Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je, mtu mwingine anaweza kudhibiti akili yako?
- Author, Subhash Chandra Bose
- Nafasi, BBC
Filamu ya Stranger na 7th Sense, zinaeleza kuhusu hiponozi ama kiinimacho - kwamba mtu anaweza kumdhibiti mtu mwingine kupitia maono, kumfanya atulie na kuzielewa habari zake za akilini.
Siku ya hiponozi huadhimishwa tarehe 4 Januari kila mwaka na vikundi vya watu kutoka nchi tofauti. Siku hiyo hutumiwa kueneza uelewa kuhusu hiponozi na faida zake.
Katika filamu nyingi zinaonyesha kupitia kiinimacho mtu anaweza kumdhibiti mtu mwingine kiakili na kumfanya afanye chochote anachotaka. Lakini wataalamu wanasema hilo si la kweli, haliwezekani.
"Hiponozi sio kudhibiti ubongo wa mtu. Bali inahusu kuituliza akili ya mtu aliye katika hali ya hofu au wasiwasi na kuileta katika hali ya utulivu na kutatua tatizo lake,” anasema mtaalamu wa magonjwa ya akili Radhika Murugesan.
''Ninaweza tu kukuarifu kitu ikiwa ubongo wako utashirikiana na kile ninachosema. Na siwezi kuchukua udhibiti kamili wa ubongo wake. Siwezi kutoa maagizo ufanye hivi au ufanye vile.''
Imani Potofu
''Mitazamo mingi potofu kuhusu hiponozi huoneshwa katika filamu: "Watu wengi wamepotoshwa na ukweli ni kwamba hiponozi inatiwa chumvi katika filamu kinyume na ukweli.
‘’Watu wanaokuja kuzungumza nami huniuliza, unaweza kufuta kumbukumbu ya mpenzi wangu wa zamani? Je, unaweza kumlaghai binti yangu na kujua anampenda nani? Wanauliza mambo kama haya. Huku ni kutoelewa na kunasababishwa na filamu. Ukweli wa mambo ni kuwa hayo hayawezi kufanyika,” anasema Radhika Murugesan
Kwanini inatumika?
Watu hutumia kwa madhumuni mbalimbali ya afya. Mtaalamu wa magonjwa ya akili na hiponozi, Soshina Saravanan anasema anaitumia kuponya majeraha mbalimbali ya zamani.
"Jambo la kwanza ninalofanya watu wakija kwangu, ni kuwarudisha nyuma pale ambapo akili zao zilipata hofu na taratibu kuifanya akili ya ndani kuelewa uhalisia wa sasa,” anasema.
Radhika Murugesan anasema, inasaidia pia katika kupunguza msongo wa mawazo, maumivu, huzuni ama tabia yoyote mbaya.
Anasema watu wanaugua shida za kisaikolojia. Watu hawa watateseka zaidi kimwili kuliko kiakili. Kuna tiba ya hayo yote pia.
Mwanasaikolojia Mohan Balakrishnan anasema Yoga ni njia bora na mbadala ya matibabu ya hiponozi. Yoga inaweza kutatua matatizo ya wale wanaotumia tiba ya hiponozi.
Mtoto mtoro shule anaweza kubadilishwa. Pia watu waliozaliwa wakiwa hawana matatizo ya kiakili, lakini baadaye wakaathirika na matukio mbalimbali na kupata aina yoyote ya matatizo ya akili wanaweza kuponywa.
Kwanini haitumiki sana?
Hiponozi haitumiki katika hospitali nyingi za serikali nchini India. Hata hivyo, daktari aliyefunzwa vizuri anaruhusiwa kutumia hiponozi. Tulimuuliza Dkt. Poornasandrika, mkurugenzi wa Hospitali ya Wagonjwa wa Akili ya Serikali ya Kilpauk, sababu ya kutotumika ni nini?
"Hiponozi ni aina ya matibabu ya kizamani. Kwa sasa tumeanza kutumia aina tofauti za matibabu kama vile tiba ya dawa. Tunaweza kusema hiponozi haitumiki sana - kwa sababu inaonekana ufanisi wake ni mdogo,” anasema.
''Na inaweza kutumika kwa mambo machache tu, kama kiwewe cha utotoni na wasiwasi na haiwezi kupendekezwa kwa kitu kingine chochote. Magonjwa mengine kama kisukari na shinikizo la damu ni mambo ambayo yanaweza kudhibitiwa kwa kutumia dawa.
‘’Hiponozi inaweza tu kutumiwa kuingiza mawazo chanya katika akili, hivyo haiwezi kutibu tatizo mara moja au kwa muda mrefu. Inaweza kutumika kama mazoezi lakini haiwezi kuchukuliwa kama matibabu kamili,’’ anasema Dkt. Poornasandrika.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah