WARIDI WA BBC : ‘Nilitolewa mfuko wa uzazi nikiwa na umri wa miaka 27’

    • Author, Anne Ngugi
    • Nafasi, BBC Swahili

Ni simulizi ya barabara yenye ‘miiba’ ambayo Caroline Ng’ang’a kutoka Kenya aliipitia . Akiwa na umri wa miaka 26 mwaka wa 2012 aliamua kujipa zawadi ya kipekee , zawadi yenyewe ilikuwa ni kufanyiwa kipimo maarufu( Pap-Smear) ambacho hufanywa na wanawake kama ukaguzi wa kina katika sehemu za uke au kizazi chao ilikuhakikisha hakuna saratani inayoathiri maeneo hayo Alikuwa amepata changamoto kuu kwani marafiki wake kadhaa walikuwa wanafanyiwa vipimo hivyo

Na kwa hivyo Carol alipoamka asubuhi kabla ya msimu wa krisimasi mwaka wa 2012 aliingia kwenye hospitali mmoja na kukusanya ujasiri wa kufanyiwa vipimo hivyo , baada ya hapo anasema alichukua mwezi hivi kabla ya kuelekea hospitalini kuchukua matokeo yake .

”Sikuwa na sababu yeyote ya kwanini nilichukua matokeo yangu kuchelewa , ila ndivyo hivyo , mapema mwaka uliyofuata wa 2013 nilirejea kuchukua vipimo vyangu. Hali ilikuwa tofauti na nilivyotarajia , pindi nilipoitisha matokeo hayo , niligundua kuwa wahudumu waliokuwa sehemu ya kupokea wageni wakiwa na hofu nilipowaitisha matokeo yangu”anakumbuka Carol

Mwanadada huyu alipewa matokeo ya kutamaushwa , kwani wahudumu walimueleza kwamba alikuwa na chembechembe za saratani kwenye njia yake ya uzazi .Carol hakuamini alichokuwa anakisikia alichofanya ni kurejea nyumbani kwake na kunyamaza kwa siku mbili bila kuzungumza na yeyote kuhusu hali hio, anasema kwamba ni kama alikuwa ameganda akili kwa muda huo

Matokeo ya Saratani ya kizazi yalivyomvunja

Mwanadada huyu anasema kwamba licha ya kupewa matokeo hayo hakuyaamini mara moja cha kwanza alichofanya ni kuingia kwenye mitandao ili kujisomea ilimaanisha nini kuwa na saratani kwenye njia ya uzazi , ni hali ambayo anasema ilimuogofya kwani dalili zilizokuwa zimeandikwa pamoja na sababu za mwanamke kupata saratani hio zilikuwa zinampa wasiwasi aidha aliamua kufanya vipimo vengine katika vituo vitano vya kiafya ili kudhibitisha iwapo kulikuwa na dosari katika matokeo ya kwanza .

”Niliamua kutembelea madaktari watano tofauti , ambao sikuwaambia shida yangu. Nilichosema ni kwamba nilihitaji vipimo vya saratani katika kizazi changu.Cha ajabu ni kuwa matokeo ya vituo hivyo vya afya hayakutofautiana na matokeo ya kwanza .Nimefunzwa kuwa mwanamke ngangari kila wakati na kwa hio nilijikaza na kuwa mgumu hata zaidi licha ya kupewa matokeo kama hayo ”anasema Carol

Carol anasema kwamba , hatua ya kwanza kwanza ya kuowaona madaktari tofauti , ilimtishia sana kwani mmojawapo ya wataalam wa afya aliowaona wakati huo alimweleza ana kwa ana kwamba kulikuwa na dharura ya kizazi chake chote kuondolewa kwa haraka .

”Mojawapo ya wataalam niliyowaona mara za kwanza baada ya kugundua nilikuwa na saratani , aliniambia bila hata tone la hofu kuhusu dharura ya kukatwa kwa sehemu zote za kizazi changu, nilipomuuliza Je ? unafahamu mimi bado ni msichana alicheka na kusema mbona una wasiwasi na hili ? hata mimi ni mtoto wa kipekee kwa mama yangu ”Carol anakumbuka

Mwanadada huyu anasema kwamba taswira aliyokuwa anapewa kulingana na yeye ni kwamba alikuwa azoee kwamba wanawake kila siku wanakatwa sehemu za uzazi na ni jamboo la kawaida ila kwake haikuwa kawaida .

Mwanadada huyu anasema kwamba ndoto yake ilikuwa kujaaliwa watoto 7 , hapo awali alikuwa amejaaliwa mtoto wa kike kabla ya masaibu haya yakuwa na saratani yampate , na sasa aliona ndoto hio ikididimia kuanzia mwaka wa 2013 .

Alihangaika kumtafuta muhudumu ambaye angemshika mkono na kumsaidia kuelewa aliokuwa anayapitia, kwa bahati nzuri alikumbana na mtaalam wa saratani ya kizazi kwa wanawake ambaye anasema alikuwa malaika wakati huo

”Nakumbuka kwa mara ya kwanza nilipata daktari ambaye alinieleza kwamba hakuwa tayari kuona nikipoteza uhai wangu kutokana na saratani , daktari wangu aliniambia nilikuwa bado mchanga kufariki! Nilihisi kwa mara ya kwanza kwamba kulikuwa na mtu ambaye alikuwa ananielewa ”Carol anakumbuka

Uamuzi wa kutolewa kizazi

Uamuzi wa kutolewa kwa sehemu yote ya kizazi changu ulifanywa kwa dharura na kwa haraka , baada ya pandashuka za kufanyiwa uchunguzi mbalimbali katika sehemu za nyungu ya uzazi na pia kwenye mlango wa kizazi iliamuliwa kwamba kuishi kwangu kungetegemea kutolewa kwa sehemu hizo anakumbuka Caro

Tarehe ambayo hajawahi kuisahau ni Machi 23 mwaka wa 2013 ndio alipofika hospitalini na ndio siku alipotolewa sehemu hizo , Carol alifahamu fika kwanzia wakati huo maisha yake yangebadilika sana .Ilikuwa ndio mwanzo wa kukoma kwa hedhi yake kabisa , na kukoma kwa maisha ya kawadia ya mwanamke mwenye mihemko ya kawaida pasipo shida zinazoandama wanawake wenye umri wa makamo ambao hupitia (MENOPAUSE) kipindi ambacho huwa na mabadiliko mengi ya mwili na hisia zao .

Mwanadada huyu anasema kwamba licha ya kwamba kizazi kilitolewa akiwa na umri wa miaka 27 , kipindi ambacho wanarika wenzake wanajaliwa watoto na wanafurahia umri huo yeye alikuwa anapambana na mabadiliko hayo , ila alichukua mkondo wa kuwasaidia wanawake wengine ambao wanapitia hayo Carol alijiuzulu kazi aliyokuwa ameajiriwa ilikubeba majukumu ya kuwa kipao mbele katika kuwasaidia na kutoa elimu kwa wanawake kuhusu saratani ya kizazi .

”Nilianza kutembea wanawake hospitalini na kuwakumbatia tu , nilifanya hivyo kwasababu nilipokuwa nauguza vidonda vya kukatwa sehemu za kizazi changu nilikuwa natamani kukumbatiwa na nilikuwa nahisi upweke usio na kifani , ndiposa nilielewa mihemko ambayo wanawake waliokuwa wanapitia hali kama yangu walivyokuwa ”anakumbuka mwanadada huyu

Kutokana na hayo alifanikiwa kufungua kituo cha kina mama wenye saratani , shirika ambalo linawaleta kina mama pamoja katika hali ya kutiana moyo , kusaidiana wakati mtu amelemewa pamoja na kutoa mafunzo mbalimbali kuhusu saratani.

Huduma ya Carol haikuishia hapo alihisi kwamba wanawake kama yeye ambao wameyapitia hayo wanatakikana wale vyakula ambavyo vinarotuba ya kutoka kwa mchanga , ndiposa alichukua fursa ya kujielimisha kuhusu vyakula mbalimbali vinavyotoka mchangani na manufaa yao kwa mwili wa binadamu.

Kama anavyosema maisha ni pandashuka na kwa hali zote amepitia siku ambazo alikuwa hajielewi , siku ambazo zilikuwa zimejaa kiza kikuu asijue kwa kupindukia hali kadhalika anasema kwamba amekuwa na siku ambazo zimejaa matumaini hasa kupitia huduma nyingi ambazo anahusika nazo za kuwasaidia wanawake na jamii.