Mkasa wa wasichana wa miaka 15 na 16 waliojiunga na IS

c

Chanzo cha picha, Emma Jones

Maelezo ya picha, Mtengeneza filamu Kawthar Ben Haniyeh kutoka Tunisia aliteuliwa kuwania tuzo ya Oscar kwa filamu yake ya "Mabinti wa Olfa."
    • Author, Emma Jones
    • Nafasi, BBC

Rahma na Ghofran Al-Sheikhawi wanaonekana wadogo katika filamu ya "Mabinti wa Olfa." Ni nyuso zao tu na hijabu nyeusi ndivyo vinavyoonekana kutoka kwa wasichana hao wawili.

Wanatokea Tunisia, walikuwa na umri wa miaka 15 na 16 walipojiunga na Islamic State (Dola la Kiislamu), kundi la kigaidi kwa serikali nyingi duniani.

Filamu hiyo iliyoongozwa na mtu-Tunisia, Kawthar Ben Hania, iliteuliwa kuwania tuzo ya Oscar katika kipengele cha makala (documentary) .

Ben Hania kwa mara ya kwanza aliteuliwa katika kipengele cha Filamu ya Kimataifa - mwaka 2021, kwa filamu yake ya "The Man Who Sold His Skin," ambayo inaangazia hadithi ya mkimbizi wa Syria aliyejiuza kwa michoro yake mwilini kwa ajili ya kupata viza ya Schengen.

Filamu ya "Mabinti wa Olfa" inahusu hadithi ya Ghufran na Rahma Al-Sheikhawi, Iya, Tayseer, na mama yao Olfa. Inasimulia matukio ambayo yalipelekea dada wakubwa kujiunga na Dola ya Kiislamu.

Mwanzoni, Ben Hania anasema, alivutiwa na kile kinachoweza kumchochea msichana kujiunga na kundi kama hilo. Aliambia BBC:

"Tumezoea wanaume hufanya hivyo, lakini jambo jipya katika hili ni kwamba wanawake pia wamejihusisha na ugaidi, na nadhani nilitaka kuelewa kwa nini wasichana nao hujiunga.”

Moja ya jambo ambalo nililiona kuwa la ajabu ni kwamba Ghufran na Rahma walikuwa wakitafuta uhuru. Walitaka uhuru kutokana na mateso ya mama yao. Kwa hiyo, nilitaka kuelewa jinsi hamu ya kupata uhuru inavyoweza kukuongoza kwenye njia kama hiyo. "

Ripoti ya 2018 ya Chuo Kiku cha King's College London inakadiria kuwa raia 4,761 wa kigeni walijiunga na shughuli za ISIS nchini Iraq na Syria kati ya 2013 na 2018.

Kama Ben Hania, vyombo vya habari pia vinavutiwa na wazo la magaidi wa kike. Msichana Mwingereza Shamima Begum, alijiunga na ISIS alipokuwa na umri wa miaka 15, alinyang'anywa uraia wa Uingereza, ingawa mawakili wake walikata rufaa dhidi ya uamuzi huo kwa madai alishawishiwa na kundi hilo.

Ben Hania anasema, "kuna vichwa vya habari, lakini ni kipi kipo nyuma ya vichwa hivi? Hapa ndipo filamu inapoingia."

Pia Unaweza Kusoma

Unyanyasaji wa Kutisha

z

Chanzo cha picha, TWENTY TWENTY VISION

Maelezo ya picha, Aliwakutanisha waigizaji na mama halisi wa wasichana ili mama aweze kusimulia hadithi yake
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mkurugenzi wa filamu hiyo, Ben Hania, anasema filamu hiyo sio hadithi ya kutunga, ingawa waigizaji wapo, nafasi za uigizaji ni ndogo sana kwenye filamu na waigizaji wanafanya kama wahusika wenyewe."

"Nilitaka kuirikodi kwa muda mfupi, lakini niligundua haitakuwa ya kuvutia. Nilihitaji kuingia ndani zaidi katika mkasa huu," anaongeza.

Kwa hiyo aliwaleta pamoja waigizaji na Olfa, mama halisi na binti zake wawili, ili waweze kuwashauri waigizaji kuhusu kumbukumbu zao na kile kilichotokea.

"Ni mazungumzo kati ya mwigizaji na mhusika halisi. Ni hadithi ya myororo wa mateso kutoka kwa mama hadi kwa mabinti zake. Mama huyo anaita - laana."

Kinachoonekana katika maisha yao, ni kwamba Olfa Al-Hamrouni (mama wa watoto hao) alikumbana na unyanyasaji akiwa msichana. Baadaye, Olfa, analea binti zake peke yake, anakuwa mkali dhidi ya wasichana wake.

Ghofran alipopaka rangi nywele zake na kunyoa miguu yake, Olfa alimpiga. Mwishoni mwa filamu, Olfa anamwambia Kawthar Ben Haniyeh alikuwa kama paka anayekula watoto wake kutokana na hofu.

Anasema, “sikuwala, lakini niliwapoteza.”

sdc

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Walikuwa na umri wa miaka 15 na 16 wakati wasichana hao wa Tunisia walipojiunga na Islamic State

Ben Hania anaeleza: “Yale Olfa aliyopitia alipokuwa mtoto, aliwafanyia mabinti zake, na anaelewa urithi huu wa unyanyasaji ulivyoathiri mabinti zake pia.”

Ben Hania anasema Ghofran na Rahma pia walikuwa vijana wakati wa kuenea kwa itikadi kali, na baada ya mapinduzi ya Tunisia 2011 na kuibuka kwa Dola ya Kiislamu.

Watu wengi wa Tunisia walivutiwa na wazo la kujiunga na shirika huko Libya, Iraq na Syria. Inakadiriwa Watunisia 6,000 walijiunga na kundi hilo kufikia 2015.

Majina ya Ghofran na Rahma Al-Sheikhawi yaliingia kwenye vichwa vya habari nchini Tunisia mwaka 2015 ilipobainika wamejiunga na ISIS.

Olfa pia alionekana kwenye televisheni ya Tunisia, akisema alitoa taarifa kwa mamlaka kwamba mabinti zake wamekuwa na itikadi kali (kufikia kuomba Rahma afungwe ili kumzuia asitoroke), na akakamatwa. Lakini baadaye wakaenda Libya.

Mwaka 2023, walihukumiwa kifungo cha miaka 16, na binti wa Ghufran mwenye umri wa miaka minane, Fatima, anakulia katika gereza la Libya na mama yake.

Ben Hania anasema filamu yake inaonyeshwa katika kumbi za sinema nchini Tunisia, takriban miezi sita baada ya kuachiliwa kwake.

Anasema mpango ulikuwa ama kuruhusu akina dada hao kuhukumiwa nchini Tunisia, au kumruhusu Fatima, binti wa Ghufran, kuondoka gerezani, lakini hadi sasa majaribio haya hayajafaulu.

Jambo la kuhuzunisha zaidi katika filamu hii ni pale dada mdogo wa dada hao alipoulizwa angewaambia nini dada zake ikiwa angewaona tena, akasema: "Familia hii iliyowaangamiza, sitairuhusu iniangamize.”

Pia Unaweza Kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Dinah Gahamanyi