Kwanini Simba SC imefungwa Morocco lakini haijachapwa fainali CAF?

    • Author, Yusuph Mazimu
    • Akiripoti kutoka, BBC Dar es Salaam
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Kwa wengi waliotazama dakika 90 za kwanza za nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kati ya RS Berkane ya Morocco na Simba SC ya Tanzania, kilichotokea jioni ya Mei 17 hakikuwa kigeni, ni mwendelezo wa simulizi ya ukatili wa nyumbani wa Wamoroko hao.

Katika dimba lao la Stade Municipal de Berkane, Simba walifungwa mabao 2-0, kwa Mabao ya Mamadou Camara na Oussama Lamlaoui ndani ya dakika 14 za kwanza za mchezo huo.

Lakini kilichoandikwa kwenye majalada ya CAF ni tu mabao mawili na si madhara halisi ya fainali hiyo kwa mizunguko yote miwili. Kwa waliotegemea Simba ingechapwa na 'kuchapika' kwenye uwanja huo wa Stade Municipal de Berkane, kama kilichowakuta CS Constantine, Dadje, au Stellenbosch, majibu hayakuwa hivyo. Simba walinusurika zaidi ya walivyoshindwa.

Kwa namna ilivyo, dakika 15 za kwanza mchezo huo zilionyesha Simba 'ingechapika', lakini waling'ang'ana na kuruhusu mabao 2-0 tu. Hii ndiyo maana makala hii haingalii tu kilichotokea lakini inaelezea kwanini Simba SC imefungwa lakini haijachapwa fainali CAF? na kwanini kilichotokea kinaacha mlango wazi kwa mapinduzi ya kihistoria kwa Simba

Imefungwa kwa matarajio, si kwa kichapo

Katika jiji dogo la Berkane, palipojengwa uwanja unaoitwa na wengi "machinjio ya Afrika," uwanja Stade Municipal de Berkane, Simba SC walijaribu kuvuka salama, wakijua fika kuwa waliokuwa mbele yao si tu wapinzani bali walikuwa ni wachinjani wa kutisha wakiwa nyumbani. Na takwimu zinaonyesha hilo.

Katika mechi sita za nyumbani msimu huu kwenye mashindano ya Kombe la Shirkisho la CAF, Berkane hajafungwa goli hata moja nyumbani wakifunga jumla ya mabao 20 kwenye uwanja huo kwa msimu huu.

Na wamekuwa wakitoa vichapo vikubwa vikubwa hapo. Katika hatua ya nusu fainali waliwachapa bila huruma CS Constantine mabao 4-0. Waliwachapa Stellenbosch ya Afrika Kusini kwa mabao 5-0 kwenye hatua ya makundi. Kichapo kingine kikubwa kiliwakuta Dadje ya Benin waliochapwa mabao 5-0 kwenye hatua za awali.

Ni ASEC Mimosas ya Ivory Coast ambayo ina ukuta mgumu iliyofungwa bao moja kwenye uwanja huo na sasa Simba imefungwa mabao 2-0.

Kwa muktadha huo, kupoteza kwa mabao mawili si tu matokeo bali ni matokeo ya kutia matumaini kwa Simba.

Wangekuwa wamefungwa kwa kuchapwa mabao 3-0, 4-0 au 5-0 kama walivyofanywa wengine, mechi ya marudiano ingekuwa sawa na taratibu za mazishi ya matumaini. Lakini mabao 2-0 kwa Simba, ni kama kuokota pumzi katikati ya kimbunga. Upo uhai na kwa namna fulani, uhai huo upo mlangoni mwa historia.

"Hatujapata bao ni kweli ila hatujilaumu, wao ndio watajilaumu kutopata bao la tatu", anasema kocha wa Simba, Fadlu Davids

Tazama hapa

Simba na rekodi ya matumaini nyumbani

Kama Berkane wana machinjio yao nyumbani, basi Simba wana zizi la halali Dar es Salaam. Wanaweza kuamua ngo'mbe apelekwa ama asipelekwe machinjioni, na wanaweza kuamua wachinje wenyewe na kumla wenyewe. Berkane anaweza kuchinjwa na kuliwa katika uwanja wa Mkapa, kama mchezo huo utapigwa kwenye uwanja huo. Kwa sababu kuna taarifa za kupelekwa uwanja wa Amani Zanzibar.

Katika mechi 11 zilizopita za mashindano ya CAF zilizopigwa Benjamin Mkapa, Simba wamepoteza moja tu dhidi ya Al Ahly. Ni katika uwanja huo huo walipopindua matokeo dhidi ya Kaizer Chiefs kwa 3-0 misimu minne iliyopita, japokuwa hawakufuzu kwa jumla, kwa kuwa mchezo wa kwanza walifungwa 4-0 kule Afrika Kusini.

Rekodi hiyo si ya kupuuzwa ni msingi wa matumaini. Na si tu historia, bali pia hali halisi. Simba wanarudi nyumbani wakijua kwamba bao la mapema linaweza kugeuza mchezo, na bao la pili linaweza kulipua jiji la Dar es salaam na Afrika Mashariki kwa ujumla. Kocha wao Fadlu Davids amesisitiza kuwa, "tutapata matokeo nyumbani," huku akisisitiza mechi kubaki Benjamin Mkapa kama haki yao badala ya kupelekwa Zanzibar, kama itathibitshwa na mamlaka za soka. Unaweza kumuelewa kocha huyo na kila mwanasimba kutaka Mchezo upigwe kwa Mkapa, kwa sababu uwanja huu umewapa matokeo ya zaidi ya asilimia 90% katika mechi 11 za hivi karibuni

Sasa swali limebaki moja, rekodi yao ya nyumbani itatosha kuvunja ukuta wa Berkane?

Je, itaweza kuifunga Berkane kwa kuichapa?

Simba hawahitaji tu kushinda iwe kwa Mkapa ama Zanzibar, wanahitaji kushinda kwa kuichapa Berkane. Kushinda kwa mabao mengi. Na hilo ndilo jambo gumu zaidi katika medani za CAF kwa sasa. Berkane ni timu isiyopasuka, isiyochapika kwa mabao mengi. Ukuta wa Adil Tahif, Moussaoui, Assal na Haytam Manaout, una ulinzi wa kisasa unaochanganya kasi, nidhamu na uzoefu. Kipa Munir Mohamedi, mwenye historia ya Kombe la dunia akiwa na Morocco, amekuwa mhimili wa ngome hiyo.

Wakiwa ugenini msimu huu, Berkane hawajafungwa hata mara moja kwa mabao mawili au zaidi. Constantine waliwashinda 1-0 tu. ASEC walifungwa 1-0. Stellenbosch walifungwa 3-1. Mamadou Camara, kiungo wao wa kati, huongoza mashambulizi na ulinzi kwa wakati mmoja, akitengeneza usawa usiopasuka. Aliisumbua sana Simba kule Morocco na wana kazi ya kupunguza kasi, akili na uwezo wake. Si mchezaji wa kawaida, hasa kwa mechi zisizo za kawaida kama hii inayokuja dhidi ya Simba.

Hata hivyo Msimu huu kwenye mashindano ya CAF, Simba iliweza kupindua meza. Robo fainali walikumbana na Al Masry, wakapigwa 2-0 kule Misri, kabla ya kurudi nyumbani na kushinda 2-0, wakafuzu kwa penalti. Huo ni ushahidi kwamba lolote linawezekana.

Lakini tatizo kubwa la Simba linaloonekana na wachambuzi wengi ni kuruhusu mabao ya mapema.

"Kwenye magoli 8 ambayo Simba SC imefungwa kuanzia makundi hadi Fainali ya kombe la Shirikisho, magoli 5 (63%) amefungwa kwenye dakika 20 za mwanzo. Magoli 8 hayo, 5 (63%) yametokana na makosa binafsi safu yake ya ulinzi (Camara, Malone, Kagoma & Hamza)", anasema mwandishi wa habari za michezo Abissay Stephen Jr kutoka Tanzania.

Na anaongeza " Hawawezi kuhimili presha ya mwanzo wa mechi".

Kwa mantiki hiyo, mechi ya Mei 25 haitakuwa tu mchezo wa marudiano, bali itakuwa fainali ya fainali na pambano la mwisho la msimu, la hadhi ya kihistoria. Simba hawataki tu kulipiza kisasi, au kuziba madhaifu yao bali wanataka pia kuandika ukurasa mpya kwenye historia ya soka la Afrika Mashariki. Kushinda taji lao la kwanza la Afrika na kuwalaza mapema watani zao Yanga kwa kejeli na utani na tambo za hapa na pale.