Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Prolapse:Niligundua uvimbe kwenye uke wangu
Na Hayley Jarvis
Mwandishi wa BBC Scotland
Natashja Wilson alipogundua kwa mara ya kwanza alikuwa na dalili za kuzorota kwa kiungo cha fupanyonga hakujua kilichokuwa kikitendeka na alikuwa na aibu sana kuomba msaada.
Akiwa na umri wa miaka 18 tu na akiishi mbali na nyumbani katika chuo kikuu, hajawahi kusikia kuhusu hali hiyo ambayo inaweza kuathiri hadi 50% ya wanawake wakati wa maisha yao.
"Niligundua wakati nikienda chooni kidonda kilikuwa kinatoka kwenye uke wangu," alisema.
"Pia nilikuwa nikipata kutoweza kujizuia na maumivu wakati wa kujamiiana na hisia za uvimbe.
"Sikujua la kufikiria kwa sababu sikujua chochote kuhusu mwili wangu wakati huo."
Natashja, ambaye sasa ana umri wa miaka 24, anasema hakujua sakafu yake ya fupanyonga au seviksi yake ilikuwa nini wakati huo.
"Kwa hivyo niliwauliza marafiki zangu 'Je, hisia hii ya uvimbe ni ya kawaida?'," alisema.
"Walisema, 'Labda ni eneo lako la G. Labda ni sehemu tu'."
Natashja, kutoka Greenwich huko London, hakujua la kufikiria hivyo aliuacha uvimbe huo na kutumaini kwamba ungeenda kadri muda ulivyopita.
Lakini dalili zake zilizidi kuwa mbaya na baada ya miezi 18 hatimaye alimweleza siri mama yake ambaye alimshawishi kuonana na daktari. Baadaye ilithibitishwa kuwa alikuwa na prolapse ya uterasi.
Kuongezeka kwa viungo vya fupanyonga au (Pelvic organ prolapse)hutokea wakati kundi la misuli na tishu ambazo kwa kawaida zinaunga mkono viungo vya fupanyonga , inayoitwa sakafu ya fupanyomga , inakuwa dhaifu na haiwezi kushikilia viungo vyema.
Husababisha kiungo kimoja au zaidi kushuka kutoka kwenye nafasi yake ya kawaida, na kusababisha uvimbe unaoweza kuhisiwa ndani au nje ya uke. Hii inaweza kuwa tumbo, kibofu au juu ya uke.
Wanawake wengi hawajui kuwa wana prolapse au wana dalili ndogo tu, lakini kwa wengine inaweza kuwa na athari halisi juu ya ubora wa maisha yao.
Dalili zinaweza kujumuisha hisia nzito ya kukokota au hisia ya kitu kikishuka chini ya uke - ambayo wakati mwingine hufafanuliwa kama hisia ya 'kuketi juu ya mpira wa tenisi' pamoja na matatizo ya kibofu na matumbo na uchungu wakati wa ngono.
Mazoezi ya sakafu ya nyonga na mabadiliko ya mtindo wa maisha yanaweza kusaidia kuboresha dalili, lakini wakati mwingine matibabu yanahitajika au hata upasuaji.
Sababu za prolapse ni pamoja na maumbile, kuinua vitu vizito, kuvimbiwa au kikohozi cha kudumu.
Mimba na kuzaa huongeza hatari ya prolapse, haswa baada ya leba ngumu.
Wanawake pia wana uwezekano mkubwa wa kuwa na prolapse kadiri wanavyozeeka, haswa baada ya kukoma kwa hedhi.
Lakini Natashja ana nia ya kuwafahamisha watu kuwa inaweza kuathiri vijana pia.
Anajaribu kuondoa unyanyapaa unaotokana na kuzorota kwa kiungo cha fupanyonga kupitia mitandao ya kijamii na blogu yake ya 'Living With Prolapse'.
"Bado kuna unyanyapaa mwingi kuhusiana na na prolapse, na kujadili sehemu zako za siri na hiyo hairuhusu watu kwenda kumuona daktari," alisema.
"Najua kama kungekuwa na unyanyapaa mdogo ningeenda kwa daktari mapema zaidi."
Vikwazo vya kupata matibabu
Kulingana na Taasisi ya Kitaifa ya Afya na Ubora wa Utunzaji (NICE) mwanamke mmoja kati ya 12 anaripoti dalili za prolapse lakini anapochunguzwa hutokea katika hadi asilimia 50 ya wanawake wote.
Utafiti ambao bado haujachapishwa na Chuo Kikuu cha Stirling unaonyesha kwamba aibu, ukosefu wa ufahamu na hofu kwamba dalili hazitachukuliwa kwa uzito, yote ni vikwazo kwa wanawake kutafuta msaada kwa matatizo ya afya ya fupanyonga.
Utafiti huo uliangalia tafiti kutoka nchi 24 zikiwemo Uingereza katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, ukichukua maoni ya zaidi ya wanawake 20,000.
Watafiti Clare Jouanny na Dk Purva Abhyankar walisema: "Kuna idadi kubwa ya ushahidi kutoka Uingereza na nchi kama hizo ulimwenguni kote kwamba wanawake bado wanakabiliwa na vizuizi vingi linapokuja suala la kutafuta msaada kwa maswala ya afya ya wanawake kama vile prolapse.
"Tunahitaji kuzingatia sio tu kuongeza uelewa na elimu miongoni mwa wanawake na matabibu, lakini muhimu zaidi tunahitaji kufanya kazi na matabibu ili kubadilisha mtazamo wa wanawake kwamba matabibu hawawachukulii kwa uzito na dalili za afya ya fupanyonga."
Daktari wa viungo vya afya ya fupanyonga Suzanne Vernazza yuko kwenye dhamira ya kuwaelimisha wanawake kuhusu afya yao ya nyonga. Yeye ndiye mwanzilishi wa kampuni isiyo ya faida ya Know Your Floors na mafunzo yake ya kila siku ya 'SqueezeAlong' ya sakafu ya fupanyonga yana zaidi ya wafuasi 600,000 kwenye TikTok.
Anasema ni muhimu kwa watu kuzungumzia masuala ya afya ya fupanyonga na daktari wao.
"Ikiwa umekuwa unahisi kitu ambacho wakati wowote haujisikii sawa kabisa, iwe ni mjamzito au baada ya kuzaa, uliza swali kwa sababu zaidi ya uwezekano, uko sahihi kwamba sio sawa - na unaweza kupata msaada kwa wakati ufaao.Chuo cha Royal Doctors kilisema madaktari wake wamefunzwa vyema kutambua na kutunza watu walioathiriwa na prolapse.
Naibu mwenyekiti wa RCGP Scotland Dr Chris Williams alisema: "Madaktari wa afya wanafahamu aibu au unyanyapaa unaoweza kuhusishwa na hali hii na kujitahidi kuhakikisha wanawake wanajisikia vizuri na kuwezeshwa kutafuta msaada ikiwa wanapata dalili."
Sam Hindle alipata tatizo la kuporomoka kwa kibofu baada ya kuzaliwa kwa mtoto wake wa kiume miaka 24 iliyopita na amekuwa hajiwezi tangu wakati huo.
"Ilikuwa mbaya sana kwamba mwanangu wa miaka miwili alilazimika kwenda kunichukua suruali safi," alisema. "Ilikuwa aibu kuwa na mtoto wako wa miaka miwili kukimbia na kusema 'Oh Mummy amepata ajali, nahitaji kumsaidia'."
Mama huyo mwenye umri wa miaka 47, kutoka Edinburgh, alikuwa mmoja wa makumi ya maelfu ya wanawake nchini Uingereza kufanyiwa upasuaji wa matundu ya uke ili kutibu prolapse .
Utumiaji wake ulisitishwa nchini Uingereza mnamo 2018 kwa sababu ya mabadiliko ya maisha ambayo wanawake wengi walipata. Sam alisema alikuwa ameachwa katika maumivu ya mara kwa mara na anaugua PTSD kama matokeo ya tiba hiyo
Anatumai kuwa kifa nyenye nyavu alichowekewa kitaondolewa na mtaalamu nchini Marekani na kwa sasa yuko kwenye orodha ya wanaosubiri kufanyiwa tathmini huko Glasgow. Alisema ni muhimu kwa watu kuzungumza juu ya afya ya fupanyonga.
"Kama ukomo wa hedhi, ni somo ambalo tunahitaji kuondoa unyanyapaa na kuzungumza juu yake na watu wasione aibu juu ya hili kwa hivyo wataenda kutafuta msaada," alisema.
"Unawaangalia wanawake wengine katika familia ambao wanapata watoto na unafikiri, 'Afadhali niwaonye, bora nihakikishe wanajua kuhusu mazoezi ya sakafu ya fupanyonga na wanajua jinsi ya kuepuka uwezekano wa kuingia kwenye matatizo niliyopata hasa kwenye kibofu."
Natashja alisema prolapse huathiri wanawake wa rika zote na haina ubaguzi.
"Niligundua dalili zangu nilipokuwa na umri wa miaka 18 na nilipoenda kwenye Google ilikuwa ikiniambia tu kwamba wanawake wazee waliathiriwa," alisema.
"Madaktari walishtuka sana kwamba mtu wa rika langu alikuwa na prolapse na ilinifanya nijisikie kutengwa sana."
Natashja alisema sasa anahisi ana matumaini kuhusu siku zijazo.
Amekuwa akifanya kazi na mtaalamu wa afya ya fupanyonga na anatumia tiba za uke, kifaa kinachosaidia kutegemeza kuta za uke na viungo vya fupanyonga, kumaanisha kwamba anajiamini zaidi kufanya mazoezi.
Alisema msaada na ushauri wa jumuiya ya mtandaoni pia umemsaidia kukabiliana na hali hiyo.
"Ikiwa umegunduliwa tu kuwa na prolapse, ni muhimu kujua sio lazima kupitia hii peke yako," alisema.
"Kuna jeshi la wanawake huko tayari kukusaidia katika safari yako na wanaweza kuelewa kile unachopitia na kukusaidia katika hilo."
Imetafsiriwa na Yusuf Jumah