Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Simba vs Stellenbosch: Falsafa, ndoto au historia itashinda leo pale Zanzibar?
- Author, Na Yusuph Mazimu
- Akiripoti kutoka, BBC Dar es Salaam
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Katika ardhi yenye ladha ya bahari na harufu ya historia, Zanzibar patakuwa na mchezo wa haja Jumapili hii: Simba SC ya Tanzania wakikabiliana na wageni waliokuja kushangaza, Stellenbosch FC ya Afrika Kusini, katika nusu fainali ya kwanza ya Kombe la Shirikisho la CAF.
Huu si mchezo wa kawaida. Ni hadithi ya kizazi kipya dhidi ya majina ya kale. Unaweza kusema ni mtindo wa maisha pengine uliozoeleka dhidi ya mtindo mpya wa maisha na roho ya mapinduzi.
Kwa Simba SC kuna imani kubwa sana kwao kwamba watafanya vyema na kufuzu hatua ya fainali. Ari ni kubwa na mashabiki wengi wanazungumzia uwezekano wa kubeba kombe mwaka huu.
Kwa Stellenbosch FC , mchezo huu ni sehemu ya burudani kwao na ushindani kwa safari yao. Na kwa ari yao ya kushangaza mpaka kuitwa 'watoto pendwa' hatua hii ya nusu fainali kwao hawana cha kupoteza, wanataka kuendelea kuja kuushangaza umma wa wapenda soka Afrika.
Kutoka divai mpaka dhahabu, safari ya Stellies ni ya kushangaza
Stellenbosch FC si klabu ya soka tu, ni simulizi la matumaini lililoanzia kwenye mji wa divai wa Cape Winelands. Ilianzishwa mwaka 2016, wakati Simba tayari walikuwa na kumbukumbu za kucheza fainali ya CAF mwaka 1993. Katika muda mfupi, Stellies wamejijengea jina kwa misingi ya nidhamu, uvumilivu na imani, chini ya kocha Steve Barker, ndugu wa marehemu Clive Barker, kocha aliyewahi kutwaa Kombe la Mataifa ya Afrika akiwa na Bafana Bafana.
Mafanikio yao si ya kawaida. Kuwatoa Zamalek, mabingwa watetezi wa CAF, kule Cairo, si ushindi wa bahati. Ni ushahidi wa mpango, moyo wa pamoja, na vipaji kama ya Sihle Nduli ambaye alitikisa Afrika kwa bao la dakika ya 79.
Ubora wao unaangaziwa pia na hata simba wenyewe kupitia kwa Meneja Habari na Mawasiliano, Ahmed Ally: "Wapinzani wetu Stellenbosch sio timu dhaifu, hadi inafika hatua hii inaonyesha ni timu ambayo imejiandaa. Wanasimba wote tulijiandaa kucheza na Zamalek lakini Stellenbosch akammaliza pale pale nyumbani kwake, hajamtoa Zamalek kwa bahati mbaya."
Simba SC wana ukongwe wenye njaa mpya
Kwa upande wa pili kuna Simba SC, klabu yenye misuli ya historia lakini ina moyo wa kisasa. Wanatoka kwenye ushindi wa kihistoria dhidi ya Al Masry, wakipindua meza kutoka 2-0 hadi kushinda kwa penalti 4-1, baada ya kupata matokeo ya 2-0 nyumbani jijini Dar es Salaam.
Wanakuja kwenye mchezo huu wa nusu fainali wakiwa na nyota kama Steven Mukwala, mshambuliaji hatari, na Elie Mpanzu, mchezaji mwenye mvuto na ubunifu wa aina yake.
Simba si wageni wa hatua hii, lakini wana kiu ya kutwaa taji la Afrika. Ni timu inayobeba shinikizo la historia, lakini pia silaha ya uzoefu wa miaka na miaka kwenye mashindano ya kimataifa.
"Simba wamecheza na timu kubwa zaidi ya Stellenbosch, Stellenbosch hawapo 'Level' (kiwango) ya Al Ahly, Zamalek, Wydad ata Kaizer Chiefs kwahiyo naamini Simba hawana hofu na Stellen bali wanawaheshimu tu" anasema George Ambangile, Mchambuzi wa soka Tanzania.
Utamaduni, hali ya hewa, na mapenzi yanavyonogesha mchezo huu
Hili ni pambano lenye tofauti nyingi na linahusisha wachezaji wa kutoka mazingira mawili tofauti. Stellenbosch ni mji wa wanafunzi, mvinyo, na rugby. Ni mahali ambapo mpira wa miguu bado unapigania nafasi yake mbele ya mchezo wa rugby. Ukiwa kwenye mji huo, habari ni kuhusu rugby, soka ni kwa kiwango kidogo. Kuna majina ya wakongwe wa rugby kama Jean de Villiers na Willie le Roux, ambayo yametawala mji huo. Lakini kwa msaada wa kocha Barker na uongozi imara, mpira wa miguu sasa unaanza kuwa sehemu ya kitambulisho cha mji huu.
Simba SC yenyewe inatoka Dar es Salaam, jiji lenye joto kali la bahari, lenye msisimko wa soka, vichaa wa soka na mashabiki wanaoimba na kushangilia kwa dakika 90. Hii si timu tu ni sehemu ya maisha ya Watanzania. Kwa Tanzania kama si Simba, basi utakuwa Yanga. Kwao, mpira ni mapenzi na lugha ya umoja.
Lakini kwa Stellenbosch, mpira ni mapinduzi ya kimya kimya yanayobadilisha jamii ya kitaaluma kuwa mji wa ndoto za soka.
Kwa sasa wana wachezaji 10 wa kimataifa katika kikosi chao wakiwemo 8 kutoka Afrika Kusini. Lakini walioitwa kwenye kikosi cha Bafanabafana cha Mwezi uliopita kucheza na Benin walikuwa walinzi wawili tu; Thabo Molloisane na Fawaaz Basadien beki wa kushoto aliyecheza dakika zote 90 katika mchezo huo.
Wanaye pia Andre De Jong mshambuliaji kutoka New Zeeland na mlinzi Kazie Godswill wa Nigeria, bila kumsahau mlinzi wa zamani wa kimataifa wa Kenya Brian Onyango.
"Simba wanao wachezaji wengi wa kimataifa kuliko hawa jamaa (Stellenbosch), wana uzoefu mkubwa wa soka la Afrika, wana ari, wana timu nzuri na wako nyumbani, wana faida, lakini sitashangaa wakishangazwa na hawa", anasema Rahman John, mfuatiliaji wa soka Tanzania.
Takwimu zinavyoleta mpambano wa akili ya Barker vs Davids
Mchezo huu si tu wa takwimu, lakini ni muhimu kutambua, timu zote zimecheza mechi 8. Stellenbosch hawajafungwa katika mechi zao tatu za mwisho, ukuta wao ni imara. Simba wamerudi kutoka kaburini na wana morali isiyoelezeka. CAF bado wanatumia sheria ya bao la ugenini, jambo linaloweza kuwa silaha kwa Stellies ikiwa watafanikiwa kupata bao huko Zanzibar.
Na kwa sababu hiyo, akili ya makocha wa timu hizi, zitaendelea kuwa za hali ya juu. Kwa Steve Barker wa Stellenbosch, kocha mpole lakini mwenye maono, anapambana na Fadlu Davids, Mzulu anayejua vyema soka ya Afrika.
Wote wawili walianza kazi za ukufunzi kwa nyakati zinazokaribiana, lakini sasa wanakutana katika soka la kimataifa. Mchezo huu ni mtihani kwa falsafa zao. Barker atajikita katika kuzuia na kushambulia kwa kushtukiza, silaha ambayo walitumia na kumtoa Zamalek. Davids yeye, anapenda mpira wa kasi, umiliki na mashambulizi ya kutokea pembeni.
Sihle Nduli, kiungo mwenye kasi, akili ya mpira na uamuzi wa dakika za mwisho, wa Stellenbosch anaweza kubadili mchezo kwa pasi moja tu. Kurudi mlinda mlango Sage Stephens kunawapa faida kubwa Stellenbosch, kwa sababu uzoefu wake utakuwa muhimu hasa kwa mechi hii ya ugenini.
Kwa upande wa Simba, Steven Mukwala anaweza kuvuruga safu yoyote ya ulinzi. Anahitaji nafasi moja tu kufunga huku Elie Mpanzu, mbunifu wa mashambulizi ya pembeni, mtu wa hatari katika nafasi ndogo. Haitaji sana nafasi za wazi kufunga. Goli lake dhidi ya AL Masry katika hatua ya robo fainali linaweza kudhihirisha hilo.
"Tunaiheshimu sana Simba. Wana uzoefu, wamefunzwa vyema, na wamezoea aina hizi za michezo. Lakini tumepata nafasi yetu katika nusu fainali. Tunajiamini na tutatoa kila kitu tulicho nacho," Barker alisema.
Kwa ujumla Jumapili hii sio tu mechi ya soka, itakuwa filamu ya maisha halisi , Stellenbosch wakifurahia marashi ya karafuu ya Zanzibar wakiwa na ari yao ya kusonga mbele, Simba wakiwa na ndoto yao ya kubeba ubingwa.
Ni vita ya roho ya vijana wa Stellenbosch dhidi ya fahari ya Simba wa Afrika. Ni mashindano ya falsafa, historia na ndoto. Na katika kila dakika ya mchezo huu, mshabiki wa kweli wa Afrika atajua: huu si mchezo wa kawaida. Hii ni historia ikijitengeneza. Simba akitaka kufuzu kwa historia, Stellenbosch wakitakamkuandika pia histria zaidi katika mashindano haya ya kwanzo kwao ya afrika.
Hapa kuna Simba, na pale kuna wale wanaokuja kuwashangaza Simba hao.Je, Stellies wataandika hadithi yao ya dhahabu au Simba watejenga himaya yao kifalme Afrika?