Mwanaume mwenye mpango wa kupanda miti milioni 5 nchini Senegal 

ik

Chanzo cha picha, JO HOLLIS/BBC

    • Author, Jo Hollis
    • Nafasi, BBC News

Mwanamume mmoja kusini mwa Senegal amejiwekea kazi kubwa ya kupanda miti milioni tano katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Mradi huu ulimjia Adama Diémé aliporudi nyumbani eneo la Casamance mnamo 2020 baada ya miaka michache ya kufanya kazi huko Ulaya.

Mwanamume huyo mwenye umri wa miaka 48 alishangaa kwamba vijiji ambavyo vilikuwa na mamia ya miti mikubwa katika ujana wake, ni michache tu ilikuwa imebaki.

Katika baadhi ya vijiji, huwezi kupata hata mti mmoja. Wanaukata lakini hawafikirii kuupanda tena," aliambia BBC.

Kotekote barani Afrika kuenea kwa jangwa ni mojawapo ya sababu zinazolaumiwa kwa ukataji miti lakini katika eneo hili, kando ya eneo kubwa la Mto Casamance, miti hiyo ina uwezekano mkubwa wa kukatwa kwa madhumuni ya ujenzi kama vile kujenga nyumba, au kuchoma mkaa.

Bw Diémé, ambaye sasa anafanya kazi kama meneja wa mradi wa shirika lisilo la kiserikali la Uhispania huko Casamance na pia anayejitolea kama mkufunzi wa kilimo, ameazimia kubadilisha hayo yote.

Akiwa hana akiba kubwa ya mali, alianza kuchangisha pesa ili kutimiza ndoto yake - na ametumia dola 5,000 (£4,100) kutoka mfukoni mwake kuanzisha mpango huo.

th

Chanzo cha picha, JO HOLLIS/BBC

Kushirikisha wanawake 

Amekuwa akifanya kazi kwa bidii ili kushirikiana na jamii zote na kufikia wanawake, ambao alijua wangeweza kukabiliana na changamoto ya kuandaa upandaji kwa wingi wa miche.

"Unaenda katika kijiji na hakuna wanawake, ni janga," Bw Diémé alisema.

"Lakini ukienda kwenye kijiji chenye wanawake pekee, ni paradiso - wanafanya kazi kwa bidii na wanafanya kazi siku nzima kila siku.

"Ikiwa unataka kuongoza mradi mzuri anza na wanawake," Bw Diémé aliongeza.

Alichokifanya ni kuunganisha mradi wake wa kupanda miti kwa kuwasaidia wanawake kupata ujuzi wa kuwa wakulima wadogo na kuuza mazao yao katika masoko ya ndani.

"Mwanzoni, hatukujua jinsi ya kupanda mbegu na nini cha kufanya ili kukuza mazao," mmoja wa wanawake, Safi Yetou, alisema.

"Sasa tuna kila aina ya matunda ya kuuza sokoni na hatumtegemei mtu yeyote. Sote tuna akaunti katika benki sasa na hakuna mtu anayeweza kuniambia ninachoweza au nisichoweza kufanya. Ni vizuri."

w

Chanzo cha picha, JO HOLLIS/BBC

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mradi wa Bw Diémé unajulikana kama Ununukolaal, jina ambalo katika lugha ya kienyeji Jola linamaanisha "Miti Yetu".

Hadi aina 12 ya miti inapandwa, kutoka kwa mitende hadi kapok na miti ya limao - aina ya miti hutegemea mahitaji ya jamii na ardhi.

Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita zaidi ya miche 142,000 imetunzwa na kuota mizizi.

Inamaanisha kuwa kiasi kikubwa cha upanzi bado kinahitaji kufanywa ikiwa Bw Diémé atafikia lengo lake ndani ya miaka mitano ijayo - lakini yeye na mshirika wake Yolanda Pereñiguez hawakati tamaa.

Bi Pereñiguez anafanya kazi kama fundi cherehani na amekuwa muhimu katika kusaidia kupanga fedha kwa kubuni fulana ambayo inauzwa nje ya nchi kwa dola 15.

Pamoja na mwenzake Raymonde Coly, wanafanya kazi katika karakana ndogo yenye cherehani mbili ili kuzitengeneza kutoka kwa nguo za kienyeji, zenye picha ya kipekee ya mbuyu. Kila moja inayouzwa inaweza kulipia miche 15 ya miti.

"Nilichagua mbuyu kwani ni alama ya mti wa Kiafrika," alisema Bi Periniguiz. "Inapendeza kujua kwamba fulana hizi zinakwenda duniani kote, Ulaya na hata Canada kusaidia mradi wa miti."

Mbuyu kuokoa nyumba

Tulipoingia zaidi katika Casamance kwa mtumbwi, wenyewe uliojengwa kutoka kwa kipande kimoja cha mbao kilichochongwa kutoka kwenye mizizi ya mti wa kapok, thamani ya kweli ya mradi ilionekana.

Katika kisiwa kidogo cha kijiji katikati ya mto, maji yalipenya hadi kwenye majengo ya nje - na wakati mwingine hata chini ya vingine vilivyosimama kwenye nguzo.

w

Chanzo cha picha, JO HOLLIS/BBC

Miaka kumi iliyopita, viwango vya maji vilimaanisha kwamba ukingo wa maji ulikuwa mbali zaidi na haungeweza hata kufika kijijini, isipokuwa katika kilele cha msimu wa mvua.

Sasa ni hali ya kukata tamaa na ikiwa itazidi kuwa mbaya inaweza kumaanisha kuwaacha wakaazi bila makazi.

"Tumeishi katika kisiwa hiki kwa mamia ya miaka - lakini kama maji yanakuja zaidi tutalazimika kuondoka na kutawanyika kila mahali," Conakry Bassene, mmoja wa viongozi wa kijiji.

Miti ya Mbuyu, ambayo inaweza kuishi ardhini na kwenye maji yenye chumvi au maji safi, sasa imepandwa kando ya ufuo kama kizuizi. Miche hupiga upepo, kwa ahadi ya matunda siku moja na hata kivuli.

"Miti inaweza kutuokoa," alisema Bw Bassene.

"Miti, ndio tumaini letu la maisha."