Upi umuhimu wa bandari ya Dar es Salaam?
Na Rashid Abdallah
Mchambuzi ,Tanzania

Chanzo cha picha, Reuters
Mjadala juu ya bandari ya Dar es Salaam, Tanzania umekuwa mkubwa katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii; ni baada ya serikali ya Tanzania, kuonesha azma ya kutaka kuingia makubaliano ya kuipa kandarasi kampuni ya DP World kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu kusimamia bandari hiyo.
Kwa mujibu wa msemaji mkuu wa serikali ya Tanzania, Gerson Msingwa akizungumza na BBC, ameeleza makubaliano ya awali ya kushirikisha kati ya pande hizo mbili ndio yamesainiwa. Lakini bado hakujatiwa saini ya mwisho kuhusu vipengele vya namna gani makubaliano hayo yatafanyika.
Kwa kuzingatia ukubwa wa jambo lenyewe, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania litatakiwa kujadili jambo hilo, baada ya wananchi kutoa maoni yao. Changamoto inayojitokeza; ni kuibuka taarifa zenye mkanganyiko – za ukweli na uongo hasa katika mitandao.
Lakini kabla ya kulitazama jambo hilo kwa sura tofauti, kwanza tuitazame bandari yenyewe na vipi inainufaisha Tanzania:
Umuhimu wa bandari ya Dar
Bandari ya Dar es Salaam ndio kuu nchini Tanzania, haitoi huduma kwa Tanzania pekee. Nchi jirani zisizo na bahari zinatumia bandari hiyo vilevile; Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Burundi, Rwanda, Malawi, Uganda na Zimbabwe.
“Watumiaji wa bandari ya Dar es Salaam, wameongezeka sana, kwa sasa ndani ya mwaka mmoja tunahudumia magari kati ya 250,000 hadi 300,000 na asilimia 60 ya magari hayo, ni ya nchi jirani,” Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Mrisho S. Mrisho, Mei 2023 katika mkutano na waandishi wa habari.
Kwa mujibu wa tovuti ya bandari hiyo, asilimia 95 ya biashara za kimataifa za Tanzania, zinahudumiwa na bandari Dar es Salaam. Bandari hiyo inaunganisha Mashariki ya Kati, Mashariki ya Kati, Ulaya na Marekani.
Mwaka 2019/2020 makusanyo ya bandari ya Dar es Salaam, yalikuwa shilingi bilioni 901, mwaka 2020/2021 ilikusanya shilingi bilioni 896, na mwaka 2021/2022 katika robo ya kwanza ilikusanya shilingi bilioni 980 hadi mwisho wa mwaka.
Hadi hapo mambo yanaonekana kwenda vizuri. Ila upande mwingine wa shilingi, bandari hii ina changamoto zake vilevile - nyingine ni za muda mrefu. Raisi wa sasa na mwendazake Magufuli kwa nyakati tofauti wame yazungumzia matatizo ya bandari ya Dar.
Madudu ya Bandari
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Bandari ya Dar es Salaam ni moja ya eneo ambalo hayati Rais John Pombe Magufuli alifanya ziara ya kushtukiza baada tu ya kuingia Ikulu, katika kipindi chake cha kwanza cha miaka mitano - ziara za kushutukiza bandarini ziliendelea na kila wakati alikutana na matatizo.
Katika ziara ya Machi 2017 alishuhudia makontena 20 ya mchanga wenye madini uliozuiliwa kusafirishwa nje ya nchi tangu alipotoa agizo la kupiga marufuku usafirishaji wa mchanga nje ya nchi Machi 2, 2017.
“Siridhishwi kabisa na kasi za bandari, siasa zilizoko, longolongo zilizoko, mabandari yanaendeshwa kwa kasi kubwa duniani, na biashara zinakuwa kwa kasi kubwa kupitia bandari, sisi bado tunasuasua. Wawekezaji wanakuja, wanazungushwa mwanzo mwisho,” Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Julai 4, 2022.
Siku hiyo hiyo Rais Samia alitengua uteuzi wa mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya usimamizi wa bandari (TPA), Eric Hamis aliyedumu katika wadhifa huo kwa mwaka mmoja na miezi mitatu. Bwana Hamis alichukua nafasi ya Mhandisi Deusdedit Kakoko aliyetumbuliwa na Rais Samia, tarehe 28 Machi 2021.
Katika kipindi cha mwongo mmoja uliopita takribani wakurugenzi sita wa bandari ya Dar es Salaam, wameteuliwa na kutumbuliwa, kwa sababu mbali mbali - ukiwemo utendaji mbovu na ubadhirifu wa fedha.
Katika ripoti ya Takukuru iliyotolewa Machi mwaka huu, Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, Kamishna Salum Hamduni alisema kutosomana kwa mifumo ya mamlaka ya bandari (TPA) na mamlaka ya mapato (TRA), ni moja ya viashiria vya rushwa.
“Tatizo la mifumo katika bandari limekuwepo kwa siku nyingi. Bandari ni lango kubwa la uchumi lenye uwezo wa kuchangia hata nusu ya bajeti ya serikali, lakini inashangaza pato lake haliinuki,” alisema rais Samia katika hafla ya kupokea ripoti hiyo.
Bandari ya Dar Inaweza kubinafsishwa?
Lengo la serikali kuipa mwekezaji bandari ni ili kuongeza ufanisi na mapato, kwa mujibu wa Msigwa, ufanisi wa bandari hiyo kwa sasa ni mdogo. Ukiachilia maelezo ya serikali, kuna maswali mengi yanayoulizwa, moja wapo ni ikiwa kuna faida kwa Tanzania kuibinafsisha bandari yake kuu.
Ubinafishaji ni hatua ya mali kutoka kwenye mikono ya serikali na kwenda kwa mtu au kampuni binafsi inaweza kuwa ya ndani ama ya nje. Na mantiki yake ni kuisaidia serikali kukusanya pesa, kuongeza ufanisi wa shughuli zitokanazo na ubinafsishaji huo na hatimaye kukuza uchumi wa nchi kutokana na ongezeko la mapato.
Nimemuliza Mhadhiri na Mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, Tanzania, Beatrice Kimaro, ni mambo gani muhimu ya kuzingatia ikiwa serikali inataka kubinafsisha mali?
“Serikali inapotaka kubinafsisha chochote kwa mfano mjadala wa bandari Tanzania ni lazima izingatia masuala haya: Je, itasaidia kuongeza ufanisi? Itasaidia kuongeza mapato na kuchochea uchumi wa nchi? Ikiwa maslahi ya nchi husika na watu wake hayaonekani, hakuna mantiki ya kubinafsisha.”
“Mwaka 2016, Serikali ya Australia ilibinafsisha bandari ya Melbourne kwa mwekezaji kwa miaka 50 kwa thamani ya dola bilioni 9.7, leo ni moja ya bandari kubwa nchini humo kwa uingizaji na usafirishaji wa shehena za mizigo,” amefafanua Beatrice na kuongeza:
“La muhimu zaidi ni lazima kuwe na ushirikishwaji wa wazi kwa mchakato wa aina hii kwa sababu jambo kama bandari ni uti wa mgongo wa uchumi wa nchi. Kukishakuwa na muafaka wa pamoja, lazima hatua zote za kisera na kisheria ziongoze mchakato ili kuondoa manung’uniko mbeleni. Na hakuna haja ya kuharakisha zoezi la aina hii kwa sababu ya unyeti wake.”












