Huntha aliyefanyiwa upasuaji mara nne akiwa mtoto ili kubadilishwa jinsia yake

Chanzo cha picha, ALEJANDRA LOPEZ
- Author, Ayelen Oliva
- Nafasi, BBC
Hii ni hadithi ya maisha ya Candelaria akiisimulia katika nafsi ya kwanza.
Mimi ni Candelaria Schamun 42, nilipozaliwa madaktari walifikiri mimi ni mvulana na wazazi wangu waliniita Esteban.
Nakumbuka nikiwa chumbani kwa mama yangu, kwenye ghorofa ya kwanza katika jumba kubwa la kifahari, mwanzoni mwa miaka ya 1900 nikiwa na miaka 17, katika jiji la La Plata (Argentina) - nikijaribu mavazi kwa ajili ya sherehe ambayo ningevaa kwenda na marafiki zangu wa shuleni.
Baada ya kuzungumza kwenye simu na mmoja wao, nilishuka ngazi na kwenda kwenye ofisi ya baba, ambayo ilikuwa imebakia wazi tangu siku ya kifo chake.
Juu ya dawati ambapo aliweka karatasi zake zote, nilifungua moja ya droo na nikakuta kabrasha la kijani linalosomeka: "Candelaria."
Miongoni mwa karatasi, niligundua cheti cha kuzaliwa, na siku yangu ya kuzaliwa, na jina langu baada ya kuzaliwa, Esteban Schamun.
Ghfla nilijua, Esteban hakuwa pacha aliyekufa, lakini ni mimi mwenyewe. Baada ya mshangao, wasiwasi ulianza. Nilificha kabrasha chini ya godoro.
Nilichokuwa nimesoma kilinikera. Katika kila ukurasa, katika kila sentensi, kulikuwa na habari ambayo ilinihusu mimi.
Nilimlaani mama yangu: "Natamani ufe." Kwa baba yangu: "Ni bahati nzuri umekufa." Nililaani kuwepo kwangu mwenyewe: "Mimi ni chukizo."
Kuanzia wakati huo na kuendelea, ujana wangu uliingia gizani. Nilianza kujiumiza, kunywa pombe, kujitenga na marafiki zangu, kuwa na hasira na mama yangu, hasira na kila mtu.
Nilipitia hali ngumu sana kwa sababu sikuweza kumwambia mtu yeyote. Ilinichukua muda mrefu kuweza kusema.
Idadi ya Operesheni

Chanzo cha picha, CEDIDA
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mwezi mmoja baada ya kuzaliwa, mama yangu aligundua kuwa kila akininyonyesha nilitapika maziwa. Kwa kujali afya yangu, alinipeleka kwa daktari.
Baada ya uchunguzi wa kimatibabu, daktari wa watoto aliamuru nilazwe. Mama alimpigia simu baba yangu, akamwomba aje upesi.
Lakini masaa yalipita na hakuna mtu aliyetambua tatizo. Siku kumi za uchungu na kukata tamaa, hadi daktari alipomuomba mtaalamu wa homoni kuingilia kati.
Ndipo tatizo likajulikana. Mabadiliko ya jeni ambayo huathiri tezi za kuzalisha homoni na kuathiri uwezo wa mwili wa kuzalisha homoni. Hilo ndilo lilibadilisha muundo wa nje wa sehemu yangu ya siri.
Madaktari wa homoni walinitibu na kuhitimisha kwamba nilihitaji dawa za kudumu maishani mwangu na upasuaji.
Nikiwa na umri wa miezi 3 nilifanyiwa upasuaji wa kwanza. Niliingia kwenye chumba cha upasuaji nikiwa nimemkumbatia mama yangu. Nilikatwa kisimi ili kiendane na kisimi cha kawaida.
Lakini waliharibu mishipa ambayo inahusika na raha ya sehemu hiyo. Matokeo ambayo bado yananitesa hadi sasa.
Nikiwa na miezi 9, operesheni ya pili ilifanyika. Walijenga uke wangu na kufungua njia ya uke. Walikata, kushona, kuondoa nyama na kuunda mashavu ya uke.
Nikiwa na umri wa miaka 12, niliingia katika chumba cha upasuaji kwa mara ya tatu. Wakati huu ilikuwa ni operesheni kubwa zaidi, kuunganisha sehemu ya nje na ya ndani. Katika operesheni hii, waligundua kuwa nina ovari, uterasi na mirija ya fallopian.
Lakini uzembe wa upasuaji ulinifanya nishindwe kuzuia mikojo. Kwa miaka mitano nilikohoa na kukojoa.
Katika umri wa miaka 17, operesheni ya nne na ya mwisho. Hii ilikuwa ni operesheni ya kutenganisha uke na urethra na kurekebisha uharibifu uliotokana na upasuaji wa awali.
Mwili wangu una kovu moja juu ya jingine. Hakuna upasuaji ulioboreshaji hali yangu. Hakukuwa na ugonjwa wa kuuponya. Operesheni zote zilikuwa ni za urembo, ili kukidhi macho ya wengine.
Mbali na kushindwa kudhibiti mkojo, upasuaji ulisababisha matatizo mengine: kupoteza raha, wasiwasi na mshtuko.
Siri ya familia

Chanzo cha picha, CEDIDA
Wakati maisha ya familia yalihusu afya yangu, wazazi wangu waliapa itakuwa siri na kuahidi kutoniambia chochote.
Sambamba na hilo, katika miezi yangu ya kwanza ya maisha, waliwasilisha ombi mahakamani kuomba kubadilisha jina na jinsia katika cheti cha kuzaliwa. Walitaka hati mpya.
Mwaka mmoja baadaye, wazazi wangu walipata habari kwamba hakimu alitia sahihi uamuzi wa kubatilishwa cheti cha kuzaliwa cha Esteban Schamun na kuagiza cheti kipya kwa jina la María Candelaria Schamun.
Lakini cheti cha Esteban bado kipo na kiko ndani ya kabrasha lenye jina lake. Wazazi wangu walisherehekea uamuzi wa mahakama kama kuzaliwa upya.
Imani yao ya kidini, hasa ya baba yangu - mwanaume ambaye katika umri wa miaka 12 alikuwa na ndoto ya kuwa kasisi - ilifanya iwe vigumu kuzungumza juu ya masuala ambayo yalionekana kuwa yasiyofaa katika familia.
Ukimya ule uliniumiza sana, lakini sasa najua kitu pekee walichokuwa wanatafuta ni kunilinda.
Nilipokuwa na umri wa miaka 17 ndipo nilipopata ukweli. Na kwa kushangaza, sikufanya chochote zaidi ya kujiunga na siri ya wazazi wangu kimya kimya.
Siri iliniumiza

Chanzo cha picha, CEDIDA
Kwa miaka mingi, sikumwambia mtu yeyote. Lakini siri hiyo iliniumiza. Nilizozana na mama yangu - baba yangu alikuwa amekufa - uhusiano ulianza kuwa mbaya na niliondoka nyumbani nilipokuwa na umri wa miaka 18.
Miaka kumi baadaye ndipo nilipoweza, kwa mara ya kwanza, kuzungumza juu y a jambo hilo na mwanasaikolojia.
"Ukeketaji unachukuliwa kuwa mateso. Walikutesa. Unapitia mshtuko, ambao unaweza kulinganishwa na mshtuko ambao askari wanapata wanaporudi kutoka vitani," mtaalamu aliniambia.
Katika umri wa miaka 30, niliweza kukabiliana na mama yangu. Aliniandikia barua alikiri hawakutaka kamwe kunilea kama msichana mgonjwa. Walitaka niwe huru. Na walifanya hivyo.
"Tulifanya kila kitu ambacho madaktari walituamuru. Ikibidi kwenda China, tulikwenda China, tulikimbia kutoka sehemu moja hadi nyingine," inasema moja ya aya za barua hiyo.
"Tulifanya kila liwezekanalo ili uwe na utoto wenye furaha na wa kawaida kama ule wa watoto wengine wa rika lako."

Chanzo cha picha, ALEJANDRA LOPEZ
Baada ya kuzungumza na Mama, niliweza kubadilisha hasira niliyokuwa nimeijenga kwa miaka mingi kuwa huruma.
Mwaka 2019, katika Mkutano wa Kitaifa wa Wanawake wa Argentina, katika Warsha ya kwanza, niliamua kupaza sauti yangu.
Hiyo ndiyo ilikuwa mara yangu ya kwanza kusimulia hadithi yangu mbele ya kundi la watu nisiowajua. Nilikuwa na wasiwasi sana.
Nilikuwa wa kwanza kuinua mkono na kuanza kuzungumza. Nilizungumza sana.
Nilipomaliza walinipigia makofi na kunikumbatia. Nilipata upendo mwingi. Hapo ndipo nilipoelewa sikuwa mnyama na hadithi yangu ingeweza kuwasaidia wengine
Sikuhitaji kujificha tena. Hatua kwa hatua, kila kitu kilianza kuwa na maana. Nimeandika kitabu kusimulia hadithi yangu ili watu waache kuwakeketa wavulana na wasichana huntha.
Nina fahari ya kuwa Candelaria, ingawa pia kuna sehemu yangu ambayo bado ni Esteban. Ninatazama nyuma na kuwa na furaha kwa namna mimi nilivyo.
Ilitafsiriwa na Rashid Abdalla na kuhaririwa na Seif Abdalla












