Senegal iko hatarini baada ya uchaguzi kucheleweshwa

dsc
Maelezo ya picha, Polisi wamewarushia vitoa machozi waandamanaji na kuwatia mbaroni waandamanaji mjini Dakar
    • Author, Yusuf Akinpelu
    • Nafasi, BBC

Sifa ya Senegal kama ngome ya demokrasia katika eneo lisilo na utulivu iko kwenye hatari - wakati waandamanaji wakipambana na polisi nje ya Bunge la Kitaifa.

Wabunge wamepitisha mswada tata wa kuongeza muda wa rais na kuchelewesha uchaguzi kwa miezi sita baada ya Rais Macky Sall kusitisha uchaguzi uliopangwa kufanywa wiki tatu zijazo.

Khalifa Sall, mpinzani mkuu na meya wa zamani wa Dakar, alitaja kucheleweshwa huko kuwa ni "mapinduzi ya kikatiba" na kuwataka watu kuandamana. Muungano wake wa kisiasa umeapa kwenda mahakamani.

Thierno Alassane Sall, mgombea mwingine, aliita hatua hiyo kuwa ni "uhaini mkubwa" na kuwataka wafuasi wake kukusanyika mbele ya Bunge la Kitaifa kuandamana na "kuwakumbusha wabunge kusimama upande sahihi wa historia".

Pendekezo hilo lilihitaji kuungwa mkono na thuluthi tatu ya wabunge 165 ili kupitishwa. Muungano unaotawala wa Benno Bokk Yakaar wa Rais Sall una wabunge wengi bungeni.

Sall alisema hana mpango wa kuwania wadhifa huo tena. Lakini wakosoaji wake wanamtuhumu kwa kujaribu kung'ang'ania madaraka au kuwa na kutaka ushawishi usio wa haki kwa mtu atakae mrithi.

Mara tu alipotangaza kuahirishwa uchaguzi - ndipo waandamanaji walipoandamana katika mji mkuu, Dakar.

Senegal kwa muda mrefu imekuwa mojawapo ya nchi zenye demokrasia imara Afrika Magharibi. Ni nchi pekee Afrika Magharibi ambayo haijawahi kuwa na mapinduzi ya kijeshi. Imekuwa na makabidhiano matatu ya madaraka kwa amani na haijawahi kuchelewesha uchaguzi wa rais.

Demokrasia Hatarini

cx
Maelezo ya picha, Wasiwasi unaongezeka nchini Senegal kwamba ikiwa uchaguzi hautafanyika machafuko yataenea
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mnamo 2017, wanajeshi wa Senegal waliongoza ujumbe wa Afrika Magharibi uliotumwa katika nchi jirani ya Gambia kumtimua mtawala wa muda mrefu Yahya Jammeh baada ya kukataa kukubali ameshindwa katika uchaguzi.

Katika eneo ambalo limekumbwa na mapinduzi, Rais Sall amekuwa mhusika mkuu wa Ecowas kuwalazimisha viongozi wa kijeshi kufanya uchaguzi na kukabidhi madaraka kwa raia.

Lakini demokrasia ya Senegal iko kwenye mgogoro wa kikatiba. Nchi inakabiliwa na mtihani mkubwa - katika uchaguzi na uhuru wa mahakama, wachambuzi wanasema.

Mvutano umekuwa ukiongezeka kwa zaidi ya miaka miwili kufuatia kile ambacho upinzani unasema ni jaribio la makusudi la kuwaondoa kwenye uchaguzi kwa kuwataka wagombea na mashitaka ya uhalifu ambao hawajafanya. Chama kimoja kikuu cha upinzani kimepigwa marufuku.

Mamlaka imekanusha kutumia mfumo wa sheria kwa manufaa ya kisiasa na Rais Sall anasema alikuwa akijaribu kutuliza hali ya mambo kwa kuchelewesha uchaguzi lakini hilo halionekani kufanya kazi hadi sasa.

"Uamuzi huo umeiweka Senegal katika mgogoro wa kikatiba. Katiba inataka uchaguzi kuandaliwa ndani ya siku 30 kabla ya kumalizika kwa mamlaka ya rais aliyeko madarakani. Utawala wa Sall unakamilika tarehe 2 Aprili," anasema Mucahid Durmaz, mchambuzi wa siasa za Afrika Magharibi.

"Na tangazo la kalenda ya uchaguzi lazima litolewe siku 80 kabla ya kupiga kura. Hata kama atamteua rais wa mpito baada ya Aprili 2, uhalali wake utapingwa."

cx
Maelezo ya picha, Mzozo ulizuka na polisi waliwazuilia wafuasi wa wagombea wa upinzani

Mamlaka ilizuia huduma za simu siku ya Jumatatu ili kuzuia kile ilichokiita "ujumbe wa chuki na upotoshaji" kuenea mtandaoni na kuleta taharuki kwa umma - kwa maneno mengine kufanya iwe vigumu kwa waandamanaji kupanga maandamano.

Baadhi ya wakazi wameiambia BBC wamekuwa wakitumia Wi-Fi na programu za VPN, kukwepa zuioa hilo lakini si kila mtu anaweza kufanya hivyo.

Upinzani umelaani kuzimwa kwa kituo binafsi cha televisheni cha Walf TV kwa tuhuma za "uchochezi'' kwa utangazaji wake wa maandamano.

Wanasiasa wawili wa upinzani, akiwemo Waziri Mkuu wa zamani Aminata Touré, aliyekuwa mshirika wa karibu wa Rais Sall lakini sasa ni mmoja wa wakosoaji wake wakali, wote walizuiliwa kwa muda mfupi kufuatia maandamano hayo.

Wakosoaji wanahofia hali hii inaweza kuitumbukiza nchi katika machafuko ya kisiasa ambayo yanaweza kuwa hatari kwa eneo zima la Afrika Magharibi.

Imani juu ya Demokrasia

cx
Maelezo ya picha, Senegal imeonekana kwa muda mrefu kama mojawapo ya nchi zenye demokrasia imara Afrika Magharibi

Imani juu ya demokrasia nchini Senegal imepungua sana chini ya Sall. Mwaka 2013, utafiti wa Afrobarometer, uligundua baada ya Sall kuchukua madaraka, zaidi ya theluthi mbili ya watu wa Senegal walikuwa na imani sana na demokrasia. Lakini kufikia 2022 idadi ilikuwa chini ya nusu.

Hata hivyo, Durmaz anasema haoni uwezekano wa mapinduzi ya kijeshi kwa sababu Senegal ina "vyama mbalimbali vya kisiasa, jumuiya za kiraia zenye nguvu na viongozi wa dini wenye ushawishi - huingilia kati ili kupatanisha mizozo ya kisiasa kati ya wanasiasa."

Wagombea 20 waliingia kwenye orodha ya mwisho ya kuwania urais, lakini wengine kadhaa walienguliwa na Baraza la Katiba, chombo cha ambacho huamua kama wagombea wametimiza masharti yanayotakiwa ili kugombea.

Waliopigwa Marufuku

dscx
Maelezo ya picha, Jumuiya za kikanda za Ecowas na Umoja wa Afrika zimetoa wito wa mazungumzo huku EU ikitaka uchaguzi huo ufanyike haraka iwezekanavyo.

Maarufu miongoni mwao ni kiongozi wa upinzani Ousmane Sonko alizuiliwa kwa sababu ya hatia ya kashfa, na Karim Wade, mtoto wa rais wa zamani, ambaye alishutumiwa kuwa na uraia wa Ufaransa. Wote wawili wanasema kesi dhidi yao zimechochewa kisiasa.

Sonko ameonyesha ana uwezo wa kuwakusanya wafuasi wake barabarani huku akiwa amezuiliwa, kwa hivyo huenda mvutano ukaendelea kuwa mkubwa.

Hii si mara ya kwanza kwa wagombea wakuu wa upinzani kuzuiwa kushiriki katika uchaguzi wa urais. Karim Wade na Khalifa Sall walifungwa jela kwa ufisadi 2015 na 2018, na kuzuiwa kushiriki katika uchaguzi wa 2019.

Madai ya ufisadi yanayohusisha Baraza la Katiba, yaliyoletwa na chama cha Karim Wade, yalisababisha uchunguzi wa bunge.

Rais Sall alihalalisha kucheleweshwa uchaguzi huo kwa kusema muda unahitajika ili kutatua mgogoro uliojitokeza kati ya Baraza hilo na baadhi ya wabunge.

cx
Maelezo ya picha, Abiria walilazimika kuteremka kwenye basi huku polisi waliokuwa na silaha wakiwavamia waandamanaji.

Licha ya hasira iliyoenea juu ya ucheleweshaji huo, chama cha Wade, Senegalese Democratic Party (PDS) kimeunga mkono hatua hiyo.

Lakini Wole Ojewale, mratibu wa kanda ya Afrika ya Kati katika Taasisi ya Mafunzo ya Usalama, anasema ucheleweshaji huo haukuwa halali.

"Rais si msimamizi wa mchakato wa uchaguzi, wakati tume ya uchaguzi haijasema kuwa ina mashaka kuhusu uwezo wao wa kufanya uchaguzi. Sidhani kama kuna jambo lolote linafaa kuvuruga mchakato wa kisiasa."

Wakosoaji wa Sall wanadokeza kuwa huenda alihofia mrithi wake aliyechaguliwa, Waziri Mkuu, Amadou Ba, alikuwa katika hatari ya kushindwa katika uchaguzi huo.

"Chama chake [cha Rais Sall] kinapoteza ushawishi. Kuna dalili kwamba huenda wanataka kujipanga au kubadilisha mgombea," Ojewale anasema.

Imetafsiriwa na Rashid Abdalla