Kashfa ya dawa ya kikohozi Gambia: akina mama wadai haki
Omar Wally
Banjul, Gambia

Chanzo cha picha, OMAR WALLY
Pikipiki ndogo nyekundu iko kwenye kona ya nyumba ya Mariam Kuyateh ikikusanya vumbi.
Ilikusudiwa mtoto wake wa miezi 20, Musa, lakini alikufa mnamo Septemba.
Yeye ni mmoja wa watoto 70 nchini Gambia wanaoaminika kufariki baada ya kupewa dawa ya kikohozi ambayo "inawezekana inahusishwa na maradhi ya papo hapo la figo", kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni.
Hakuna mtu katika familia anayegusa pikipiki ndogo ya mtoto Musa - ukumbusho wa kile kilichopotea.
Mama yake mwenye umri wa miaka 30, ambaye ana watoto wengine wanne, alitokwa na machozi alipokumbuka kilichompata mwanawe.
Akiwa ameketi nyumbani kwake katika kitongoji cha jiji kubwa la Gambia, Serrekunda, alieleza kuwa ugonjwa wake ulianza na mafua.
Baada ya kuonwa na daktari, mume wake alinunua dawa ya kutibu tatizo hilo. "Tulipompa dawa, mafua yalikoma, lakini hilo lilisababisha tatizo lingine," anasema Bi Kuyateh. "Mwanangu hawezi kutoa haja ndogo." Alirudi hospitali na Musa alipelekwa kupimwa damu, ambayo ilithibitisha kuwa hakuna ugonjwa wa malaria.
Alipata matibabu mengine, ambayo hayakufanya kazi, basi catheter iliwekwa, lakini hakukojoa.
Hatimaye, mtoto mdogo alifanyiwa upasuaji. Hakukuwa na nafuu. "hivyo, alifariki."

Chanzo cha picha, KUYATEH FAMILY
Mapema wiki hii, WHO ilitoa tahadhari ya kimataifa kuhusu dawa nne za kikohozi zinazohusishwa na vifo nchini Gambia. Bidhaa hizo - Promethazine Oral Solution, Kofexmalin Baby Cough Syrup, Makoff Baby Cough Syrup na Magrip N Cold Syrup - zilitengenezwa na kampuni ya Kihindi, Maiden Pharmaceuticals, ambayo haikuwa imetoa hakikisho kuhusu usalama wake, ilisema WHO.
Serikali ya India inachunguza hali hiyo. Kampuni hiyo haikujibu ombi la BBC la kutoa maoni.
Kuna hasira nyingi nchini Gambia juu ya kile kilichotokea.
Kuna ongezeko la wito wa kujiuzulu kwa Waziri wa Afya, Dk Ahmadou Lamin Samateh, pamoja na kufunguliwa mashtaka kwa waagizaji wa dawa za kulevya nchini. "Sabini ni idadi kubwa. Kwa hivyo tunahitaji haki kwa sababu waathiriwa walikuwa watoto wasio na hatia," anasema Bi Kuyateh.

Chanzo cha picha, OMAR WALLY
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mtoto Aisha mwenye umri wa miezi mitano ni mwathirika mwingine.
Mama yake, Mariam Sisawo, alitambua asubuhi moja kwamba baada ya kunywa dawa ya kikohozi, mtoto wake alikuwa haendi haja ndogo tena.
Wakati wa kwenda hospitalini kwa mara ya kwanza , mama huyo mwenye umri wa miaka 28 aliambiwa kuwa kibofu cha binti yake hakikuwa na tatizo.
Ilibidi aende hospitali mara mbili mfululizo kabla ya Aisha kupelekwa hospitali katika mji mkuu, Banjul, kilomita 36 kutoka nyumbani kwao Brikama.
Lakini baada ya siku tano za matibabu, alikufa. "Binti yangu alipata kifo cha uchungu. Wakati mmoja madaktari walipotaka kumweka kwenye IV, hawakuweza kuona mishipa yake.
Mimi na wanawake wengine wawili katika wodi moja, sote tulipoteza watoto wetu. "Nina watoto wawili wa kiume na Aisha alikuwa binti pekee. Mume wangu alifurahi sana kumpata Aisha na bado hawezi kukubaliana na kifo chake."
Kwa sasa Gambia haina maabara yenye uwezo wa kupima iwapo dawa hizo ziko salama na hivyo zinatakiwa kutumwa nje ya nchi kwa ajili ya kuhakikiwa, Mkurugenzi wa Huduma za Afya wa Gambia, Mustapha Bittay, alikiambia kipindi cha Focus on Africa cha BBC.
Siku ya Ijumaa, Rais Adama Barrow alionesha kuwa nchi hiyo inapanga kufungua maabara kama hiyo. Katika hotuba yake kwa taifa kupitia televisheni, pia aliitaka Wizara ya Afya kupitia upya sheria na miongozo ya dawa zinazoagizwa kutoka nje.
Bi Sisawo anaamini kuwa serikali ilipaswa kuwa macho zaidi. “Ni fundisho kwa wazazi, lakini jukumu kubwa ni la Serikali, kabla ya dawa yoyote kuingia nchini ni lazima iangaliwe vizuri iwapo inafaa kwa matumizi ya binadamu au la,” alisema.

Chanzo cha picha, OMAR WALLY
Isatou Cham alikuwa amekasirika sana kuzungumzia kifo cha mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka miwili na miezi mitano, Muhammed.
Alitoka sebuleni mwa nyumba yao huko Serrekunda akilia pamoja na watoto wake wengine wawili.
Baba yake Muhammed, Alieu Kijera, alieleza kilichompata mtoto wake wa kiume.
Alisema alipelekwa hospitalini akiwa na homa na kushindwa kujisaidia haja ndogo. Lakini madaktari walikuwa wakimtibu Muhammed ugonjwa wa malaria na hali yake ilikuwa inazidi kuwa mbaya.
Madaktari kisha wakasema anapaswa kutibiwa katika nchi jirani ya Senegal, ambako huduma ya afya inachukuliwa kuwa bora zaidi, lakini ingawa kulikuwa na nafuu, bado hawakumuokoa.
Bw. Kijera ana hasira kwamba nchi yake haina mfumo mzuri wa afya na kwamba alilazimika kusafiri nje ya nchi. "Kama kungekuwa na vifaa na dawa nzuri, mwanangu na watoto wengine wengi wangeweza kuokolewa," alisema.














