Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je, dini zitatoweka siku za usoni ?
Idadi ya watu wanaoamini kwamba hakuna Mungu, hakuna maisha baada ya kifo na hakuna kuzaliwa upya baada ya kufa inaongezeka kwa kasi ulimwenguni. Kukana uwepo wa Mungu kuko waziwazi katika baadhi ya nchi, ni jambo ambalo halikuwa maarufu hapo awali.
“Kuna watu wengi wasioamini Mungu zama hizi, kuliko wakati mwingine wowote,” anasema Phil Zuckerman, profesa wa sosholojia katika Chuo cha Pitzer, Claremont, California, na mwandishi wa kitabu cha Living the Secular Life.
Kulingana na utafiti katika nchi 57 uliofanywa na Gallup International, idadi ya waumini wa dini imepungua kutoka asilimia 77 hadi asilimia 68 kuanzia mwaka wa 2005 hadi 2011. Huku idadi ya watu wanaodai hawaamini Mungu imeongezeka kwa asilimia tatu. Inakadiriwa wasioamini kuwako kwa Mungu ulimwenguni ni asilimia 13.
Ni kazi ngumu kutabiri kuhusu siku zijazo, lakini kwa kuzingatia kile tunachokijua juu ya dini; jinsi ilivyokua, kwa nini watu wengine walianza kuiamini na kwa nini wengine waliiacha, tunaweza kutoa vidokezo juu ya nini kitatokea miongo ijayo. Upi utakuwa uhusiano wetu na Mungu kwa karne zijazo?
Moja ya sababu za watu kufuata dini ni kuwad ini hutoa usalama katika ulimwengu usio na uhakika. Kwa hivyo haishangazi kuona nchi zinazowapa raia wake usalama mkubwa wa kiuchumi, kisiasa wana idadi kubwa ya wasioamini Mungu.
Mgogoro wa imani
Japani, Uingereza, Korea Kusini, Uholanzi, Jamhuri ya Cheki, Estonia, Ujerumani, Ufaransa, na Uruguai ni nchi ambazo dini ilikuwa muhimu karne moja iliyopita, lakini sasa imepungua sana.
Nchi hizi zina mifumo mizuri ya elimu na usalama wa kijamii, kuna usalama wa kutosha na nchi hizi zote ni tajiri, anasema Quentin Atkinson, mwanasaikolojia katika Chuo Kikuu cha Auckland huko New Zealand.
Vilevile, imani ya dini inaonekana kupungua katika nchi nyingi ambazo zilishika dini, ikiwa ni pamoja na nchi kama Brazili, Jamaica na Ireland.
Marekani ni nchi moja kati ya nchi tajiri yenye kiwango cha juu sana cha dini. Utafiti wa hivi karibuni wa wa Pew, uligundua idadi ya Wamarekani wanaodai hawaamini Mungu imeongezeka tu kutoka asilimia 1.6 hadi asilimia 2.4 kati ya 2007 na 2012.
Ara Norenzyan, mwanasaikolojia wa kijamii katika Chuo Kikuu cha British Columbia huko Vancouver, Canada na mwandishi wa kitabu cha 'Big God', anasema kupungua kwa idadi ya waumini haimaanishi kutoweka kwa dini. Kila kitu kinaweza kubadilika muda wowote.
Hata ikiwa matatizo yote ya ulimwengu yangetatuliwa kimuujiza na sote tukaishi maisha ya amani, bado dini zingekuwepo. Hiyo ni kwa sababu inaonekana kuna uhusiano wa Mungu na spishi zetu.
Moja ya mfumo wetu wa kufikiri, ni ule unaoturuhusu kuzungumza lugha ya awali, na huwapa watoto uwezo wa kutambua wazazi na kutofautisha kati ya vitu vilivyo hai na visivyo hai. Pia mfumo huo unatutia moyo kuelewa ulimwengu wetu.
Wasomi wanaamini mfumo huu huiwezesha dini kujiendeleza yenyewe, pamoja na kusaidia kushinda hatari. Vilevile, unatuongoza kuhisi kuwepo kwa vitu visivyoonekana.
Tabia ambazo haziwezi kuzuilika
Wasioamini Mungu wanapaswa kupigana dhidi ya imani za kitamaduni na za kimageuzi. Wanadamu hupenda kuamini kwamba wao ni sehemu ya uumbaji na maisha yana maana, na akili zetu hutafuta uazi.
Watu wengi wasioamini Mungu hutafuta usaidizi wa sayansi ili kuelewa ulimwengu na asili, lakini sayansi si nyepesi wakati wote.
Robert McCauley, mkurugenzi wa Kituo cha Akili, Ubongo na Utamaduni katika Chuo Kikuu cha Emory huko Atlanta, Georgia, anasema, mfumo wa sayansi unahusu utoaji sahihi wa taarifa. Huenda tusihisi, lakini ni lazima tukubali dunia inazunguka na maisha hayana lengo. Lakini hisia yetu inaweza kufikiria vinginevyo. Kwa hivyo tunaamini kwamba ukweli unabadilika kila wakati.’
Ailimia 20 ya Waamerika hawaendi kanisani, lakini asilimia 68 wanasema bado wanaamini Mungu na asilimia 37 wanajiona ni watu wa kiroho. Wanaamini kuna nguvu fulani ya kimungu huongoza ulimwengu.
Vivyo hivyo, watu wengi wanaodai kutomwamini Mungu bado wanaamini kuhusu mizimu, unajimu, karma au kuzaliwa upya katika mwili mwingine baada ya kufa.
"Watu wengi katika nchi za Skandinavia wanasema hawamwamini Mungu, lakini imani za kishirikina zinaaminiwa kuliko tunavyofikiri," anasema Norenzyn.
Mbali na hayo, wasioamini Mungu hutegemea vitu kwa ajili ya kuwaongoza kimaadili katika maisha yao. Hii inathibitishwa na kuongezeka kwa wafuasi wa uchawi huko Marekani, na Upagani unaonekana kuwa dini inayokua kwa kasi zaidi nchini Uingereza.
Mbali na hilo, dini huhimiza umoja na ushirikiano. Hofu ya Mungu huenda ilisaidia kudumisha utulivu katika jamii za kale.
Atkinson anasema, "dhana juu ya adhabu - ikiwa kila mtu anaamini adhabu ni ya kweli, inaweza kutokea kwa jamii nzima. Katika hali kama hiyo kudumisha dini na kanuni kali za maadili linaweza kuwa ni jukumu muhimu sana.’
Joseph Bulbulia wa Chuo Kikuu cha Victoria cha Wellington huko New Zealand na wenzake waligundua katika utafiti wa makumi ya nchi, kuwa watu katika nchi masikini zenye hali mbaya, wana imani zaidi juu ya Mungu.
Vilevile, kuna hesabu rahisi nyuma ya kuenea kwa dini. Ulimwenguni kote, watu walio na dini wana watoto wengi zaidi kuliko watu wasio na dini, kuna ushahidi wa hilo," anasema Norenzyan.
Pia ni ukweli kwamba watoto huwafuata wazazi wao linapokuja suala la kuamua kuwa wafuasi wa dini au la. Katika mazingira hayo ulimwengu usio na dini kabisa linaonekana ni jambo lisilo wezekanaa.
Kwa sababu za kisaikolojia, neva, kihistoria, kitamaduni - wataalam wanaamini dini haitakufa kamwe. Iwe dini inafuatwa kwa sababu ya upendo au hofu, imefanikiwa sana kudumisha uwepo kwake.
Zuckerman anasema, “Licha ya maumivu na mateso, mwanadamu anahitaji kupumzika, na watu wengi lazima wafikiri kuna kitu zaidi ya maisha, kiumbe kisichoonekana ambacho kinawapenda. Sitashangaa ikiwa wanao amini ni wengi zaidi ya wasio amini.”