia kudhibiti kuvimba
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kuvimba sio jambo baya kila wakati.
Kwa kweli, mwili wako hutegemea vichocheo ili kujilinda dhidi ya maambukizi au kuharakisha uponyaji.
Aina hii ya kuvimba kwa papo hapo ni hali ya kawaida panapotokea jeraha au maambukizi.
Kwa upande mwingine, uvimbe unaotokea kwa muda mrefu unahusishwa na magonjwa mengi, ikiwa ni pamoja na ugonjwa wa moyo, ugonjwa wa kukakamaa viungo na ugonjwa wa maambukizi katika utumbo.
Mboga kama kabichi zina madini ambayo husaidia kupunguza kuvimba kwa muda mrefu.
Kwa kweli, utafiti mmoja wa 2014 uliojumuisha vijana walio na umri wa miaka 20-40 ulionyesha kuwa kula mboga za aina ya kabichi kunaweza kupunguza alama fulani za damu kuvimba.
Utafiti mwingine wa zamani kwa zaidi ya wanawake 1,000 ulionyesha kuwa wale waliokula kiasi kikubwa cha mboga za jamii ya kabichi walikuwa na viwango vidogo vya kuvimba, ikilinganishwa na wale waliokula kabichi kwa kiasi cha chini zaidi.
Sulforaphane, kaempferol, na vioksidishaji vingine vinavyopatikana katika kundi hili la mimea husaidia kuzuia makali ya kuvimba inapotokea jeraha au maambukizi.
3. Kabichi imejaa vitamini C
Vitamini C, pia inajulikana kama asidi ascorbic, ni vitamini iliyokatika hali ya majimaji ambayo hufanya kazi nyingi muhimu katika mwili.
Kwa mfano, inahitajika kutengeneza collagen, protini nyingi zaidi mwilini. Collagen hutoa muundo na unyumbulifu kwa ngozi na ni muhimu kwa utendakazi mzuri wa mifupa, misuli na mishipa ya damu.
Zaidi ya hayo, vitamini C husaidia mwili kunyonya madini chuma ,inayopatikana katika vyakula vya mimea.
Kwa kuongezea, ni antioxidant yenye nguvu. Kwa kweli, imefanyiwa tafiti mbalimbali na kusifika sana kwa kupambana na saratani.
Vitamini C hufanya kazi kulinda mwili kutokana na uharibifu unaosababishwa na athari ambazo zimehusishwa na magonjwa mengi sugu,ikiwemo saratani.
Ushahidi unaonyesha kuwa lishe iliyo na vitamini C nyingi husaidia sana kupunguza hatari inayosababishwa na saratani.
Ingawa tafiti nyingi zimegundua kuna uhusiano kati ya ulaji zaidi wa vitamini C na kupungua kwa hatari ya kupata saratani.
Japo matokeo ya tafiti yamekuwa yakitofautiana.
Ingawa utafiti zaidi unahitajika ili kujua athari ya vitamini hii katika kuzuia saratani, ni hakika kwamba vitamini C ina umuhimu mkubwa katika kulinda mwili.
Ingawa kabichi ya kijani na nyekundu ni vyanzo bora vya antioxidant hii kali, kabichi nyekundu ina kiwango kikubwa zaidi.
Kikombe kimoja (89 g) cha kabichi nyekundu iliyokatwakatwa katika 56% ya ulaji uliopendekezwa wa vitamini C, ni kiasi sawa kinachopatikana katika chungwa ndogo.

Chanzo cha picha, Getty Images
4. Inasaidia kuboresha mmeng'enyo wa chakula
Ikiwa unataka kuboresha afya yako ya mmeng'enyo, kabichi yenye nyuzinyuzi ni chaguo sahihi.
Mboga hii imejaa nyuzi ambazo ni rafiki kwa afya ya utumbo,aina ya kabohaidreti ambayo haiwezi kusagwa ndani ya utumbo.
Nyuzi zisizoyeyushwa husaidia kuweka mfumo wa usagaji chakula kuwa na afya njema kwa kusaidia upataji wa haja kubwa kuwa rahisi na wa mara kwa mara.
Hii ni kwa sababu nyuzinyuzi ndicho chanzo kikuu cha mafuta kwa spishi rafiki kama Bifidobacteria na Lactobacilli .
Bakteria hawa hufanya kazi muhimu kama vile kulinda mfumo wa kinga na kutoa virutubisho muhimu kama vitamini K2 na B12.
Kula kabichi nyingi ni njia bora ya kuweka mfumo wako wa usagaji chakula kuwa na afya njema.
5. Huimarisha afya ya moyo
Kabichi nyekundu ina lishe inayojulikana kama anthocyanins kitaalamu. Imepewa rangi ya zambarau.
Tafiti nyingi zimegundua uhusiano kati ya kula vyakula vilivyo na rangi hii na kupunguza hatari ya kupata ugonjwa wa moyo.
Katika utafiti wa 2013 unaojumuisha wanawake 93,600, watafiti waligundua kuwa wale walio na ulaji mwingi wa vyakula jmii hii walikuwa na hatari ndogo ya kupata mshtuko wa moyo.
Uchambuzi mwingine wa tafiti 15 za uchunguzi ulikuwa na matokeo sawa, ikiripoti kwamba kuongezeka kwa ulaji wa flavonoids kulihusishwa na kupungua kwa hatari ya vifo vinavyohusishwa na ugonjwa wa moyo.
Kuongezeka kwa ulaji wa jamii hii pia kumeonyeshwa kupunguza shinikizo la damu na viwango vya lehemu ya LDL (mbaya).
Kabichi ina zaidi ya aina 36 tofauti za lishe zijulikanazo kama anthocyanins zenye nguvu, na kuifanya kuwa chaguo bora kwa afya ya moyo.
6. Inaweza kupunguza shinikizo la damu
Shinikizo la juu la damu huathiri zaidi ya watu bilioni moja duniani kote na ni sababu kuu ya ugonjwa wa moyo na kiharusi.
Madaktari mara nyingi huwashauri wagonjwa wenye shinikizo la damu kupunguza ulaji wao wa chumvi.
Walakini, ushahidi wa hivi karibuni unaonyesha kuwa kuongeza potasiamu yako ya lishe ni muhimu vile vile katika kupunguza shinikizo la damu.
Potasiamu ni madini muhimu.
Moja ya kazi zake kuu ni kusaidia kudhibiti shinikizo la damu kwa kukabiliana na athari za sodiamu mwilini.
Potasiamu husaidia kutoa madini ya sodiamu ya ziada kupitia mkojo.
Pia hupunguza kuta za mishipa ya damu, ambayo hupunguza shinikizo la damu.
Ingawa sodiamu na potasiamu ni muhimu kwa afya, lishe ya kisasa huwa na sodiamu nyingi na potasiamu chini sana.
Kabichi nyekundu ni chanzo kizuri cha potasiamu, ikitoa 9% ya DV katika vikombe 2 (178-g).
Kula kabichi iliyo na potasiamu zaidi ni njia nzuri ya kupunguza shinikizo la damu na inaweza kusaidia kuiweka katika kiwango kizuri cha afya.
7. Inaweza kusaidia kupunguza viwango vya lehemu
Cholesterol mafuta yanayopatikana katika kila seli katika mwili wako.
Watu wengine wanafikiri lehemu yote ni mbaya, lakini ni muhimu kwa utendaji mzuri wa mwili.
Michakato muhimu mwilini hutegemea lehemu, kama vile usagaji chakula vizuri,homoni na vitamini D.
Walakini, watu ambao wana lehemu kwa wingi pia huwa na hatari ya kuongezeka kwa ugonjwa wa moyo, haswa wanapokuwa na viwango vya juu vya LDL (mbaya).
Kabichi ina vitu viwili ambavyo vimeonyeshwa kupunguza viwango vya LDL (mbaya) lehemu.
Kabichi ina vitu vinavyoitwa phytosterols. Utafiti wa 2020 wa Taasisi ya Moyo ya nchini Marekani ilionyesha kuwa gramu 2-3 za mimea ya stanol esta kwa siku ilipunguza lehemu ya LDL kwa 9-12%.
8. Kabichi ni chanzo cha vitamini K
Vitamini K ni mkusanyiko wa vitamini ambayo ina majukumu mengi muhimu katika mwili.
Vitamini hii imegawanywa katika makundi mawili makuu:
- Vitamini K1 (phylloquinone): Hii hupatikana hasa katika vyanzo vya mimea.
- Vitamini K2 (menaquinone): Fomu hii hupatikana katika vyanzo vya wanyama na baadhi ya vyakula vilivyochachushwa. Pia huzalishwa na bakteria kwenye utumbo mpana.
Kabichi ni chanzo kizuri sana cha vitamini K1, ikitoa 56% ya DV katika kikombe kimoja cha ujazo wa (89 g).
Vitamini K1 ni kirutubisho muhimu ambacho kina majukumu mengi muhimu katika mwili.
Mojawapo ya kazi zake kuu ni kufanya kama kiambatanisho cha vimeng'enya vinavyohusika na kuganda kwa damu.
Bila vitamini K, damu ingepoteza uwezo wake wa kuganda vizuri, na hivyo kuongeza hatari ya kutokwa na damu nyingi.
9. Ni rahisi sana kuongeza kwenye lishe yako
Mbali na kuwa na afya njema, kabichi ni tamu.
Inaweza kuliwa mbichi au kupikwa na kuongezwa kwa aina mbalimbali za mapishi kama saladi, supu, kitoweo na kadhalika.
Mboga hii yenye matumizi mengi inaweza hata kuchachushwa.
Mbali na kubadilika kwa mapishi mengi, kabichi ni ya bei nafuu sana.
Haijalishi namna unavyotayarisha kabichi, kuongeza mboga hii kwenye sahani yako ni njia ya nzuri ya kufaidisha afya yako.
Kabichi ni chakula cha kipekee chenye afya.
Ina virutubishi na ina kiwango kikubwa cha vitamini C na K.
Kwa kuongeza, kula kabichi kunaweza hata kupunguza hatari ya magonjwa fulani, kuboresha mfumo wa mmeng'enyo wa chakula, na kupunguza kuvimba.
Kwa manufaa mengi sana ya kiafya, unaweza kuila kama mboga au kama sharubati.
Maudhui yote ya afya kwenye BBC yametolewa kwa maelezo ya jumla pekee, na hayapaswi kuchukuliwa kama mbadala wa ushauri wa matibabu wa daktari wako au mtaalamu mwingine yeyote wa afya. Ikiwa una wasiwasi wowote kuhusu afya yako kwa ujumla, unapaswa kuwasiliana na mtoa huduma wa afya wa eneo lako.















