Kile Arteta na Arsenal walichojifunza kutokana na kichapo dhidi ya PSG

Martin

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Nahodha wa Arsenal, Martin Odegaard haamini kilichotokea
    • Author, Alex Howell
    • Nafasi, BBC Sport football news reporter
  • Muda wa kusoma: Dakika 3

Arsenal walichapwa 1-0 na Paris Saint-Germain katika mechi ya kwanza ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya iliyochezwa kwenye uwanja wa Emirates.

Kikosi cha Mikel Arteta kilipata nafasi nzuri kupitia Gabriel Martinelli na Leandro Trossard lakini walishindwa kuzitumia vyema kusawazisha bao.

Hapa, BBC Sport inaangazia mambo yakujifunza kutokana na mchezo huu

Pengo la Partey laonekana wazi

Changamoto kubwa kwa Arteta kabla ya mechi hii ilikuwa jinsi ya kupanga kikosi bila kiungo wake muhimu Thomas Partey aliyekuwa amesimamishwa.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 31 ni nguzo muhimu katika safu ya kiungo ya Arsenal na alipata kadi ya njano isiyo ya lazima mwishoni mwa mechi dhidi ya Real Madrid hatua ya robo fainali, jambo lililomnyima nafasi ya kucheza mchezo huu.

Kutokana na majeraha yaliyopo kwenye kikosi cha Arsenal na Mikel Merino kucheza kama mshambuliaji wa kati katika wiki za hivi karibuni, kutokuwepo kwa Partey kulimlazimu Arteta kufanya mabadiliko kikosini.

Merino alirudi katika nafasi yake ya kawaida ya kiungo, Declan Rice alishushwa hadi namba sita (kiungo wa ulinzi), badala ya namba nane ambayo aling'ara nayo dhidi ya Real Madrid. Trossard alicheza kama mshambuliaji.

PSG walitawala kuanzia mwanzo wa mchezo na walikuwa na umiliki wa mpira kwa 75% katika dakika 15 za mwanzo, wakifunga bao la mapema dakika ya nne kupitia kwa Ousmane Dembele.

Dembele alikuwa akipenya mara kwa mara kati ya safu ya ulinzi na kiungo ya Arsenal, na alifunga bao la kuongoza kwa mbinu hiyo hiyo.

Swali ambalo Arteta atajiuliza ni kama Partey angekuwepo, je, angeweza kumzuia Dembele kupokea mpira kabla hajafunga?

Partey amekuwa katika kiwango bora wiki za karibuni na atakuwa muhimu kwa Arsenal wiki ijayo iwapo wanataka kupindua matokeo na kufuzu fainali.

Kvaratskhelia dhidi ya Timber - vita muhimu

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Ubora wa PSG haukuwa jambo la kushangaza kwa Arsenal wala Arteta.

Timu hiyo ya Ufaransa tayari imewaondoa vilabu viwili vya Ligi Kuu ya England, Aston Villa na Liverpool hadi kufika hatua hii, na waliwafunga Manchester City katika hatua ya makundi.

Hata hivyo, walipokutana na Arsenal Oktoba katika hatua ya makundi, PSG hawakuwa na Khvicha Kvaratskhelia aliyesajiliwa Januari kwa euro milioni 70 (pauni milioni 59).

Jurrien Timber amekuwa mmoja wa wachezaji bora zaidi wa Arsenal msimu huu kwa sababu ya uthabiti, ubora wa kushambulia na uwezo wa kucheza nafasi yoyote ya ulinzi.

Lakini beki huyo wa Uholanzi alipata wakati mgumu kipindi cha kwanza dhidi ya winga huyo wa upande wa kushoto wa PSG.

Kvaratskhelia alitoa pasi ya bao hilo, akipenya hadi ndani ya boksi na kumrudishia mpira Dembele aliyefunga kutoka pembeni ya eneo la hatari.

Mwingereza Bukayo Saka alirudi mara kadhaa kumsaidia Timber kumdhibiti Mgeorgia huyo.

Timber alionekana kupata nafuu kipindi cha pili ambapo Arsenal walimiliki mpira zaidi na alifanikiwa pia kupanda kushambulia.

Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Timber kwa muda mrefu kukumbana na mshambuliaji aliyemsumbua kiasi hicho.

"Tusipomiliki mpira, tumekwisha" – Rice

Hayo yalikuwa maneno ya kiungo Declan Rice wakati akipasha misuli na wenzie kabla ya mechi, yaliyorekodiwa na kamera za TV.

Hofu ya Arsenal kutokumiliki mpira ilijidhihirisha waliposhindwa kupata udhibiti wa mchezo, huku PSG wakitawala sehemu kubwa ya kipindi cha kwanza.

Hata hivyo, Arsenal walirejea mchezoni kipindi cha pili na licha ya PSG kuanza kwa kasi, walimaliza mechi wakiwa na 52% ya umiliki wa mpira.

Mikel Arteta alisema haiwezekani kuidhibiti PSG kwa dakika 95 na kwamba mchezo uliamuliwa na "mambo madogo sana."

Arteta alisema:

"Hii ni moja ya timu bora kabisa, wakiwatoa vilabu vyote vya England. Huwezi kuitawala timu hii kwa dakika 95. Sahau kabisa."

"Na lazima uelewe maana ya kuitawala timu kama hii na ni maeneo gani ya uwanja unaweza kufanya hivyo."

'Tofauti ilikuwa ndogo sana'

Ni kipindi cha kwanza tu cha pambano hili na Arteta anasema kikosi chake kitashughulikia mechi ya marudiano kwa mtazamo uleule waliosafiri nao kwenda Madrid na uongozi wa 3-0 katika robo fainali.

"Lazima tuende Paris na kushinda mchezo huo," aliongeza. "Tuna uwezo wa kufanya hivyo."

"Nimeona timu mbili bora, lakini tofauti ilikuwa ndogo sana. Wao walitumia vizuri nafasi yao mbele ya goli. Kipa pia alitoa mchango mkubwa kwenye matokeo."

"Sijui asilimia, lakini tuna nafasi kubwa ya kufuzu fainali. Ni lazima ufanye kitu cha kipekee kwenye mashindano kama haya ili kufuzu. Na wakati wa kufanya hivyo ni kule Paris."

Luis Enrique: PSG "watalazimika kuteseka"

Ingawa Donnarumma aliokoa michomo miwili kuzuia mabao ya Arsenal, PSG walipata nafasi pia za kuongeza idadi ya mabao.

Bradley Barcola alipiga shuti lililoenda nje, na Goncalo Ramos aligonga mwamba dakika za mwisho.

Kocha wa PSG Luis Enrique anatarajia timu yake "iteseke" katika mechi ya marudiano kule Paris.

Luis Enrique alisema:

"Hisia huwa juu sana kwenye mechi za aina hii hivyo ni vigumu kufanya tathmini. Kulikuwa na mazingira ya ajabu lakini tulionyesha aina ya timu tuliyonayo."

"Tulicheza kwa mtindo wetu na tukapata bao la mapema kwa mtindo huo huo. Tuliteseka kwa wakati fulani lakini tulistahili bao la pili. Mechi ya pili itakuwa ngumu sana."

"Tunatakiwa kujiandaa kwa mechi hiyo. Ingawa tuna faida ndogo, tunajua tutateseka. Lakini tunaamini tunaweza kufuzu fainali."