Wakili aliyetajwa na mwanafunzi wa Saudia aliyejitoa uhai alihusishwa na ubalozi, BBC yabaini

...

Chanzo cha picha, X

Maelezo ya picha, Eden Knight alijitoa uhai mnamo 2023 baada ya kurudi Saudi Arabia na wakili Bader Alomair
Muda wa kusoma: Dakika 7

Wakati mwanamke mashuhuri wa Saudi Arabia aliyekuwa akiomba hifadhi alipochapisha barua yake ya kujitoa uhai kwenye mtandao wa X, marafiki na wafuasi wake walipata taharuki.

Ujumbe huo, uliotazamwa na mamilioni, ulieleza wakili mmoja nchini Marekani - ambako amekuwa akijaribu kuomba hifadhi - alikuwa amemshawishi kurejea nyumbani kwa familia na nchi ambayo haitakubali utambulisho wake.

BBC imebaini kuwa Bader Alomair ni wakili mwenye uhusiano na ubalozi wa Saudi Arabia huko Washington, DC.

Rekodi zinaonyesha kwamba Alomair alihusika katika kuwarudisha nyumbani wanafunzi wengine wa Saudia kutoka Marekani, baadhi yao wakikabiliwa na mashtaka makubwa, ikiwa ni pamoja na mauaji wakiwa chuo kikuu.

Bw Alomair hatoa tamko lolote kuhusiana na madai yaliyoibuliwa katika uchunguzi wetu.

Eden Knight alitoka katika familia mojawapo inayoheshimika katika moja ya falme za Mashariki ya Kati.

Baada ya kuhamia Virginia mwaka 2019 kwa ufadhili kutoka serikali ya Saudi Arabia ili kusoma katika Chuo Kikuu cha George Mason, mwanzoni mwa mwaka 2022 Eden alifanya uamuzi wa kubadilisha utambulisho wake kutoka kwa mwanaume na kuwa mwanamke, kwa kuvaa mavazi ya kike na kutumia homoni za kike.

Eden alikutana na jamii hiyo kwenye mtandao wa X kadhalika alijisikia kukubalika na kuanza kupata wafuasi mtandaoni.

Katika moja ya machapisho, aliweka picha yake ya kitambulisho cha Saudi Arabia kabla ya muonekano wake mpya wa kike, na chapisho hilo likapata umaarufu mkubwa.

...

Chanzo cha picha, X

Maelezo ya picha, Chapisho hili la Eden Knight lilizua mtindo wa kuchapisha picha za utambulisho wa zamani wa watu waliobadili jinsia kote ulimwenguni
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kuwa watu waliobadili jinsia nchini Saudi Arabia hakukubaliwi na jamii au serikali - tumezungumza na Wasaudi kadhaa waliobadili jinsia, ambao sasa wanaishi nje ya ufalme huo, ambao walituambia kuhusu unyanyasaji huo, na katika visa vingine vurugu walizopitia.

Kurudi Saudi Arabia kwa hiyo inaweza kuwa vigumu kwa Edeni. Tunaelewa kuwa muda wake wa visa ya mwanafunzi uliisha wakati wa tweet yake ya virusi hivyo aliamua kutafuta hifadhi nchini Marekani ili abaki huko kabisa.

Kufanya mabadiliko ya utambulisho wa kijinsi haikubaliki Saudi Arabia kwa jamii wala serikali - tumekuwa na mazungumzo na Wasaudia wengi waliofanya hivyo,ambao kwa sasa wanaishi nje ya ufalme, ambao walituambia kuhusu kunyanyaswa, na katika baadhi ya kesi, vurugu walizoshuhudia.

Kurejea Saudi Arabia inaweza kuwa ilikuwa vigumu kwa Eden. Tunaelewa kuwa visa yake ya mwanafunzi ilikamilika karibu na wakati wa tweet yake maarufu, hivyo aliamua kutafuta hifadhi nchini Marekani ili akae huko milele.

...

Chanzo cha picha, Supplied

Maelezo ya picha, Rafiki wa Eden Hayden (kushoto) anasema alisikia mazungumzo ya awali ya Edeni na mpelelezi binafsi Michael Pocalyko.

Marafiki wengine wametueleza ujumbe kutoka Eden, ambao unasema Bw Pocalyko alimwambia alihitaji kuhama kutoka Georgia hadi Washington DC ili kuwasilisha madai yake.

Kwa mujibu wa ujumbe wa mwisho aliochapisha kwenye mtandao wa X, mwishoni mwa Oktoba 2022, mpelelezi huyo wa kibinafsi alikutana na Eden nje ya gari moshi katika mji huo nchini Marekani. Aliandamana na wakili wa Saudi anayeitwa Bader, aliandika.

Eden alisema katika chapisho lake la mwisho, 'Kwa kweli nilikuwa na matumaini na nikaamini hili linaweza kufanikiwa.' Alisema Bader alimweka katika ghorofa nzuri karibu na Washington DC na kumpeleka kutalii.

Lakini nyakati kadhaa, inaonekana alianza kuhoji kuhusu uamuzi wake. Eden aliandika kwa marafiki zake, katika ujumbe ulioonwa na BBC, Bader alikuwa 'akiirejesha' hali yake ya awali ya kijinsia. Alisema kuwa Bader alijaribu kutupa mavazi yake yote ya kike na kumwambia aache tiba ya homoni."

Eden pia aliwaambia marafiki kwamba Bader alimshauri kuwa asingeweza kuomba hifadhi nchini Marekani na kwamba lazima arudi Saudi Arabia kufanya hivyo. Mtaalamu wa masuala ya uhamiaji wa Marekani alisema ushauri huo usingekuwa sahihi.

Mnamo Desemba 2022, Edeni alituma ujumbe kwa marafiki kusema: "Ninarudi [Saudi] na wakili na ninawatakia kila la kheri." Ujumbe wake wa kujiua kwenye mtandao wa X unaonyesha wazi kwamba wakili anayehusishwa alifahamika kama "Bader".

Haikuchukua muda mrefu kabla Eden kueleza marafiki zake kuwa kurudi Saudia ilikuwa makosa.

Aliwatumia ujumbe kuwaambia kuwa wazazi wake walichukua hati yake ya kuafiria na serikali ilimwamuru afunge akaunti yake ya X.

Eden aliwaambia marafiki zake kuwa alikuwa na ushahidi kwamba wazazi wake walikuwa wameajiri watu kumrudisha Saudi Arabia, ingawa hakuonesha ushahidi huo.

"Wakili ambaye alikuwa ananisaidia kuhusu masuala ya hifadhi alikuwa akifanya kazi na wazazi wangu kwa siri," aliwaambia mmoja wao.

Baada ya miezi kadhaa iliyofuata,marafiki wa Eden wanasema alipoteza matumaini ya kutoroka Saudi Arabia.

Alifanya kazi akiwa katika nafasi ya chini kwenye kampuni ya teknolojia huku hadharani akitumia utambulisho wake wa asili wa kiume.

Eden alituma ujumbe kwa rafiki yake kusema alikuwa akijaribu kuendelea kutumia tiba ya homoni za kike, lakini wazazi wake walimnyang'anya mara kwa mara.

Eden aliwaambia marafiki kwamba aliteswa na matusi ya mara kwa mara, na akawatumia marafiki video - ambayo tumeona - ambayo alirekodi kwa siri ya mwanafamilia akimfokea kwamba alikuwa amechanganyikiwa kwa kuwa na fikra za kimagharibi.

Unaweza pia kusoma

Eden alijitoa uhai tarehe 12 Machi 2023.

Tulitaka kupata "Bader" - wakili ambaye Eden alimshutumu kwa kumsababishia kurejelea utambulisho wake wa awali wa kiume na kumshawishi kurejea nyumbani, kumuuliza zaidi kuhusu matukio ya kifo chake.

Tulitafuta mawakili wa jina hilo katika eneo la DC, na mmoja akapatikana: Bader Alomair. Kulikuwa na maelezo machache kumhusu mtandaoni, lakini orodha ya zamani ya wataalamu wanaofanya kazi huko Riyadh ilitoa jina lake kamili kwa Kiarabu - ambayo ilitupeleka kwenye akaunti ya Facebook ambayo haikutumika inayoonyesha picha yake akiwa katika Chuo cha Sheria cha Harvard.

Katika maandishi ambayo Edeni alituma kwa marafiki, alitaja wakili wake alikuwa amesoma Harvard.

Kisha, chanzo kimoja kilichapisha picha muhimu - iliyopigwa na Eden kutoka kwenye nyumba ambayo Bw Alomair alikuwa amempangishia.

Tuliweza kupata makazi yake kwenye mtaa wa nje kidogo ya Washington DC.

Mtu mmoja pale alituambia alikuwa anamfahamu Edeni na alikuwa amemwona akiwa na Bw Alomair.

Alisema Eden alikuwa na nguo za kike, vito na vipodozi, lakini ilibidi afiche Bw Alomair alipowasili. Alimsababisha akakata nywele na kumwambia asinyoe ndevu, shahidi alisema.

Tulijaribu mara kwa mara kuwasiliana na Bw Alomair, lakini hakujibu. Tulipotembelea makazi yaliyoorodheshwa kwenye usajili wake wa DC Bar, tuliona mwanamume anayefanana na picha zake akiingia kwenye gari la SUV na kuondoka.

..
Maelezo ya picha, Nambari ya uthibitisho kwenye nambari ya gari ya Bader Alomair ilitusaidia kujua zaidi kumuhusu

Tulifuatilia, tukichukua tahadhari juu ya namba za kipekee za gari hilo - ilionyesha kuwa gari lilitolewa na ubalozi wa Saudi Arabia huko Washington DC, na kwamba mmiliki wa gari alikuwa mfanyakazi wa ubalozi.

Jukumu la Bwana Alomair katika ubalozi lilikuwa kusaidia wanafunzi wa Saudi Arabia nchini Marekani - wakili mmoja ambaye alifanya kazi naye awali alituambia.

Tuligundua makala za habari zikielezea mifano ya Bwana Alomair akisaidia wale waliokuwa wameachwa bila makazi baada ya kimbunga huko Florida, kwa mfano. Lakini pia tuligundua kwamba msaada wake ulifanyika hadi kwa hali za kutatanisha zaidi.

Mnamo tarehe 13 Oktoba 2018, wanafunzi wawili wa Saudi walikuwa wanahojiwa na polisi wa Marekani kuhusiana na kifo cha msanii wa rap chipukizi huko North Carolina - aliyeuawa kwa kisu, akisemekana kuwa na mabishano na wawili hao.

Miezi miwili baadaye, Abdullah Hariri na Sultan Alsuhaymi walikabiliwa na mashtaka ya mauaji, lakini kufikia wakati huo walikuwa wameshaondoka Marekani.

Siku nne tu baada ya shambulio la kisu, Bwana Hariri alikuwa kwenye ndege akirejea Saudi Arabia, kulingana na barua pepe tuliyoiona.

Inajumuisha maelezo ya safari za kurudi nyumbani ambapo chanzo chetu kilituambia Bwana Alomair aliandaa kwa ajili ya Bwana Hariri na Bwana Alsuhaymi.

Hakuna mwanafunzi yeyote aliyewahi kutoa maoni hadharani kuhusu kesi hiyo.

Bwana Alomair alituma taarifa za safari mwezi mmoja baadaye, barua pepe nyingine inaonyesha, ambayo chanzo chetu kinasema alihitaji ili kupata fidia kutoka kwa ubalozi wa Saudi Arabia.

...

Chanzo cha picha, Supplied

Maelezo ya picha, Picha ya Bader Alomair, tuliyopewa na chanzo kimoja

Chanzo kingine kinaeleza kuwa alifanya kazi na Bwana Alomair kuwawakilisha wanafunzi wengi wa Saudi Arabia nchini Marekani dhidi ya mashtaka mbalimbali kuanzia kuendesha gari kwa mwendo kasi hadi kuendesha gari baada ya kulewa.

"Bader alikuja kwenye mikutano akiwa na fomu ya Kiarabu iliyoandikwa na ubalozi wa Saudi Arabia kwa wanafunzi kusaini [ambayo] iliahidi kurejesha ada kwa serikali ya Saudi Arabia baada ya kurudi nyumbani."

Chanzo kilituambia kwamba wanafunzi waliweza kuonekana kwenye siku ya kwanza ya kusikiliza kesi lakini kisha kupotea kabla ya vikao vya baadaye, ingawa hatujui kama Bwana Alomair alikuwa na jukumu katika hili.

Mnamo mwaka 2019, FBI ilitoa onyo kuwa maafisa wa Saudi Arabia huenda walirahisisha kutoroka kwa raia wa Saudi kwenye mchakato wa kisheria nchini Marekani.

"FBI inatathimini kwamba maafisa wa Saudi Arabia kwa karibu wanawasaidia raia wa Saudi walioko Marekani kuepuka masuala ya kisheria, na kudhoofisha mchakato wa kimahakama wa Marekani. Tathmini hii imefikiwa kwa uhakika mkubwa."

Vyanzo vimetuambia Bw Alomair anaendelea kuishi na kufanya kazi nchini Marekani.

Anamiliki mali nyingi za kibiashara karibu na Washington DC na mnamo Agosti 2024 anaonekana kuwa ameanzisha kampuni mpya ya sheria huko Virginia, ambapo yeye anatajwa kama mshirika.

Michael Pocalyko, Bader Alomair na ubalozi wa Saudia huko Washington DC hawakujibu maswali yetu.

Tuliwasiliana na familia ya Edeni ili kuuliza ikiwa walitaka kushiriki katika simulizi hii lakini hawakujibu.

Unaweza pia kusoma

Imetafsiriwa na Martha Saranga na kuhaririw ana Ambia Hirsi