Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Siku ya Kupinga Tumbaku: Jinsi tumbaku inavyoharibu mwili wako
- Author, Rashid Abdallah
- Nafasi, BBC Swahili
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Siku ya Kupinga Matumizi ya Tumbaku Duniani, pia inajulikana kama "Siku ya Tumbaku," huadhimishwa Mei 31 kila mwaka. Siku hii inalenga kuongeza uelewa juu ya hatari za matumizi ya tumbaku, hatua za kudhibiti tumbaku na kufichua mbinu hatari zinazotumiwa na makampuni ya tumbaku.
Nchi Wanachama wa Shirika la Afya Ulimwenguni ziliunda Siku ya Kupinga Matumizi ya Tumbaku Duniani mwaka 1987 ili kueleza janga la tumbaku, vifo vinavyoweza kuzuilika na magonjwa yanayosababishwa na tumbaku.
Matumizi ya tumbaku, haswa kupitia sigara, yana athari mbaya kwa mwili - hudhuru karibu kila kiungo katika mwili, na uvutaji sigara ni moja ya sababu kuu ya vifo vya mapema.
Kwa mujibu wa WHO, matumizi ya tumbaku huuwa takribani watu milioni sita kila mwaka. Watu laki sita kati ya hao, hufa kutokana na kuathiriwa na moshi wa sigara zinazovutwa na watu wengine.
Inakadiriwa kuwa kufikia mwaka 2030 watu milioni nane watakuwa wanakufa kwa sababu ya tumbaku, kwa mujibu kwa Taasisi ya Saratani ya Marekani (ACS). Katika nchi ya Marekani pekee, uvutaji sigara husababisha vifo vya watu 480,000 kila mwaka.
Matumizi ya tumbaku barani Afrika yana athari mbaya kiafya, kimazingira na kiuchumi. Kwa upande wa afya, ni chanzo kikuu cha vifo vinavyoweza kuzuilika, kutokana na magonjwa mbalimbali ya saratani, magonjwa ya moyo na mapafu. Kimazingira, kilimo cha tumbaku kinaweza kusababisha ukataji miti na uharibifu wa udongo. Kiuchumi, matumizi ya tumbaku huelemea mifumo ya afya kama hospitali.
Saratani
Kwa mujibu wa Taasisi ya Kufuatilia Matumizi ya Dawa za Kulevya (NIDS), yenye makao makuu yake Marekani, kuna takribani kemikali 69 katika moshi wa tumbaku – kemikali ambazo husabaisha kansa. Uvutaji wa sigara husababisha asilimia 30 ya vifo vyote vya saratani.
Viwango vya jumla vya vifo vinavyotokana na saratani ni vya juu miongoni mwa wavutaji sigara kuliko wale wasiovuta sigara. Wavutaji wana hatari zaidi ya kufa kutokana na saratani mara nne kuliko watu wasiovuta.
Kati ya saratani zinazosababishwa na matumizi ya tumbaku ya kwanza ni saratani ya mapafu. Uvutaji wa sigara huchangia asilimia 80 hadi 90 ya visa vyote vya saratani ya mapafu. Vilevile sigara huongeza hatari ya saratani ya mapafu mara tano hadi kumi.
Uvutaji sigara pia unahusishwa na saratani za mdomo, koromeo, zoloto, umio, tumbo, kongosho, mlango wa uzazi, figo na kibofu cha mkojo, na pia kansa ya damu.
Mfumo wa upumuaji
Utumiaji wa tumbaku, haswa kupitia uvutaji sigara, una madhara makubwa kwenye mfumo wa upumuaji. Huathiri njia za hewa, hupunguza utendakazi wa mapafu, na huongeza hatari ya magonjwa mbalimbali ya kupumua, na huzidisha hatari ya kupata pumu kwa watu wazima na watoto.
Kwa mujibu wa shirika la kukagua ubora wa chakula na dawa la Marekani (FDA), moshi wa tumbaku una kemikali nyingi hatari zinazoweka utando katika mirija ya hewa, na hivyo huleta muwasho unaosababisha uvimbe katika njia ya hewa, na kufanya kuwa vigumu kupumua. Mwili hujaribu kupambana na hali hiyo kwa kutoa kamasi zaidi, ambazo zinaweza kukinza njia za hewa.
Uvutaji sigara hudhoofisha ulinzi wa asili wa mwili dhidi ya maambukizo, na kuwafanya wavutaji sigara kuathiriwa zaidi na maambukizo ya kupumua kama vile nimonia na kifua kikuu. Moshi wa tumbaku una kabon monoksidi, ambayo hupunguza kiasi cha upitishaji wa oksijeni ambayo damu inaweza kubeba.
Uvutaji sigara ni sababu kuu ya saratani ya mapafu, ugonjwa mbaya na mara na hatari. Moshi wa sigara pia huleta hatari kubwa kwa mfumo wa upumuaji, haswa kwa watoto na wale walio na pumu.
Magonjwa ya moyo
Uvutaji wa sigara huathiri moyo na mishipa ya damu, na hivyo kuongeza hatari ya magonjwa mbalimbali ya moyo na mishipa, kama shinikizo la damu na mapigo ya moyo, hupunguza mtiririko wa damu na oksijeni kwenda katika tishu, na huongeza hatari ya kuganda kwa damu, ugonjwa wa moyo, mshituko wa moyo na kiharusi.
Kwa mujibu wa taasisi ya Heart Foundation kutoka Australia, uvutaji sigara hupunguza kiwango cha oksijeni ambayo damu inaweza kubeba, na kuifanya iwe vigumu kwa moyo kufanya kazi kwa ufanisi. Sigara huongeza hatari ya kuganda kwa damu kwenye mishipa, na kuzuia mtiririko wa damu na kusababisha mshtuko wa moyo au kiharusi.
Matumizi ya sigara yanaweza pia kusababisha mapigo ya moyo yasiyo ya kawaida, kupanuka kwa moyo, na udhaifu wa moyo. Kwa mujibu wa taasisi ya Moyo, Mapafu na Damu (NHLBI), kutoka Marekani, magonjwa ya moyo yanahusika kwa asilimia 40 na vifo vyote vinavyohusiana na uvutaji sigara.
Habari Njema
Kwa mujibu wa ripoti ya WHO ya mwaka 2024, matumizi ya tumbaku miongoni mwa vijana katika eneo la Afrika yalipungua kwa karibu 18% kati ya 2020 na 2022, na kwa 46% kati ya watu wazima katika kipindi kama hicho huku nchi zikichukua hatua kali za kudhibiti matumizi ya tumbaku.
Kanda ya Afrika iko mbioni kufikia asilimia 30 ya kupunguza kiwango cha matumizi ya tumbaku ifikapo mwaka 2025, kulingana na WHO. Kwa msaada kutoka WHO na washirika, nchi za Afrika zimeanzisha sheria na kanuni madhubuti dhidi ya tumbaku.
Asilimia 96 ya nchi hizo sasa zimeridhia Mkataba wa WHO wa Kudhibiti Tumbaku, Mauritius ikiwa nchi ya kwanza Afrika kutekeleza kikamilifu mpango mzima wa WHO MPOWER katika kudhibiti tumbaku, na kuchangia kupungua kwa matumizi ya tumbaku miongoni mwa watu wenye umri wa kuanzia miaka 16 hadi 64, kutoka 18% hadi 10% kati ya 2012 na 2021.
Kwa kuongezea, nchi 37 za Afrika sasa zina marufuku ya uvutaji sigara hadharani, huku 14 kati ya hizi zikiweka katazo la kutovuta sigara katika maeneo yote ya umma. Nchi nyingine 16 zimeanzisha maonyo ya kiafya kuhusu bidhaa za tumbaku.
WHO pia ilianzisha hatua za kibunifu za kukabiliana na ongezeko la uzalishaji wa majani ya tumbaku, na kuhimiza zaidi ya wakulima 5,000 wa tumbaku nchini Kenya na Zambia kuanzisha kilimo kingine mbadala. Hii ilikuwa na faida kadhaa, kupunguza uzalishaji wa tumbaku, ulinzi wa mazingira, na uwezeshaji wa watu masikini.
Ni muhimu kukumbuka, habari hii njema inawahusu walioacha tu matumizi ya tumbaku, ikiwemo sigara.