Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Euro 2024: Je, Ronaldo ni mchezaji wa kipekee Ureno au ni mzigo?
- Author, Marcus Alves
- Nafasi, BBC
Ingawa alitarajiwa kustaafu soka ya kimataifa baada ya Kombe la Dunia lililopita, gwiji wa Ureno, Christianto Ronaldo bado ana ushawishi mkubwa na atacheza kuwania ubingwa wa Ulaya kwa mara ya sita msimu huu nchini Ujerumani.
"Nilikutana na Ronaldo nilipokuwa nikifundisha Everton mwaka 2013," meneja wa Ureno, Roberto Martinez anasema.
"Inavutia kwa umri wake ila bado ana tabia na hamu ya kijana wa miaka 18. Ana mawazo na hana mipaka. Amekuwa na timu ya taifa kwa miaka 20 sasa.”
Licha ya kuwa na umri wa miaka 39, Ronaldo ameonyesha hana mpango wa kuondoka katika soka la kimataifa.
Nyota huyo wa zamani wa Manchester United amemwambia Martinez lengo lake ni kufikisha mechi 250 akichezea Ureno. Kwa sasa ana mechi 207.
Ili kufanikisha hilo, atalazimika kukabiliana na ukosoaji unaoongezeka kutoka kwa mashabiki wa nyumbani ambao wanaamini Ureno inafanya vizuri zaidi bila yeye.
Mjadala Kuhusu Ronaldo
Mchambuzi wa soka kutoka Ureno, Sofia Oliveira, anasema, "inaonekana wazi uwepo wake kwenye timu unawaweka wachezaji wengine katika wakati mgumu."
"Angalia matendo yao utaona wakati mwingine wanamtafuta Ronaldo katika mazingira ambayo hayana faida kwa timu. Pia, kuna suala kwamba hataki kutumia muda mwingi bila mpira, kwa hivyo anaufuta maeneo wanayocheza wachezaji wengine, tabia hiyo inaathiri nafasi za wachezaji wengi," anasema Oliveira.
Amemaliza kampeni ya kufuzu Ureno kama mfungaji bora nyuma ya Romelu Lukaku wa Ubelgiji akiwa amefunga mabao 10.
Ni mchezaji wa tatu aliyetumiwa zaidi nchini humo kwa dakika 725, nyuma ya Ruben Dias na Bruno Fernandes, hayo yametosha kwa Ronaldo kuzima mjadala dhidi yake.
Ingawa hayo hayasaidii kwani mchezo pekee aliokosa wakati wa kufuzu Euro – ulikuwa wa ushindi wa 9-0 dhidi ya Luxembourg – ushindi mkubwa zaidi wa enzi ya Martinez kufikia sasa.
Lakini Bosi huyo wa Uhispania amekataa kuingia katika mjadala kuhusu hali ya mchezaji huyo wa Al-Nassr, akisema Ureno imejiandaa kushinda bila yeye.
Kati ya michezo mitatu ya maandalizi ya Euro, Ronaldo alicheza mchezo mmoja tu katika ushindi wa Jumanne dhidi ya Jamhuri ya Ireland na alipata sifa, sio tu kwa mabao yake mawili bali pia kwa tabia ya mchezaji huyo uwanjani.
Alisema kufuatia ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Ireland, "bila kujali nitacheza au la, nitaheshimu maamuzi ya kocha."
“Mara nyingi Ronaldo hucheza dakika nyingi na kufunga magoli, lakini, tukiangalia uchezaji wake, idadi ya makosa afanyayo ni mengi kuliko matendo yake chanya,” anasema Oliveira.
Gazeti la michezo la Ureno, A Bola linasema, swali lisilo sahihi ndilo analoulizwa Martinez.
Swali lisiwe ikiwa Ureno: Je, washindi wa Euro 2016 wanacheza vizuri zaidi bila nahodha wao? Badala yake swali liwe, "ni wakati gani mwafaka iwe kawaida kwa timu hii kucheza bila Ronaldo?"
Fernandes ndiye tegemeo?
Hii ni mara ya kwanza kwa Ureno kushinda kila mechi ya kufuzu mashindano makubwa.
Baada ya kupita katika kundi lililojumuisha Slovakia, Luxembourg, Iceland, Bosnia-Herzegovina na Liechtenstein, ingawa, kuna hisia kwamba timu hii haijajaribiwa kweli kweli.
Kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Croatia katika mechi ya kirafiki mapema mwezi huu kilionekana kuwa mtihani wa kwanza dhidi ya timu hiyo.
"Kumekuwa na michezo ambapo Ureno hawakucheza vizuri na bado waliishia kuwachabanga wapinzani wao,” anasema Oliveira.
Na ikiwa wanataka kurejea nyumbani na taji la Ubingwa wa Ulaya, watahitaji Bruno Fernandes kucheza katika kilele cha uwezo wake.
Nyota huyo wa kati huenda hakuwa na msimu wake bora akiwa na Manchester United, lakini amekuwa mchezaji bora wa Ureno chini ya Martinez, akifunga mabao sita na akisaidia nane katika mechi 10 za kufuzu.
La muhimu zaidi, ameonyesha kuwa yeye na kiungo wa Manchester City, Bernardo Silva wanaweza kucheza vyema pamoja kwa nchi yao.
"Bila shaka hiyo ndiyo habari njema zaidi tuliyonayo hadi sasa. Lakini habari mbaya, ni ukosefu wa matumizi mazuri ya Vítor Machado Ferreira," aliongeza Oliveira.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na Kuhaririwa na Seif Abdalla