Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Sababu sita za kiafya za kupoteza hamu ya tendo la ndoa
Kupungua kwa hamu ya kufanya mapenzi, ni tatizo linaloathiri mwanaume mmoja kati ya watano na idadi kubwa ya wanawake katika hatua fulani ya maisha yao.
Kuna sababu kadhaa zinazochangia tatizo hilo, mfano msongo wa mawazo katika kipindi fulani - kama wakati wa ujauzito, kujifungua au kunyonyesha.
Daktari wa magonjwa ya akili katika Hospitali ya das Clínicas huko Recife, Brazil na katibu wa Chama cha Madawa ya Kujamiiana, Catarina de Moraes anaeleza:
"Wakati mwingine, ukosefu wa hamu ya tendo hudhaniwa ni kule kupata ugumu wa kusimamisha uume au kutoridhika - lakini maana yake hasa ni ule ukosefu wa hamu ya ngono."
Kwa mujibu wa mtaalamu wa homoni katika Hospitali ya Wanawake ya Mariska Ribeiro, Dtk. Diego Fonseca, ili uhesabiwe una tatizo la kukosa hamu na tendo la ndoa, hali hiyo inapaswa iendelee kwa kwa angalau miezi sita.
Sababu za kukosa hamu:
Mabadiliko katika maisha
Kupungua kwa hamu kunaweza kutokea kwa hali ambazo kila mtu humpata, kama vile mfadhaiko au uchovu.
Pia kubadilika kwa ratiba yako, pale unapokuwa na shughuli zingine katika wakati ambao ni muda wa kufanya mapenzi; kama vile kulea watoto.
Matatizo ya akili
Shida ya kiakili kama vile sonana, msongo wa mawazo na wasiwasi zinaweza kuathiri sana hamu ya ngono.
"Wagonjwa walio na msongo wa mawazo wanaweza kupata tatizo la kupungua kwa hamu kutokana na kuvurugika kwa mwenendo wa kemikali katika ubongo, pamoja na mabadiliko ya homoni.
Kwa upande mwingine, aina fulani za dawa zinazotumiwa kutibu sonona na msongo wa mawazo zina athari ya kupunguza hamu ya tendo.
Mtaalamu anaonya - wagonjwa hawapaswi kuacha matibabu ya sonona ikiwa wataona dalili za kupungua kwa hamu, kwani sonana isiotibiwa inaweza pia kuharibu hamu ya ngono.
Mabadiliko ya homoni
Ikiwa mgonjwa hana magonjwa ya akili au mabadiliko ambayo yanasababisha kushuka kwa hamu ya tendo, hatua inayofuata ni kuchunguza mabadiliko ya homoni.
Kwa wanawake ni homoni zinazoshughulika na afya ya tishu za uzazi na ute. Kwa wanaume ni kuchunguza homoni za uzalishaji wa manii, afya ya tishu za uzazi na hamu ya ngono.
Utambuzi katika kesi hizi unaweza kuwa changamoto, anasema Diego Fonseca.
"Kwa wanaume, kwa mfano, hatutathmini tu kama kiwango cha homoni za testosteroni kiko chini, lakini pia tunachunguza historia ya kimatibabu ili kuangalia kama hali nyingine zinaweza kuwa nyuma ya mabadiliko ya homoni."
Madaktari pia wanataja hali kama vile ujauzito, baada ya kuzaa, kunyonyesha na kunenepa kupita kiasi - pamoja na sababu nyingine ambazo pia hubadilisha viwango vya homoni kwa wanawake.
Magonjwa ya Kuambukiza
Sababu nyingine ni uwepo wa magonjwa ambayo - moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja - huathiri hamu ya tendo.
Ugonjwa wa tishu kukauka, ugonjwa wa kukakamaa, majeraha ya uti wa mgongo, ugonjwa wa neva zinazodhibiti mwitikio wa ngono, na kusababisha ugumu wa kudumisha kusimama, kufika kileleni, au kutopata msisimko wa ngono.
Vilevile ugonjwa wa kisukari, husababisha mabadiliko ya homoni , unaweza pia kusababisha kupungua kwa hamu. Kisukari pia husababisha uchovu na ugonjwa wa neva na kusababisha mishipa kuharibiwa.
Watu walio na matatizo ya moyo, wanaweza kupata uchovu sugu kutokana na kupungua kwa uwezo wa moyo wa kusukuma damu kwa ufanisi. Uchovu huu wa mara kwa mara unaweza kupunguza hamu ya ngono.
Zaidi ya hayo, baadhi ya dawa zinazotumiwa kutibu ugonjwa wa moyo zinaweza kuwa na madhara ambayo huathiri mfumo wa ngono.
Matibabu
Madaktari waliohojiwa wanasisitiza - hakuna suluhisho moja au la kimiujiza. Kwa kuwa kila kesi ni ya kipekee na matibabu inategemea mbinu binafsi, kwa kuzingatia sababu za msingi na mahitaji ya mtu binafsi.
"Ni muhimu kuwa na mazungumzo ya wazi na ya dhati kuhusu suala hili. Kuzungumza juu ya kupungua kwa hamu kunasaidia kuepuka kutokuelewana na kuruhusu washirika wote kuelewa hali na kutafuta ufumbuzi pamoja," anasema Diego Fonseca. .