Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mkutano mkuu: Nato inatarajia umoja kuhusu Ukraine huku Urusi ikifuatilia kwa karibu
Na Katya Adler, Mhariri Ulaya
Nato imebakiza masaa machache kabla ya kufanyika kwa mkutano wake mkubwa wa kilele wa kila mwaka, upande wa pili Rais wa Urusi Vladimir Putin akifuatilia kwa makini kutoka pembeni.
Huku Joe Biden, Emmanuel Macron, Rishi Sunak, Olaf Scholz na viongozi wengi zaidi wa dunia wakihudhuria, mabalozi wa nchi 31 wanachama wa muungano huo wamekusanyika pamoja, wakibishana kuhusu kile wanachoweza kufanya, wanachopaswa kufanya au kutangaza hadharani juu ya Ukraine.
Mwishoni mwa wiki hii hii ilitimia siku ya 500 tangu Urusi ilipoanzisha uvamizi wake kamili nchini Ukraine, kunyakua ardhi, kushambulia raia na kuwateka nyara watoto.
Kwa masikitiko ya Vladimir Putin, Ulaya na mshirika wake wa karibu Marekani wamekimbilia kutoa msaada kwa Ukraine (baadhi ya misaada hiyo ni ya haraka zaidi kuliko mengine, kiasi cha $165bn (£129bn) zilizotumiwa katika msaada wa kibinadamu, kifedha na kijeshi mpaka kufikia mwezi Mei mwaka huu, kulingana na Taasisi inayoheshimika ya Kiel ya Uchumi wa Kimataifa.
Imekuwa ni tendo nyeti, wakati fulani lisilopendeza, la kuweka sawa - kwa nchi moja moja za Ulaya, kwa Umoja wa Ulaya wenyewe kwa ujumla, na bila shaka zaidi ya yote kwa muungano wa kijeshi wa Nato, unaojumuisha adui wa zamani wa Urusi, Marekani.
Kwa mujibu wa Rais wa Marekani Joe Biden: "Sidhani kama kuna umoja katika Nato kuhusu kuileta au kutoileta Ukraine katika familia ya Nato sasa, wakati huu, katikati ya vita."
Alidokeza kuwa Ukraine kujiunga Nato kutamaanisha kwamba "ikiwa vita vinaendelea, basi sote tuko vitani. Tuko vitani na Urusi, ikiwa ndivyo ilivyokuwa."
Na siku 500 baada ya uvamizi wa Urusi, bado Nato haijaweza kuweka mambo sawa kwa urahisi.
Ukraine ni wazi inataka kiti chenye nguvu sawa katika meza ya Nato - na dhamana zote za usalama zinazoambatana na hilo.
Na inataka sasa - au, kwa sababu inatambua Nato haiwezi kukubali mwanachama mpya wakati taifa hili liko vitani, inataka angalau kuwe na "ishara ya wazi kwamba Ukraine itakuwa katika muungano", anasema Rais wa Ukraine mwenye ujuzi wa vyombo vya habari Volodymyr. Zelensky.
"Si kwamba mlango uko wazi kwa ajili yetu, ambapo hiyo haitoshi, lakini ni kwamba Ukraine itakuwa ndani yake," anasema.
Jambo lolote tofauti na hilo na ametishia hata kususia mkutano huo, na hata kuwaudhi wanachama wengi wa Nato, ikiwa ni pamoja na Ujerumani na Marekani.
Ikiwa Bw Zelensky hatashiriki, mtazamo wa umoja wa Magharibi na Ukraine - unaolenga kutoa ujumbe wazi kwa Moscow katika mkutano huo - utakuwa mbaya.
Tatizo kubwa ni kwamba Nato tayari iliiambia Ukraine kuwa ilikuwa katika muungano mwaka 2008, kabla ya uvamizi wa Urusi.
Matarajio ni makubwa kwamba Nato lazima sasa iipatie Kyiv kitu kingine cha umuhimu. Je ni kitu gani?
Wanadiplomasia wa ngazi ya juu kutoka mataifa kadhaa muhimu ya Nato walizungumza nami katika makala hii kwa sharti la kutotajwa majina, ili kuweza kutoa maoni yao kwa uhuru.
Wanasema wanachama wa Nato wameungana kuhusu Ukraine kuwa ndani ya "familia" yao. Lakini wanabaki kugawanyika uhusu maelezo.
Mkutano huo unafanyika Vilnius, mji mkuu wa Lithuania. Ni moja ya mataifa matatu madogo ya Baltic yaliyo upenuni mwa Urusi ambayo yalimezwa na kukaliwa na Umoja wa Kisovieti mwishoni mwa Vita vya pili vya dunia.
Watu wa Lithuania, Walatvia na Waestonia wanaumia kwa maumivu ya Ukraine. Wao, pamoja na taifa la Ulaya mashariki la Poland, ambalo pia linajiona kama mwathirika wa zamani wa uvamizi wa Urusi, wanadai Ukraine ipewe uanachama wa Nato haraka baada ya kusitishwa kwa mapigano na Moscow.
Lakini maamuzi ya Nato yanahitaji makubaliano ya pamoja kati ya nchi wanachama. Ujerumani, Marekani na Uingereza ni miongoni mwa mataifa yenye uangalifu zaidi.
Kwanza, kwa sababu ya masharti rasmi, muungano huo kwa kawaida ungetaka nchi iliyojiunga kutimiza masharti hayo kabla ya kuwa mwanachama.
"Kama vile Ukraine inastahili kuwa sehemu ya Nato, tuna wasiwasi sawa na vile tulivyokuwa mwaka wa 2008," mwanadiplomasia mmoja mashuhuri aliniambia.
"Tunahitaji kuona mageuzi, vita dhidi ya rushwa na udhibiti sahihi wa majeshi," alisema. Lakini aliongeza kuwa anafikiri mamlaka ya Ukraine imepata somo la wazi kwa kile kinachotokea katika jeshi la Urusi kuhusu ufisadi uliomeza mabilioni ya fedha na kuwaacha Warusi wakiwa wamedhoofika na kutokuwa tayari kwa vita.
Baadhi ya nchi za Nato pia zinasikitika kwamba ikiwa kuna ahadi ya kukubali Kyiv kuwa mwanachama mara tu baada ya kusitishwa kwa mapigano na Urusi, hilo linaweza kuifanya Moscow kurefusha mashambulizi yake kwa Ukraine kuendelea zaidi na zaidi.
Je Ukraine ina matarajio gani kutoka kwenye Mkutano huo?
Kwanza, subira ya kimkakati - kama Camille Grand, mmoja wa maafisa wa zamani wa Nato na sasa mtaalam wa ulinzi katika Baraza la Ulaya la Mahusiano ya Kigeni, anavyosema. Ahadi ya wazi kutoka nchi za Magharibi kwamba Ukraine ni sehemu ya muungano huo kwa muda mrefu.
Nilipigwa na butwaa wakati wa mazungumzo yangu na wanadiplomasia jinsi nchi zao zinavyoonekana kulegea kuhusu kasi ndogo ya mashambulizi ya Ukraine dhidi ya Urusi.
Walionekana wana fikra sawa na katibu wa mambo ya nje wa Uingereza, ambaye anadokeza kuwa "hii si sinema ya Hollywood".
"Moscow ilikuwa na muda mrefu sana wa kujiandaa kwa uvamizi huu," balozi mmoja aliniambia. "Na sasa tunatarajia Ukraine kuwa na mafanikio makubwa katika muda wa wiki tatu au nne? Hilo ni jambo lisilowezekana."
"Ukraine inajaribu kupiga hatua kwenye vita huku ikiheshimu maisha ya binadamu," alitoa maoni mwingine, akilinganisha hilo na kile alichokiita tabia ya Urusi ya kuwasukuma wanajeshi wake
"Tunawapa msaada muhimu wa kijeshi, unaozidi kuwa wa kisasa zaidi na wao - na Moscow pia - wanahitaji kujua kuwa itaendelea kuja."
Mojawapo ya mazungumzo muhimu katika mkutano wa kilele wa Vilnius yatazingatia sekta ya ulinzi ya Ulaya: Uwekezaji unaohitajika ili kuhakikisha ugavi wa silaha na misaada mingine ya kibinadamu unaweza kuendelea kutiririka kwenda Ukraine, huku bado ukiwaacha wanachama wa EU na Nato wakiwa na uwezo wa kutosha wa ulinzi na kujilinda wenyewe.
Kila nchi ya Nato kwa sasa hutuma msaada wake wa kijeshi kwa Ukraine, na kuacha Kyiv ikikabiliana na aina tofauti za magari ya kivita, mizinga, nk. Sio njia bora zaidi ya kusonga mbele.
Pili, kutokana na kukosekana kwa uwanachama wa haraka wa Nato kwa Ukraine, kundi la nchi (zilizo karibu lakini sio tu kwa Uingereza, Marekani, Ufaransa na Ujerumani) zinaunda "muungano wa walio tayari" kutoa dhamana ya usalama ya Kyiv. Tahadhari zaidi kama Marekani inavyorejelea hilo kama "hakikisho la usalama". Taarifa zaidi zinatarajiwa kujitokeza wakati wa mkutano huo.
Tatu, katika Siku ya Pili ya mkutano huo wa kilele, Nato itaitisha Baraza jipya la Nato-Ukraine - ambalo litafanya iwe vigumu sana ikiwa Rais Zelensky ataamua kutohudhuria! Wazo la baraza litakuwa kuboresha ushirika wa Kyiv na muungano, na kuipa ufikiaji mkubwa wa rasilimali za Nato.
Nne, Nato pia ina uwezekano wa kutupilia mbali Mpango wake wa Utekelezaji wa Uanachama unaohitajika wa kawaida kwa Ukraine, na kupunguza angalau baadhi ya michakato mirefu na ya awamu ya maandalizi ambayo nchi zingine zinazotaka uanachama kwa kawaida hupitia.
Hatimaye hakuna mtu katika Nato anayehoji haja ya kuunga mkono Ukraine katika kipindi cha muda mfupi, wa kati na mrefu.
Baadhi ya wanachama wa Nato - hasa Italia - wana wasiwasi ingawa maoni ya umma yanasalia kuunga mkono msaada wa gharama kwa Ukraine. Muungano pia unahitaji kufanya kazi (kwa bidii) juu ya msimamo wa pamoja juu ya Urusi wakati vita vitakapoisha.
Rasmi wanachama wa Nato wanasema itakuwa juu ya Kyiv kuamua ni lini masharti ya mazungumzo ya kusitisha mapigano na Moscow yanatimizwa.
Lakini nyuma ya pazia, wanadiplomasia wananiambia kunaweza kuja wakati ambapo nchi za Magharibi zinaweza kuinong'oneza Kyiv kwamba inapaswa kuchukua usitishaji wa mapigano unaofikiwa, badala ya kupoteza maisha zaidi ya Waukreni na kutumia mabilioni zaidi ya pesa za Magharibi kwenye vita ambayo haiwezi kushinda. .
Ingawa mazungumzo hayo, wanasisitiza, hakika si ya sasa.