Utafiti wabaini sababu za homa ya ini kwa watoto

ggg
Maelezo ya picha, Rebeka anasema kwamba mwanawe aliugua haraka sana.

Kwa miezi kadhaa, Homa ya Ini (hepatitis) nadra imekuwa ikiwakumba watoto ulimwenguni kote. 

Zaidi ya watoto 1,000, wengi wao wakiwa chini ya umri wa miaka 5, wanaaminika kuathirika katika zaidi ya nchi 35, huku baadhi ya visa vikiwa vikali kiasi cha kuhitaji upandikizaji wa ini. 

Sababu zake hazikujulikana, lakini sasa kundi la wanasayansi wa Uingereza wanadai kuwa wamegundua sababu inayowezekana.

Watafiti wanaamini kuwa nyuma ya mlipuko huo mpya kuna virusi viwili vya kawaida ambavyo vimerudi baada ya kumalizika kwa marufuku ya kutoka nje kufuatia mlipuko wa corona.

  • Adenovirus, ambayo kwa kawaida husababisha mafua na tumbo
  • Adeno-associated virus 2 (AAV2), ambayo kwa kawaida haisababishi ugonjwa na inahitaji "msaidizi" wa virusi vinavyoambukiza, kama vile adenovirus, ili kuzaliana.

Timu hizo mbili za watafiti, kutoka London na Glasgow, zinaamini kwamba watoto hao, waligundulika baadaye kuliko kawaida kuwa na virusi hivi kwa sababu ya vizuizi vya Covid, walipoteza kinga ya awali dhidi yao.

Hiyo inaeleza, kwa maoni yao, kwa nini wengine walipata matatizo ya ini yasiyo ya kawaida na yenye wasiwasi.

Kesi kadhaa

Noah, miaka 3, anaishi Chelmsford, Uingereza, na ni mmoja wa kesi hizo.

Mtoto huyo alihitaji kupandikizwa ini haraka baada ya kuugua sana homa ya ini.

Mama yake, Rebecca Cameron-McIntosh, anasema hali hiyo imekuwa ya kusikitisha.

"Hakuna kitu kibaya kilichowahi kutokea kwetu pamoja naye hapo awali. Na ilikuwa ni ghafla. Nadhani hiyo ndiyo ilitushangaza," anakumbuka.

"Tulichukulia kuwa ni tatizo dogo ambalo lingetatuliwa kwa urahisi, lakini kwa kweli liliendelea kusambaa," anaongeza.

ggg
Maelezo ya picha, Noah alihitaji kupandikizwa.

Rebecca awali alikuwa tayari kutoa sehemu ya ini lake kwa ajili ya kupandikizwa, lakini baada ya majibu ya dawa alizotumia, aliishia kuwa kwenye uangalizi maalum.

Noah aliwekwa kwenye orodha ya wanaopandikiza na mara baada ya kupokea kiungo kipya alipata nafuu lakini atahitaji kutumia dawa za kuzuia kinga maishani mwake ili kuzuia mwili wake kukataa ini mpya.

"Kuna jambo la kuhuzunisha sana katika hili, kwa sababu unafuata sheria, unafanya kile unachopaswa kufanya ili kulinda watu walio katika mazingira magumu, halafu kwa njia nyingine ya kutisha, mtoto wako anakuwa hatari zaidi kwa sababu ulifanya ulichofanya. ulipaswa kufanya,” anasema Rebecca.

Kesi za nadra

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kesi kama za Noah zimekuwa chache na watoto wengi wanaopata aina hii ya virusi hupona haraka.

Haijulikani kwa nini wengine hupatwa na kuvimba kwa ini lakini jenetiki inaweza kuwa na kazi ya kufanya.

Wanasayansi wamekataa uhusiano wowote na virusi vya corona au chanjo ya covid.

Mmoja wa watafiti wa utafiti huo, Profesa Judith Breuer, mtaalam wa virusi katika Chuo Kikuu cha London na Hospitali ya Great Ormond Street, anaamini kuwa kutengwa wakati wa janga hilo kulisababisha viwango vya maambukizi vya virusi vingine kucheleweshwa kwa watoto wengi.

"Wakati wa kipindi cha karantini, wakati watoto hawachanganyiki, hawakuambukizana virusi kutoka kwa mmoja hadi mwingine, hivyo hawakukuza kinga dhidi ya maambukizi ya kawaida ambayo wangekutana nayo kwa kawaida," anafafanua.

"Vizuizi vilipoondolewa, watoto walianza kuchanganyika, virusi vilianza kuzunguka kwa uhuru, na ghafla wakajikuta kwenye hii ya ukosefu wa kinga ya awali wa maambukizo mengi mapya," anaongeza.

hhh
Maelezo ya picha, Rebecca anaeleza kwamba mwanae atahitaji dawa maisha yake yote.

Wataalam wanatumai kuwa visa hivyo sasa vimepungua, lakini bado wako macho kwa maambukizo mapya.

Profesa Emma Thomson, ambaye aliyeongoza utafiti huo kutoka Chuo Kikuu cha Glasgow, anaeleza kuwa bado kuna maswali mengi ambayo hayajajibiwa.

"Tafiti kubwa zinahitajika kwa haraka kuchunguza jukumu la AAV2 katika homa ya ini kwa watoto," anasema.

"Pia tunahitaji kuelewa zaidi kuhusu mzunguko wa msimu wa AAV2, virusi ambavyo havifuatiliwi mara kwa mara, inaweza kuwa kwamba kuongezeka kwa maambukizi ya adenovirus kumeendana na ongezeko la uwepo wa AAV2 na kusababisha udhihirisho usio wa kawaida wa homa ya ini kwa watoto wanaoshambuliwa," anaongeza.