Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
'Kisiwa cha kifo' kilichofanyiwa majaribio wakati wa Vita vya Pili vya Dunia
Katika miaka ya 1960, BBC iliamua kuchunguza ripoti za siri, majaribio ya kushangaza ya Vita vya Pili vya Dunia, uchafuzi hatari na vifo vya wanyama visivyoelezewa kwenye kisiwa cha mbali karibu na pwani ya Scotland.
"Hapa, wanakiita kisiwa cha kifo, Kisiwa cha ajabu, na kwa sababu nzuri," alisema mwandishi wa BBC Fyfe Robertson alipokuwa akisimama kando ya bahari kutoka kisiwa cha Gruinard cha Uskoti mwaka wa 1962.
"Sasa, hii si hadithi ya matendo ya zamani ya giza au ushirikina. Hapana, hadithi hii ilianza mwaka wa 1942. Vita vilikuwa vinaendelea kwa miaka mitatu ambapo ghafla kundi la kisayansi kutoka Ofisi ya Vita lilitwaa kisiwa na kuanza majaribio ya siri sana kwamba hata leo, miaka 20 baadaye, watu wachache sana wanajua nini kiliendelea huko.
Robertson alikuwa akilenga kuchunguza hadithi za majaribio hatari ya serikali ambayo yaliaminika kutokea kwenye Gruinard. Wakati alipokuwa akiripoti, Wizara ya Ulinzi ya Uingereza ilikuwa tayari imetangaza kuwa kisiwa hicho hakiruhusiwi na Robertson hakuweza kuwashawishi wenyeji wenye uoga kuzunguka kisiwa hicho ili kukiangalia kwa karibu.
Ilikuwa ni janga la mazingira. Kisiwa hicho kilibakia kikiwa hatari na eneo la kutokwenda kwa karibu nusu karne, hadi, siku hii ya 1990, serikali ya Uingereza hatimaye ilitangaza Kisiwa cha Gruinard kuwa salama.
Ukweli ni kwamba Kisiwa cha Gruinard kilikuwa mahali pa jaribio la siri la Uingereza wakati wa Vita vya Pili vya Dunoa ili kufanyia majaribio ya Kimeta, maambukizi hatari ya bakteria. Maelezo kamili ya kile kilichotokea huko yangedhihirika tu mnamo 1997 serikali ilipoondoa uainishaji wa filamu ambayo wanajeshi waliitengeneza wakati huo, ambayo ilielezea kwa undani majaribio hayo.
Mradi huo, unaoitwa Operation Vegetarian, ulianza chini ya Paul Fildes, ambaye wakati huo alikuwa mkuu wa idara ya biolojia huko Porton Down, kituo cha kijeshi huko Wiltshire, Uingereza, ambacho bado kipo hadi leo.
Porton Down kilikuwa kimeanzishwa kwa mara ya kwanza mnamo 1916 kama Kituo cha Majaribio cha Idara ya Vita ili kuchunguza athari za silaha za kemikali, ambazo zilikuwa zikitumika zaidi wakati Vita vya Kwanza vya Dunia vilikuwa vikiendelea. Katika miaka ya 1940, Uingereza ikiwa vitani tena, Porton Down kilipewa jukumu la kutengeneza silaha za kibaolojia ambazo zingeweza kutumika dhidi ya Ujerumani ya Nazi kwa athari mbaya, kupunguza mapigano ya moja kwa moja kati ya askari.
Mpango ulikuwa ni kuweka kwa keki spora za Kimeta na kuzitupa kwa ndege kwenye malisho ya ng'ombe karibu na Ujerumani. Ng’ombe wangekula keki na kuugua Kimeta, saw ana wale waliokula nyama iliyoambukizwa. Kimeta ni kiumbe kinachotokea kiasili lakini kinaua. Dalili za maambukizo zinaweza kuchukua muda kuonekana kikamilifu lakini zinapotokea ni za kutisha na zinaweza kuua haraka sana. Mpango uliopendekezwa ungepunguza ugavi wa nyama wa Ujerumani, na kusababisha uchafuzi wa Kimeta nchini kote, na kuchangia idadi kubwa ya vifo.
Lakini ili kuelewa jinsi Kimeta kingefanya kazi kama silaha katika mazingira halisi, watafiti walihitaji eneo le nje mbali na maeneo yenye watu wengi ili kujaribu. Katika majira ya kiangazi ya 1942, wanajeshi walinunua kisiwa cha Gruinard cha mbali, kisicho na watu cha ekari 522, na kupiga marufuku wenyeji kufika huko.
Timu ya kijeshi, chini ya usimamizi wa wanasayansi, kisha ikaanza kufanya majaribio ya kutisha. Kwa kutumia mifugo iliyoletwa kisiwani humo kufanyiwa majaribio, walianza mfululizo wa majaribio ya kutoa spora za Kimeta katika eneo la kisiwa hicho.
"Lengo lilikuwa kupima kama ugonjwa wa Kimeta ungebaki baada ya mlipuko uwanjani, hawakujua hilo, halafu ungebaki na hali mbaya baada ya hapo," Edward Spiers, profesa aliyestaafu katika Chuo Kikuu cha Leeds aliambia makala ya BBC The Mystery of Anthrax Island mnamo 2022.
"Kondoo themanini walikuwa wamefungiwa katika hatua mbalimbali chini ya uwezekano wa mlipuko. Mlipuko huo ulifanywa na udhibiti. Sio mlipuko mkubwa, ni spora zinazosonga kwenye upepo na kusababisha maambukizi na kifo popote zinapokwenda."
Matokeo yalikuwa mabaya: ndani ya siku kadhaa kondoo walianza kuonyesha dalili na haraka wakaanza kufa. Mizoga yao iliyoambukizwa ilichomwa moto au kufukiwa chini ya tani nyingi za udongo.
Baadhi ya majaribio haya yalishuhudiwa na wafugaji wa ndani ambao waliona mawingu ya Kimeta juu ya kisiwa hicho. Mtu mmoja, ambaye alikuwa ameuza kondoo kwa timu ya wanasayansi, alikumbuka kwamba aliona kile alichoeleza kuwa moshi ukishuka juu ya wanyama hao. "Nadhani ilikuwa kila aina ya gesi ya sumu, Kimeta," aliiambia Robertson mnamo 1962.
Majaribio ya siri yaliendelea hadi 1943, wakati jeshi liliona kuwa na mafanikio, na wanasayansi walipakia na kurudi Porton Down. Matokeo yake keki milioni tano zilizounganishwa na Kimeta zilitolewa lakini mpango huo hatimaye uliachwa huku uvamizi wa Washirika wa Normandy ukiendelea, na kusababisha keki kuharibiwa baada ya vita.
Kufikia 1952, Uingereza ilikuwa imetengeneza silaha tofauti ya maangamizi makubwa na ilikuwa imefaulu katika azma yake ya kuwa nchi ya tatu yenye nguvu za nyuklia duniani. Miaka minne baadaye ilimaliza mipango yake ya silaha za kemikali na kibaolojia, na mwaka wa 1975 iliidhinisha Mkataba wa Silaha za Kibiolojia, ambao unapiga marufuku matumizi yote, uzalishaji au kuhifadhi.
'Operation vegetarian'
Matokeo ya Operation Vegetarian yalikuwa janga kwa kisiwa hicho. Kimeta ni bakteria sugu sana na inaweza kudumu kwa miongo kadhaa kwenye udongo, na kusababisha maambukizi inapomezwa hata miaka kadhaa baada ya mlipuko. Majaribio ya wanajeshi yalikuwa yamekiacha kisiwa hicho kuwa hatari sana kwa watu au wanyama kuishi, huku hata maji ya mvua yakioshwa kutoka kisiwani kuwa hatari.
Katika miezi iliyofuata majaribio hayo, wanyama kwenye bara karibu na Gruinard Bay walianza kufa. Kama Elizabeth Willis anavyosema katika makala yake, serikali ya Uingereza ililipa fidia kimya kimya kwa wale walioathiriwa lakini ilidai vifo hivyo ni matokeo ya kondoo mgonjwa ambaye alikuwa ameanguka kutoka kwa meli ya Ugiriki iliyokuwa ikipita.
Mmoja wa wenyeji aliiambia BBC mwaka wa 1962: "Ilikuwa dhahiri kwetu kwamba walijua kitu kuhusu hilo la sivyo hawangelipa haraka kama walivyofanya."
Wanajeshi waliweka kuzuizi kwenye kisiwa hicho kwa muda usiojulikana, na kuweka mabango ya kuwaonya wageni.
Katika miongo iliyofuata mwisho wa Vita vya Pili vya Dunia, majaribio yalifanywa ili kuondoa uchafuzi wa tovuti kwa kutumia kemikali na uchomaji uliodhibitiwa, lakini haukufaulu. Msururu wa majaribio mwaka wa 1971 ulionyesha kwamba ingawa hakukuwa na spora za Kimeta juu ardhi, bado zilikaa kwenye udongo chini, na hivyo kusababisha hatari kubwa kwa mtu yeyote anayeingia kwenye kisiwa hicho.
Mnamo 1981, kikundi cha mazingira kinachoitwa Dark Harvest Commandos kilitua kwenye kisiwa hicho na kuchukua sampuli za udongo wenye ugonjwa wa Kimeta. Waliacha ndoo ya udongo huo nje ya Porton Down ili kuangazia uchafuzi huo mbaya kwenye kisiwa hicho, wakilenga kulazimisha serikali kufanya jambo fulani.
Miaka mitano baadaye, wanasayansi walirudi kujaribu tena juhudi za kuondoa uchafuzi, wakilowesha kisiwa katika mchanganyiko wa maji ya bahari na formaldehyde, na pia kuondoa na kuchoma udongo wa juu uliochafuliwa. Wakati huu walikuwa na mafanikio zaidi na hatimaye, tarehe 24 Aprili 1990, baada ya miaka 48 ya karantini, Serikali ya Uingereza ilitangaza kisiwa cha Gruinard kuwa salama.
Gruinard halikwa eneo pekee ambapo Uingereza ilifanya majaribio ya siri ya silaha za kibaolojia, lakini ilikuwa ya kwanza. Matokeo ya kile kilichotokea huko ni ushuhuda mbaya wa hatari za vita vya kibiolojia na uwezo wa kumuangamiza mwanadamu.